Advertisements

Friday, January 20, 2017

Gavana BoT asifu mafanikio Kagera Sugar

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu akimsikiliza Mchumi kilimo wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera (KSL) wakati alipotembelea kiwanda hicho wilayani Missenyi mkoani Kagera juzi. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa KSL, Seif Seif. (Na Mpigapicha Wetu).
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ametembelea mashamba na Kiwanda cha Sukari ya Kagera Limited (KSL) na kupongeza mafanikio ambayo kampuni hiyo imeyapata.

Katika ziara yake hiyo, Profesa Ndulu, alipatiwa taarifa fupi kuhusu utendaji wa kiwanda hicho ikiwemo mipango yake ya kuongeza uzalishaji.

Akizungumza na menejimenti ya kiwanda hicho, aliipongeza kampuni hiyo kwa kufanya mageuzi makubwa ya uzalishaji ikiwemo mpango wa KSL wa kuwaongezea ujuzi wafanyakazi wake.

Kiwanda hicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ya programu mbalimbali ikiwemo teknolojia za kisasa za uzalishaji wa sukari na maendeleo ya ufundi stadi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KSL, Ashwin Rana alisema kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani 68,000 za sukari msimu huu, ingawa kumekuwa na tatizo la ukame tangu mwaka jana.

Alielezea mipango na mikakati ya kukuza kiwanda hicho ya miaka mitano, kuwa ina lengo la kuoneza uzalishaji ili kuendana na nia ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania iwe nchi ya kujitegemea ifikapo 2021.

Alisema kiwanda hicho kinatarajia kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi, maji na rasilimali watu ili kuiwezesha sekta sukari kuimarika lakini pia kukifanya kiwanda hicho kiwe kinaongoza nchini kwa uzalishaji wa sukari.

Naye Mwenyekiti wa kiwanda hicho, Seif Ally Seif, alimuomba Gavana Ndulu huyo kufuata mfano wa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa sukari, kwa kuwawekea masharti nafuu ya kifedha wawekezaji.

Kwa upande wake, Profesa Ndulu, alipongeza rekodi nzuri ya uzalishaji wa kiwanda hicho na kuihakikishia Menejimenti ya KSL kuwa atayafanyia kazi mambo yao ili kuwasaidia kukuza sekta hiyo. Alisema endapo serikali itawasaidia wafanyabiashara wa sukari, itasaidia kutengeneza ajira, kuingiza fedha za kigeni na kukuza viwanda.

HABARI LEO

No comments: