Advertisements

Monday, October 23, 2017

STATOIL: BILA MTAMBO WA KUSINDIKA, UCHIMBAJI WA GESI HAUTAKUWA NA TIJA KWA TANZANIA

Meneja Mkazi wa Statoil, Øystein Michelsen, akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa Mtambo wa Kusindika Gesi ya Kimiminika (LNG) wakati wa warsha ya siku moja ya waanahabari (hawapo pichani) iliyofanyika kwenye makao makuu ya kampuni hiyo, Masakini jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya uelewa wa sekta ya mafuta na gesi iliyoandaliwa na kampuni ya Statoil Tanzania katika ofisi zake zilizoko Masaki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa taasisi ya Environmental Media Agenda – EMA, Secelela Balisidya (kushoto), akibadilishana mawazo na mwandishi mwandamizi, Nelson Goima, kabla ya kuanza kwa warsha ya uelewa wa sekta ya mafuta na gesi iliyoandaliwa na Statoil na kuratibiwa na taasisi yake na kufadhiliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Duniani (WWF).

Na Daniel Mbega
KAMPUNI ya utafiti na uchimbaji wa gesi ya Statoil ya Norway imesema serikali inapaswa kuona kipaumbele cha kufikia makubaliano ya kujengwa kwa mtambo wa kusindika gesi ya kimiminika (Liquified Natural Gas – LNG) kwa faida ya usafirishaji wa gesi hiyo kwenye soko la kimataifa pamoja na matumizi ya ndani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na kampuni yake, Meneja Mkazi wa Statoil, Øystein Michelsen, alisema mtambo wa LNG ndio utakaosaidia kuchakata na kusindika gesi hiyo ili kurahisisha kuisafirisha nje.
“Huwezi kusafirisha gesi katika hali yake ya kawaida, ni lazima kuisindika kwa kuibadili kuwa katika hali ya kimiminika, hivyo mtambo wa LNG una umuhimu mkubwa kwa biashara ya gesi kwa kusafirisha kwenye soko la kimataifa pamoja na matumizi ya ndani,” alisema Michelsen.
Statoil na mshirika wake ExxonMobil wamefanya ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika visima vya Zafarani, Lavani, Tangawizi, Piri, Giligilani na Mronge katika Kitalu namba 2, chenye eneo la takriban kilometa za mraba 5,500, ambalo lipo umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka ufukweni katika kina cha maji kati ya meta 1,500 hadi 3,000.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, Statoil na ExxonMobil vilevile wanafanya kazi kukuza maeneo mengine tarajiwa katika kitalu hicho na wamekamilisha upatikanaji wa taarifa za kitaalam katika maeneo hayo, ambapo kwa mujibu wa Michelsen, wanatarajia kuchimba kisima kingine kuanzia Januari 2018.
Katika warsha hiyo iliyofanyika kwenye makao makuu ya kampuni hiyo, Masakini jijini Dar es Salaam na kuratibuwa na taasisi ya Environmental Media Agenda (EMA) na kudhaminiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori (WWF), ilielezwa kwamba, umuhimu wa kujenga mtambo huo utasaidia kuongeza mapato ya taifa, kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa wazawa na kukuza uchumi.
“Tunaangalia namna ya kuzungumza na serikali kuona watachukua hatua gani na lini kuruhusu ujenzi wa mtambo wa LNG, serikali haijaamua kwa kuwa inaonekana kama iko bado iko kwenye maandalizi ya kanuni na taratibu hasa baada ya kupitishwa kwa sheria mpya za gesi na mafuta, hata hivyo inapaswa kuangalia vipaumbele ili kufanikisha mradi huu,” aliongeza Michelsen.
Mapema mwaka huu wa 2017, serikali ilisema kwamba mtambo huo wa LNG utajengwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, katika ujenzi wa mtambo wa LNG, gharama zote zitalipwa na wawekezaji wakati serikali jukumu lake ni kutoa ardhi mahali mtambo huo utakapojengwa.
Kampuni ya Statoil na mshirika wake ExxonMobil ya Marekani ambazo zinamiliki Kitalu namba 2 kwa asilimia 65 na 35 mtawalia ambazo zimegundua kiasi cha futi za ujazo trilioni 22 kwenye eneo hilo, ziliingia ushirika na kampuni za BG (Shell), Ophir na Pavillion zinazomiliki vitalu namba 1 na namba 4 ili kujenga mtambo huo.
Shughuli hiyo ya pamoja itakuwa ya kwanza nchini ambako hadi sasa akiba ya gesi yenye futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 imegundulika nchini kote. 
Hata hivyo, ratiba ya utekelezaji wa mradi huo bado haijawekwa wazi ingawa tayari eneo maalum la ujenzi wa mtambo huo limekwishapatikana mkoani Lindi na taarifa zinasema tathmini inatakiwa kufanyika ili kuwalipa fidia wananchi pamoja na kuwatafutia eneo jingine.
Statoil na BG walipendekeza mtambo wa gesi ya kimiminika ujengwe eneo la Likong’o-Mchinga kusini mwa mji wa Lindi.
Tayari serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta za mraba 2,071.705 (ekari 5,119) katika Kijiji cha Likong'o kusini mwa mji wa Lindi katika mwambao wa bahari ya Hindi, takriban kilometa 460, kwa barabara, kusini mwa Dar es Salaam. Huo ni umbali wa kilometa 103 kaskazini-masharibi mwa mji wa Mtwara, ambao uko jirani.
Kwa mujibu wa mkataba, MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, pamoja na kuisafirisha katika soko la kimataifa, lakini asilimia 10 ya gesi itakayopatikana itasambazwa kwa matumizi ya ndani ya nchi, na serikali inaweza kuuza ziada kwa nchi jirani zenye uhitaji.
Mkuu wa kitengo cha uwezeshaji cha Statoil, Profesa Richard Rwechungura, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, gesi iliyowekwa katika hali ya kimiminika (LNG), ni safi, isiyo na rangi, yenye kimiminika kisicho na sumu, inayotengenezwa kwa kuipoza gesi ya asili kufikia kipima joto cha Sentigredi -163°, ambapo inakuwa kimiminika na husindikwa hadi mara 615 ya gesi iliyo katika muundo wa hewa. 
“Mchakato huu hufanywa ili kurahisisha usafirishaji wa gesi asilia uwe na ufanisi zaidi kwa kutumia maroli au meli,” alisema.
Zaidi ya hayo, gesi ya kimiminika hailipuki katika mazingira yasiyodhibitiwa, kwa hiyo, katika hali isiyotegemewa ya kumwagika kwa gesi ya kimiminika, gesi hiyo inakuwa na uwezekano mdogo wa kutoa mlipuko.

Faida nyingine za gesi ya kimiminika inajumuisha ukweli kwamba mchakato wa kuifanya kimiminika unapunguza oksijeni, carbon dioxide, salfa na maji kutoka kwenye gesi hiyo, inayofanya gesi hiyo kuwa karibu na metheni asilia. Gesi hiyo ikifikishwa mwisho wa safari yake, huifadhiwa katika hali yake ya kimiminika hadi inapotiwa joto tena kurudi katika hali yake ya gesi ya asilia.

No comments: