Advertisements

Monday, August 21, 2017

Benki ya Standard Chartered kulipa bilioni 50 kesi ya IPTL

SAKATA la malipo ya Dola za Kimarekani 168, 800,063 (takribani 400bn / -) dhidi ya kampuni mbili za Kitanzania limechukua sura mpya mara baada ya kampuni hizo kugeuza kibao na kutaka benki mbili za Standard Chartered kuweka dhamana mahakamani ya shilingi billioni 50.

Kampuni hizo, Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP), zimewasilisha maombi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kusaka amri hiyo dhidi ya Standard Chartered Bank Hong Kong Limited na Standard Chartered Bank Malaysia Berhard.

Katika maombi namba 241/2017 yaliyowasilishwa mahakamani wiki iliyopita, IPTL na PAP wanaomba benki hizo za kigeni ziamriwe kuweka dhamana hiyo kabla ya kusikizwa shauri lilofunguliwa kupinga kusajili hukumu ya kigeni ya Uingereza inayohusu malipo hayo ya Dola za Kimarekani 168, 800,063.

Maombi hayo yameungwa mkono na hati ya kiapo iliyowasilishwa na wakili wa kampuni hizo, Joseph Makandege. Jaji Barke Sahel anayesikiliza shauri la kupinga kusajiliwa hukumu iliyotolewa Novemba mwaka jana na Mahakama Kuu ya Biashara ya Uingereza, amepanga kusikiliza maombi hayo Octoba 10.


Katika hati yake ya kiapo, Makandege ameeleza kuwa benki hizo mbili ni mali za kigeni na zimesajiliwa nchini China na Malaysia na kwamba hazina mali yoyote hapa Tanzania ambayo inaweza kufidia gharama zitakazotumiwa na wateja wake kuendesha shauri hilo hapa nchini.

Ameeleza kuwa hadi leo hakuna miongoni mwa maafisa wa juu kutoka benki hizo ambao wamesaini nyaraka au kukumbukumbu zozote zilizowasilishwa mahakamani kupinga shauri hilo na hivyo itakuwa vigumu kwa IPTL na PAP kuwataka maofisa hao kuwajibika kwa kile kitakachotokea baade.

Makandege amebainisha kuwa wakili anayezitetea benki hizo za Standard Chartered Bank Hong Kong na Standard Chartered Bank Malaysia Berhard ameshindwa kuonyesha mahakamani au kwa wateja wake uhalali wa kuendelea kusimamia shauri hilo au kufungua mashauri yoyote kwa niaba ya benki hizo.

Ameendelea kueleza kuwa hata nchi kule benki hizo zilikotoka hazina mikataba au utaratibu na Tanzania wa kutekeleza hukumu zinazotolewa na mahakama za nchi hizo hapa nchini, kitendo ambacho kinaweza kuzihakikishia IPTL na PAP kulipwa gharama watakazozitumia baada ya shauri hilo kufika mwisho.

Makandege amefafanua kuwa kiwango cha fedha kinachodaiwa na mabenki hayo dhidi ya wateja wake ambacho ni Dola za Kimarekani 168, 800,063, sawa na 376,424,142,274/- ni kikubwa, hivyo inahitajika gharama kubwa na haijaonyeshwa kama IPTL na PAP wamesamehewa kulipa gharama ya kujitetea.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya kiapo, mabenki hayo yamekuwa na mwenendo wa kubadili misimamo na wakati mwingine kuondoa au kufuta mashauri waliyokwisha fungua mahakamani na hivyo kuwafanya walalamikiwa kuingia gharama kubwa za kujitetea bila msingi wowote.

Makandege ameeleza pia kuwa kulingana na kile alichokieleza kwenye hati yake ya kiapo kwa ujumla wake, hukumu ya nje inayotaka kusajiliwa imeghubikwa na makosa mengi na hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kutokubaliwa na mahakama za hapa nchini.

Alikumbushia kuwa hata IPTL, PAP na VIP Engineering and Marketing Limited zilipokuwa zinapambana huko Uingereza ziliamriwa kuweka dhamana kwa ajili ya gharama za mabenki hayo kujitetea kwa kampuni hizo hazikuwa zimesajiliwa huko na wala kuwa na mali yoyote inayoweza kufidia gharama hizo.

Katika shauri la msingi, makampuni hayo yanaomba mahakama kutengua amri iliyotolewa Februari 9, 2017, kusajili hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Malkia Uingereza, Idara ya Mahakama ya Biashara ya Novemba 16, 2016 juu ya malipo hayo.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Flaux baada ya kusikiliza upande mmoja inazinufaisha benki hizo mbili. Makapuni hayo yanaomba mahakama itamke kuwa hukumu ya kigeni iliyosajiliwa mbele ya Jaji Barke Sahel haisajiliki na wala haitekelezeki nchini Tanzania.

No comments: