Advertisements

Tuesday, July 26, 2016

KOFFI OLOMIDE AHUKUMIWA MIEZI 18 JELA KWA KOSA LA KUMSHAMBULIA DANSA WAKE

Mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) Koffi Olomide leo amehukumiwa kifungo cha jela miezi 18 kwa kosa la kumshambulia moja wa madansa wake jijini Nairobi juzi.

Mahakama moja mjini Kinshasa imetoa hukumu hiyo leo baada ya mwanamuziki huyo kukamatwa wakati akiwa nyumbani wake. Alipangiwa kutumbuiza mashabiki wake Bomas of Kenya Jumamosi lakini tamasha hiyo ikaahirishwa.

Olomide alikamatwa Ijumaa usiku na maofisa wa polisi wa Kenya na siku iliyofuata asubuhi akaingizwa kwenye ndege na kurejeshwa Kinshasa. Katika hatua nyingine, waandalizi wa tamasha ambalo Olomide alipangiwa kutumbuiza nchini Zambia pia walitangaza kufuta hafla hiyo kutokana na yaliyotokea Nairobi.

Mwanamuziki huyo, akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumapili, aliomba radhi mashabiki wake na hasa “wanawake na watoto”. “Najutia sana yaliyotokea… kilikuwa ni kipindi kifupi cha wenda wazimu,” aliambia kituo cha televisheni cha taifa cha RTNC.

Baadaye, aliomba msamaha kutoka kwa raia wote wa DRC ambao huenda alihisi kwamba tabia yake iliwavunjia heshima.

Waziri wa masuala ya vijana na jinsia Kenya, Sicily Kariuki katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya video iliyoonyesha tukio hilo kusambaa, alipendekeza Olomide azuiwe daima kutembelea Kenya.

No comments: