Advertisements

Monday, January 22, 2018

TAARIFA KWA UMMA

Image result for ssra logo
TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KWA WATUMISHI WA UMMA, 2017(THE PUBLIC
SERVICE SOCIAL SECURITY FUND ACT, 2017), KUHUSIANA NA
MASUALA YA KODI, MAFAO YA MAJAJI NA MAFAO
YATAKAYOTOLEWA KWA WATEGEMEZI


Kumekuwa na tafsiri potofu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (The Public Service Social Security Fund Act, 2017), inayotolewa aidha kwa bahati mbaya au kwa lengo la kupotosha maudhui ya Muswada huo kuwa unakusudia kutoza kodi mafao ya Wastaafu, kubagua Wajane na kuathiri mafao ya Majaji.
Tunapenda kuutaarifu Umma na Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa ujumla kwamba tafsiri hiyo siyo sahihi na ni upotoshaji mkubwa na kwa misingi hiyo tunapenda kutoa taarifa na ufafanuzi kama ifuatavyo:
1.0. Serikali haijawahi na wala haikusudii kutoza kodi Mafao ya Wanachama na wala si malengo ya kifungu cha 56 cha Muswada huu. Ni vema ifahamike kwamba hata katika Sheria za sasa za Mifuko ya Pensheni na Sheria za Kodi, mafao ya wanachama hayatozwi kodi, rejea kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Mfuko PSPF, kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Mfuko wa GEPF, kifungu cha 90(2) cha Sheria ya Mfuko wa NSSF na kifungu cha 54 cha Sheria ya Mfuko wa PPF. Aidha, masharti na maudhui ya kifungu cha 56 cha Muswada yanafanana kabisa na masharti ya vifungu tajwa hapo juu vikisomwa pamoja na sheria za kodi ambazo ndiyo misingi wa misamaha yote ya kodi nchini.



2.0. Masharti kuhusu mafao ya Majaji yamechukuliwa kutoka kwenye Sheria ya Mfuko wa PSPF ambako ni vifungu vya 21 na 22 vya Sheria Hiyo. Hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwenye maudhui ya vifungu hivyo zaidi ya kuboreshwa kwa kutenganisha masharti ya Pensheni na stahili nyingine. Hivyo taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu mafao ya Majaji ni upotoshaji wa makusudi unaolenga kujenga taswira potofu mbele ya macho ya Jamii.

3.0. Eneo la mafao ya Wajane na warithi katika Muswada ni moja ya maeneo ambayo yameboreshwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na masharti yalivyo kwenye Sheria za sasa. Muswada umebainisha kwa uwazi stahili za Wajane na Warithi pale mwanachama au mstaafu anapofariki.

Tunawashauri na kuwaasa wananchi na Taasisi nyingine kuepuka kutoa maoni ambayo yanalenga kupotosha nia njema ya Serikali katika Muswada huu.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846 Tovuti: www.ssra.go.tz
Dar es Salaam

22/1/2018

No comments: