Advertisements

Monday, September 26, 2016

BODABODA MIRERANI WATAKIWA KUJIPANGA KULIPIA LESENI YA USAFIRISHAJI

Mkuu wa Kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Evarest Makala akizungumza juzi na wamiliki na madereva wa pikipiki katika warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra). 
Wamiliki na madereva wa pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani manyara, wakiwa katika warsha iliyoandaliwa juzi na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra). 

Mmoja wa wamiliki wa pikipiki Abubakary Sadiq akizungumza juzi mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Mnayara kwenye warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).


MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amewataka wamiliki na madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kujiandaa kulipia mapato kupitia leseni ya usafirishaji wa abiria.

Mhandisi Chaula aliyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, akizungumza na wamiliki na madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kwenye semina iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).

Alisema wanapaswa kujiandaa na ulipaji wa leseni ya usafirishaji itakayoanza kutozwa hivi karibuni kwani haikwepeki, hivyo wajipange kwa ajili hiyo ili wachangie mapato ya nchi, ambayo inalenga kujitegemea.

“Hivi karibuni tutawapa taarifa ya kuanza kwa zoezi hilo ila sasa subirini kidogo kwani hii ni serikali ya awamu ya tano inayotaka kujitegemea kupitia mapato ya wananchi na siyo kuomba misaada nje ya nchi,” alisema Mhandisi Chaula.

Afisa mfawidhi wa Sumatra mkoani Manyara, Nelson Mmari alisema lengo la kukutana na bodaboda hao ni kuhakikisha kila mmiliki anakuwa na leseni ya usafirishaji inayotolewa kupitia halmashauri ya wilaya husika.

Mmari alisema Machi 2009, Bunge lilipitisha sheria ya kuruhusu pikipiki za magurudumu mawili au mitatu kubeba abiria kwa malipo au kukodisha na iliyoanza kutumika mwaka 2010 hivyo leseni ya usafirishaji inapaswa kulipiwa.

Alisema kila mtu anapaswa awe na leseni ya usafirishaji wa biashara ya kubeba abiria wa pikipiki ya magurudumu mawili au matatu na  atakayekiuka atatozwa faini ya kati ya sh50,000 au sh100,000 au kufungwa jela miezi sita au mwaka.

Alisema mkuu wa wilaya ya Simanjiro aliwaelewesha vizuri wamiliki na madereva wa bodaboda kuwa wajiandae na zoezi la ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwani zoezi hilo linatarajia kuanza hivi karibuni kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake, mkuu wa askari polisi wa usalama barabarani wa mkoa wa Manyara, Mary Kipesha, alisema wanasubiri taarifa ya mkuu wa wilaya hiyo ili waanze zoezi la ufuatiliaji ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwa bodaboda.

“Tunasubiri mazungumzo hayo ila mjiandae na ninyi kwani baada ya hapo ndipo tutaanza ukamataji kwa wale ambao watakuwa hawajalipa leseni ya biashara ya kubeba abiria kwa wenye bodaboda hapa Mirerani,” alisema Kipesha.

No comments: