Advertisements

Monday, January 22, 2018

WAZIRI MPINA AKIPIGA FAINI YA SHILINGI MILIONI 100 KIWANDA CHA SUNFLAG


Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Sunflag cha mjini Arusha, Ajay Shah, akiongoza zoezi la kuchoma  nyavu haramu za dagaa zilizo chini ya sentimita 8 (marobota 584) zenye jumla ya shilingi milioni mia moja zilizokamatwa kwenye Kiwanda chake na Kikosi Kazi Maalum cha Kutokomeza Uvuvi Haramu nchini  kilichoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwenye dampo la  takataka nje kidogo ya jiji la Arusha leo.(Na John Mapepele)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (mwenye kofia) akikagua chumba cha baridi cha kuhifadhia samaki (Cold room) cha kampuni ya Alpha Choice mjini Arusha  leo  akiwa katika operesheni  maalumu ya kudhibiti uvuvi haramu kulia ni mmliki wa kampuni hiyo Yussuf Khatry. (Na John Mapepele)
Marobota 584 ya nyavu haramu yaliyotengenezwa na Kiwanda cha Sunflag cha mjini Arusha yenye thamani ya shilingi milioni 100 wakitekea kwenye dampo nje ya jiji la Arusha leo. Marobota hayo alikamatwa na Kikosi Kazi Maalum cha Kutokomeza Uvuvi Haramu nchini  kilichoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina ambapo uteketezaji huo uliongozwa na mmliki  wa kiwanda hicho Ajey Shah(Na John Mapepele)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (mwenye kofia) akisikiliza taarifa ya ukamataji wa marobota 584 ya nyavu haramu yaliyotengenezwa na Kiwanda cha Sunflag cha mjini Arusha yenye thamani ya shilingi milioni 100  kutoka kwa kiongozi wa Kikosi Kazi Maalum cha Kutokomeza Uvuvi Haramu nchini  West Mbembati aliye kulia, kushoto mwakilishi wa Afisa Tawala wa Mkoa wa Arusha David Lyamongi. (Na John Mapepele)
  • Mmiliki wa kiwanda aongoza zoezi la kuteketeza nyavu zilizokamatwa kwenye kiwanda chake.
Na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina  amekitoza  faini ya Shilingi milioni mia moja Kiwanda cha Sunflag  Tanzania Limited cha jijini Arusha  baada ya kukutwa na makosa  mawili ambayo ni kuzalisha na kuuza nyavu bila kuwa na leseni kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuzalisha na kuuza nyavu ambazo ziko kinyume na matakwa ya Sheria ya Uvuvi  namba 22 ya mwaka 2009.
Kulingana na maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Ajay Shah, kiwanda kimekuwa kikitengeneza  vyavu hizo haramu kwa miaka mitatu mfululizo sasa ambapo inakadiliwa kuwa tayari kimeshatengeneza tani  1296 nyavu hizo  zenye thamani ya shilingi bilioni nne.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mpina, Kiongozi wa kikosi kazi cha kutokomeza  uvuvi haramu katika kanda ya Ziwa Victoria, West Mbembati amesema kuwa tarehe 17/1/2018 walifika kwenye kiwanda hicho na kukamata marobota 584 yenye thamani ya milioni mia kufuatia  maelekezo ya Waziri Mpina yaliyotolewa Mjini mwanza hivi karibuni baada ya mfanyabiashara Dastan Venanti kukamatwa na nyavu hizo zenye thamani ya milioni sitini na tano ambazo nyaraka zilionyesha alinunua katika kiwanda hicho.
Akipokea taarifa hiyo Waziri Mpina alisema mkakati uliopo kwa sasa ni kuwabaini watengenezaji na wasambazaji wote wa zana haribifu za uvuvi ikiwa ni pamoja na vyavu zisizoruhusiwa kisheria ambapo amesema hatua za kali za kisheria dhidi yao zitatumika ili kudhibiti uvuvi haramu kwenye  maji(mito,maziwa na bahari) ya nchi yetu.
“Operesheni ya kuwabaini na kuwachukulia hatua wafanya biashara wakuu wanaofadhili na kuendeleza  biashara ya uvuvi haramu ni ya kudumu ambapo mkakati uliopo  sasa ni kuwanyang’anya na kuwafutia lesseni zao za biashara” alisisitiza Mpina
Aliwaonya wafanyabiashara wanaosafirisha  samaki na mazao yake katika nchi za jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kongo wanaotishia kugoma ambapo amesisitiza kwamba hatua waliyoichukuwa ni ndogo badala yake waachane kabisa na biashara hiyo kwa kuwa wamekuwa wakikwepa kodi na kuikosesha  Serikali mapato yake kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Ajay Shah alikiri kutenda makosa hayo na kueleza kuwa  kiwanda kimekuwa kikiendelea kutengeneza vyavu hizo bila kujua kuwa kilikuwa hakizingatii sheria  za Uvuvi ambapo alisema kimekuwa kinauza nje ya nchi hususan kwenye soko la Nairobi nchini Kenya  na Mwanza
Aliwataja baadhi ya wateja wake wakuu  wa mkoani Mwanza kuwa ni pamoja na Dastan Venant, Morice Otieno na Majani Masagati  ambao wote walikamatwa hivi karibuni na nyavu zisizoruhusiwa kisheria  na kikosi kazi cha kudhibiti uvuvi haramu kilichoundwa na Waziri Mpina na kutozwa faini ya jumla ya shilingi milioni 120 huku vyavu hizo zikitaifishwa na kuteketezwa mara moja.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo aliongoza zoezi la kuteketeza  nyavu hizo haramu kwa kushirikiana na Waziri na Watendaji  mbalimbali wa Serikali katika dampo la kuwekea takataka nje kidogo ya jiji la Arusha huku akikiri kuwa  atazingatia taratibu zote za Serikali katika kutengeneza nyavu zinazoruhusiwa kisheria ambapo alisema tayari wameshapeleka barua Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupata kibali cha kutengeneza nyavu.
Aidha Waziri Mpina ametoa siku tatu kwa Watendaji wa Wizara yake  kumempatia kibali cha kutengeneza nyavu hizo kwa mujibu wa sheria za nchi. Kulingana na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 kibali hicho kinatolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi.

1 comment:

Anonymous said...

Hapakuwa na namna nyingine ya kubadilisha matumizi ya nyavu hizo ,ili isiwe hasara kwa pande zote mbili serikali na mwekezaji?