Advertisements

Wednesday, March 22, 2017

Mahakama yamweka huru Manji kesi ya Uhamiaji

Yusuf Manji
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeamuru mfanyabiashara Yusuf Manji ambaye alikuwa kizuizini chini ya Idara ya Uhamiaji, kuachiwa huru chini ya dhamana aliyopewa kwenye kesi namba 63 ya kutumia dawa za kulevya iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Manji aliondoka mahakamani hapo na kuingia katika hoteli moja maarufu jijini Dar es Salaam akiwa na mlinzi wake.

Hatua hiyo imekuja baada ya jopo la mawakili wa mdai, Alex Mgongolwa, Alex Musumbushi na Jeremiah Ntobesya kuieleza mahakama kuwa mteja wao anashikiliwa na polisi kwa siku 30.

Mgongolwa alidai Manji akiwa Hospitali ya Aga Khan walikuwepo askari sita waliokuwa wanamlinda na kwamba hata jana aliletwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi.

Pia alidai katika kiapo cha Ofisa wa Uhamiaji, Arnold Munuo amekiri kwamba alimchukulia maelezo Manji, hivyo ni kweli kwamba wanamshikilia.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Osward Tibabyenko alidai kuwa maofisa hao wa polisi hawamshikilii Manji, hatua ambayo Jaji Ama Munisi alitaka kujua ukweli kuhusu suala hilo.

Jaji Munisi aliutaka upande wa mdai kuleta vielelezo vya kuthibitisha kama kweli mshitakiwa alikuwa kizuizini.

Aidha, aliamuru Manji kuwa huru kwa dhamana aliyoipata katika kesi namba 63 ya mwaka huu ambayo ni ya kutumia dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia alisema maombi hayo yatasikilizwa Machi 27, mwaka huu na kiapo kuhusu kuthibitisha kama kweli Manji aliwekwa kizuizini itapelekwa Machi 24, mwaka huu.

Mgongolwa alidai watawasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo ya wafanyakazi wa Aga Khan hospitali na majina ya askari waliokuwa wakimshikilia Manji ili kuthibitisha suala hilo.

Katika kesi hiyo wajibu maombi hayo ni Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Katika maombi hayo, yaliyopelekwa mahakamani hapo na Wakili Hudson Ndusyepo, alieleza kushangazwa na kitendo cha mteja wake kuwekwa chini ya ulinzi na Idara ya Uhamiaji akiwa Hospitali ya Aga Khan ambapo anashikiliwa isivyo halali, hivyo wanaiomba mahakama kumwachia huru.

Manji alikuwa chini ya ulinzi baada ya kuachiwa kwa dhamana, Februari 20, mwaka huu alipopelekwa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa na kuhojiwa kwa madai ya kuingiza wageni nchini kinyume cha sheria.

Wakili wa Manji, Ndusyepo alifungua kesi ya maombi hayo, akitaka mahakama iagize maofisa uhamiaji na polisi kumfikisha mahakamani ili iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kuagiza aachiwe.

Katika hati ya maombi hayo, Ndusyepo anadai kuwa alimtembelea mteja wake Hospitali ya Aga Khan, Februari 17, mwaka huu na kukuta maofisa wa uhamiaji wakimsubiri mteja wake wampeleke kwa ofisa uhamiaji mkoa kwa mahojiano dhidi ya tuhuma siyo raia wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Ndusyepo, Manji amedai kuwa alitoa maelezo kwa maofisa uhamiaji na alirudishwa Aga Khan ambako yupo chini ya ulinzi hadi sasa.

Katika kesi inayomkabili Kisutu, Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, mwaka huu akidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu, katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin, ambayo aliachiwa kwa dhamana ya Sh milioni 10.

HABARI LEO

No comments: