Advertisements

Tuesday, November 24, 2015

Watu 829 wauawa na wananchi wenye hasira


ASIFIWE GEORGE NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

WATU 829 wameuawa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu kutokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alisema matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yameongezeka, ikilinganishwa na mwaka jana katika kipindi kama hicho ambapo watu 785 waliuawa kwa matukio kama hayo.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa tabia hiyo inaendelea kujengeka na kuonekana kama ni jambo la kawaida, wakati ni ukiukwaji wa taratibu na sheria za nchi.

Bulimba alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi, linatoa onyo kali kwa watu wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi, na kwamba yeyote atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Endapo mwananchi ataona uhalifu au wahalifu katika eneo lake, atoe ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa ili hatua za haraka za ukamatwaji ziweze kufanyika.

“Mwananchi yeyote atakayefanikiwa kurekodi tukio la watu wanaojichukulia sheria mkononi na kutufikishia kwa siri, sisi kama polisi tutampatia donge nono.

“Sheria inamruhusu mwananchi kukamata mhalifu na kumfikisha katika dola na si kujichukulia sheria mkononi kwa kumpiga, kumuua au kumdhalilisha mbele za watu,” alisema Bulimba.

Alisema jeshi hilo limewaagiza makamanda wote nchini kufanya ukamataji wa watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kisingizio cha hasira.

Bulimba alisema mtu yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Aliwataka wananchi wote kuheshimu na kufuata sheria za nchi ili kudumisha amani, usalama na utulivu kwa sababu kufanya hivyo kutasaidia vyombo vyenye mamlaka ya utoaji haki kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila kuingiliwa kwa kisingizio cha hasira kali.

“Hatutamfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kuhusika na uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi, hivyo tutakayemkamata tutamuwajibisha ipasavyo kwa mujibu wa sheria,” alisema Bulimba.

Mtanzania

1 comment:

Anonymous said...

It about time they do something...this was getting out of hand.