Advertisements

Saturday, April 30, 2016

MAPENDEKEZO YA SHERIA YA WAZEE KUWASILISHWA BUNGENI

NAIBU WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema Serikali imekamilisha mapendekezo ya uundwaji wa Sheria ya Wazee ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Septemba.

Dk. Kigwangalla aliyasema hayo jana (Ijumaa, Aprili 29, 2016) wakati akitoa ufafanuzi kwa Viongozi wa Mtandao wa Wazee waliomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma.

Dk. Kigwangalla alisema kuwepo kwa Sheria ya Wazee kutawezesha mambo mbalimbali yanayohusu wazee kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo likiwemo suala la pensheni.
“Mimi pamoja na Waziri wangu, Ummy Mwalimu baada ya kupewa jukumu la kuongoza wizara tuliunda kikundi cha wazee kwa ajili ya kuamua mambo makubwa mawili ambayo tutayatekeleza likiwemo la pensheni kwa wazee wote,” alisema.
Naibu Waziri huyo alisema suala jingine ambalo wamepanga kulitekeleza ni utoaji wa huduma ya bure kwa wazee, ambapo watawapatia bima ya afya ili wasiendelee kusumbuka.

Kwa upande wake Waziri Mkuu aliwahakikishia wazee hao kwamba Serikali inawatambua na ndiyo sababu ya waliamua wawe na sehemu ya kufikishia malalamiko yao ambayo ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto .

Kuhusu ombi la wazee hao kwa Rais Dk. John Magufuli la kuwa na uwakilishi Bungeni kwa kupitia nafasi zake 10 za uteuzi, Waziri Mkuu alisema amelipokea na atalifikisha kwa Mhe. Rais.

Pia amewataka wapanue taasisi yao na kuimarisha mtandao uweze kujulikana na wazee wengi zaidi, wawe na viongozi kuanzia ngazi za vijiji ambapo Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa karibu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na utoaji wa huduma za afya kwa wazee katika hospitali mbalimbali alizotembelea na kukuta yameanzishwa madirisha maalumu ya kuhudumia.

Akizungumzia kuhusu suala la wazee kupewa elimu ya mapambano dhidi ya UKIMWI aliwataka waandaaji wa matamasha na semina za mafunzo hayo kujumuisha watu wote wakiwemo wazee.

Naye Mwenyekiti wa mtandao huo , Bw. Sebastian Bulegi alisema lengo la kumtembelea Waziri Mkuu ni kumuomba awafikishie shukurani zao kwa Rais Dk Magufuli kwa kuwapatia wizara maalumu inayoshughulikia masuala yao.

“Vile vile shukurani hizi tufikishie kwa mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli kwa kufanya wazee kuwa agenda yake ya kwanza na tayari ameshatembelea makazi ya Nunge Kigamboni (Dar es Salaam) na Bukumbi (Mwanza),”alisema.

Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na wajumbe wanane wa mtandao huo unaoundwa na Asasi 26 za wazee katika ngazi za wilaya na mkoa kutoka mikoa ya Kigoma, Tanga, Arusha, Mwanza, Lindi na Dodoma, aliiomba Serikali isimamie kutokomeza mauaji ya wazee.

Ombi jingine alilolitoa kwa Serikali ni utekelezwaji wa Sera ya Wazee ya mwaka 2003, Sera ya Matibabu bure kwa wazee, mafunzo ya kupambana na UKIMWI pamoja na uwakilishi katika ngazi za kutoa maamuzi.

Pia wazee hao wamemhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamekubali ombi linalotolewa na viongozi wakuu wa nchi la kuwataka wawaombee ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980, DODOMA.
JUMAMOSI, APRILI 30, 2016.

No comments: