Advertisements

Friday, May 27, 2016

NECTA SASA KUFUNGA MITIHANI KWA KUTUMIA MASHINE.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 20016/2017 mjini Dodoma.(Picha kutoka maktaba)


Na Fatma Salum-MAELEZO, Dodoma.
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limejipanga kuanza kufunga bahasha zenye karatasi za mitihani kwa kutumia mashine maalum ili kuondokana na hatari ya kuvuja kwa mitihani hiyo na gharama za ufungaji wa mitihani kwa kutumia mikono.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2016/2017, jana Bungeni Mjini Dodoma.

Prof. Ndalichako alisema kuwa katika kuimarisha utendaji kazi wake NECTA itanunua mashine mbili za kufunga mitihani (Auto Poly Wrapping and Packing Machine) ili kuimarisha usalama wa mitihani kwa kupunguza watu wanaoshiriki kwenye maandalizi ya mitihani hiyo.

“Katika mwaka 2016/2017 Baraza litasimika mashine mbili za kufunga bahasha za mitihani hivyo kuondoa hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuwa idadi ya watu wanaofanya kazi hiyo itapungua.” alisema Prof. Ndalichako.

Aidha, Prof. Ndalichako aliongeza kuwa Baraza litaboresha mfumo wake wa ukusanyaji na uchakati takwimu na kuweka Mfumo wa Kielektroniki wa kumtambua mwanafunzi kwa namba maalum tangu anapoandikishwa shuleni hadi atakapomaliza mzunguko wa masomo yake.

Alisema kuwa mfumo huo wa utambuzi utaunganishwa nchi nzima ili kuwezesha kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi kwenye shule yoyote atakayoenda kusoma ndani ya nchi kwa kuwa namba hiyo atakayopewa na Baraza ataitumia hata kwenye shule nyingine atakazohamia.

“Wizara itaweka Mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji taarifa za wanafunzi chini ya Baraza la Mitihani ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo wakati wa mitihani na utaratibu huu utapunguza matumizi makubwa ya fedha kupitia mfumo wa TSM9.” alisema Prof. Ndalichako.

Pia alieleza kuwa katika kufanikisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), mwaka wa fedha uliopita Mamlaka ya Elimu Tanzania imechapisha vitabu 558,720 vya jinsi ya kujibu mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne ili kuwawezesha wanafunzi watahiniwa kujibu maswali vizuri katika mitihani yao hatimaye kuongeza ufaulu.

No comments: