Advertisements

Monday, September 26, 2016

IPTL, PAP waungana na Tanesco kupinga kuilipa Standard Chartered

Sakata  la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kugeuziwa kibao kwa kutakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 216.2 kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limezidi kuchukua sura mpya baada uongozi wa kampuni hiyo kuibuka.

Kuibuka kwa viongozi hao kumekuja siku chache baada ya Wakili wa Tanesco, kueleza hatua watakazochukua kuhusu uamuzi huo baadaya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID), uliotolewa Septemba 12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti ambaye pia ni Mwanasheria wa Kampuni  wa IPTL,  Joseph Makandege alisema hawatambui madai ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) kama mdai na wala hawana haki kwa mujibu wa sheria.

Kutokana na hali hiyo alisema inaungana na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukata rufaa katika Mahakama ya ICSID kwani hukumu iliyotolewa ina mapungufu mengi ya kisheria.

Licha ya uamuzi huo Makandege alisema IPTL haikulipwa kwa kutumia viwango vya zamani bali walilipwa kutokana na umeme waliouuza kwa Tanesco na si vinginevyo.

Alisema watu wasifanye makosa kuilipa benki hiyo kwani inachotaka kufanya ni kitendo cha utapeli kwa msukumo wa kampuni za mabeberu.

“Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong hawastahili kulipwa fedha na Watanzania kwani hawastahili kwa mujibu wa sheria nasi kama IPTL/PAP hatuwatambui na hawana haki ya kutuzungumzia. Na ndiyo maana wameamua kukimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje, hawa wana msukumo wa mabeberu wenye nia ovu.

“Kwa uamuzi huu wenye utata uliotolewa na ICSID ni wazi Standard Chartered walikuwa na nia ovu, ninasema hivyo kwa sababu tangu Septemba 5, mwaka 2013 suala hili liliamuriwa vizuri chini ya Jaji Utamwa (John) na IPTL ikashinda kesi na kutwaa uongozi.

“Na hili si la kwanza kwani Aprili 3, 2014  tulifungua shauri namba 60 chini ya Jaji Dk. Fauz Twalib la kuitaka Mahakama itamke kwamba  benki ya Standard Chartered Hong Kong si wadeni wetu, tena awali waliibuka na hoja kwamba hawasikilizwi na Mahakama zetu za ndani kwa wakati  ambapo shauri hilo lilipangiwa kusikilizwa mfululizo.

“Lakini pia dai letu lingine tuliomba Mahakama Kuu itupe nafuu ya Standard kutulipa gharama kama fidia ya Dola za Marekani bilioni 3.240 ambapo hata tuzo waliopewa na ICSID eti wanataka walipwe Dola za Marekani milioni 148 na kama wakitulipa fedha zetu hata madai yao yaingia humo nabado kuna fedha nyingine inabidi watupatiwe sisi,” alisema Makandege

Wakili huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa IPTL/PAP, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini, alisema licha ya mahakama kutoa uamuzi wataendelea kusimamia uamuzi huo wa kutomtambua mtu anayeitwa Martha Renju wala Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

“Sisi msimamo wetu kama IPTL/PAP tunasema hadharani kwamba hatuitambua Benki ya Standard Chartered ambao hawa kila wakati wamekuwa wakikimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje na hata hukumu hii ya tuzo ina viashiria vya mabeberu.

“Tuzo husika waliyopewa ni dhahiri Standard Chartered ni batili kwa mujibu wa sheria. Wao ni kina nani hadi wakafungie kesi kwa niaba yetu. Hii ni kesi ya ngedere imepelekwa kwa nyani,” alisema

Kutolewa fedha za Escrow
Akizungumzia mchakato wa kutolewa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Makandege alisema mchakato wa kutolewa kwa fedha hizo ulikuwa wa kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema Julai 5, mwaka 2006, Serikali na IPTL waliingia mkataba wa Escrow ambao ulipelekea kutolewa kwa fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bila kuwahusisha Benki ya Standard Chartered.

“Oktoba 8, 2010 IPTL na Tanesco kwa kuzingatia kipengele cha 10 cha mkataba huo ambayo kinaeleza kuwa endapo kuna mgogoro baina ya pande hizo mbili wahusika watakutana na kujadiliana  na hatua ya kuafikiana itahesabika kuisha kwa mgogoro.

“Hata ripoti mbalimbali ikiwemo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hakuna sehemu yoyote inayoeleza kuwa zile fedha ni za umma. Hata ICSID imetoa hukumu na kusema si fedha za Serikali lakini wanakiri zilitolewa kihalali ingawa hawakupewa Standard na kama kungelikuwa na mgogoro fedha zile singetolewa,” alisema

Kunyang’anywa mitambo
Alipoulizwa kuwa hatua ya suala hili kugubikwa na utata na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge la 10 likiwemo la wao kunyang’anywa mtambo, Makandege alisema wanajua kuna watu hivi sasa wanahaingika wakitaka kuona suala hilo linafanyika.

Pamoja na hali hiyo alisema kuwa mitambo bado ni mali yao kwa mujibu wa sheria na hakuna hatua itakayowafanya wafanikiwe watu hao ambao hakuwataja.

“Tunajua kuna watu hivi sasa wanataka kuona suala hili likitekelezwa ikiwemo IPTL kunyang’anywa mtambo, ninawaambia hakuna jambo kama hilo, nasi kila wakati tumekuwa wazi ikiwemo kulaani maazimio ya Bunge ambayo ni wazi yalikuwa na lengo la kukimbiza wawekezaji wazawa. Suala hili hata Rais mstaafu (Jakaya Kikwete) aliliweka wazi kwa nini lianze sasa baada ya mjadala wake kufungwa,” alisema.

No comments: