Advertisements

Friday, November 20, 2015

Mke: Mtikila alikabwa koo hadi kufa

ELVAN STAMBULI NA MAKONGORO OGING

Dar es Salaam

Asimulia mazito tena, apeleka waraka kwa rais Magufuli

Georgia Mtikila: “Nguo zake alizovaa siku aliyofariki dunia, hazijulikani zilipo, waliotuma picha za maiti mtandaoni, washindwa kupatikana, sakata lafika kwa Magufuli…”

“Madaktari waliomfanyia uchunguzi kule katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha nao walijichanganya nilipokwenda kupata habari ya uchgunguzi wao”…

“Nakumbuka Ijumaa jioni aliniambia kuwa anakwenda Njombe kwenye kampeni. Democratic Party (DP) ilikuwa na mgombea kule. Sikumkubalia”…

MKE wa marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, Georgia Mtikila anasema anaamini kifo cha mumewe kilichotokea Novemba 4 mwaka huu hakikusababishwa na ajali

kama ilivyoripotiwa. Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum nyumbani kwake Mikocheni B, Dar es Salaam, mama Mtikila anasema mumewe walimnyonga kisha kumtupa eneo linalodaiwa kutokea ajali. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

MWANDISHI:Unaweza kutufahamisha siku Mchungaji Chrisopher Mtikila alipokuwa anakwenda safari ya Njombe, muliagana vipi?

MAMA MTIKILA: Ilikuwa safari ya ghafla sana. Nakumbuka Ijumaa jioni aliniambia kuwa anakwenda Njombe kwenye kampeni. Democratic Party (DP) ilikuwa na mgombea kule. Sikumkubalia. Nilimwambia kwamba hakuna haja ya kwenda Njombe badala yake kama ana fedha angetuma kwa viongozi wa DP waliokuwa Mwanza ili waende Kigoma ambako nako kulikuwa na mgombea wetu.

MWANDISHI: Baada ya kumwambia hivyo, Mchungaji Mtikila alisema nini?

MAMA MTIKILA: Alikataa kuahirisha safari akasema nimuandalie vitu vidogovidogo vya kusafiri navyo. Nilimuandalia mswaki na dawa ya meno, sabuni, nikamuwekea kwenye begi. Alisema hatakaa, atakwenda na kugeuza kurudi siku ya pili yake. Nilimshauri tena kwamba kama ni kwenda ni bora aondoke na gari kubwa (basi) kwa kuwa nilimwambia safari za usiku ni mbaya. Alikataa.

MWANDISHI: Alikuambia anakwenda Njombe kwa gari gani?

MAMA MTIKILA: Aliniambia kuna gari imekodishwa na James Manyahi, akaniambia alikuwa na shilingi laki sita ambazo zingetosha kwa bajeti ya safari yake.

MWANDISHI: Wakati mnazungumzia safari hiyo alikuambia atasafiri na akina nani?

MAMA MTIKILA: Alisema atakwenda na Patrick Mgaya ambaye alinitambulisha kama mlinzi wake binafsi na madereva wawili, hivyo safari itakuwa na watu wanne.

MWANDISHI: Uliridhika na kuwaamini watu hao?

MAMA MTIKILA: Kwanza wakati wa kushuka ghorofani (nyumbani kwao) tulikuwa wawili na begi lake la safari nilikuwa nimelichukua mimi. Tulipofika chini na kukuta gari dogo, Patrick Mgaya alitaka kunipokea lile begi, sikumpa, nikaliweka kwenye gari. Sikutaka alishike kwa sababu maalum. Mchungaji akasema kuna madereva wawili. Niliuliza, kwa nini madereva wawili? Hakunipa jibu.

MWANDISHI: Je, uliwashuhudia wakiondoka?

MAMA MTIKILA: Hapana. Nililiagana naye nikawaacha palepale nje ya nyumba yetu wakizungumza. Mimi niliingia ndani kwa ajili ya kujiandaa na mkesha, kila Ijumaa huwa tunakesha tukisali.

MWANDISHI: Siku ya tukio, yaani taarifa za kifo zilikufikiaje?

MAMA MTIKILA: Nilipigiwa simu na Mgaya, sikuamini na hata sasa ni kama siamini.

MWANDISHI: Huyu Patrick Mgaya alitoka wapi? Ni ndugu yake mchungaji?

MAMA MTIKILA: Huyu bwana anatoka Mlangali, Njombe na mume wangu alikuwa ni mtu wa Miro, Njombe, walikuwa ndugu, naambiwa alikuwa askari na nikaambiwa ni mlinzi binafsi wa mchungaji.

MWANDISHI: Baada ya kifo cha Mchungaji Mtikila, Patrick Mgaya amewahi kuja hapa kwako kukufariji na kukusimulia ajali ilivyotokea na kusababisha kifo cha mumeo?

MAMA MTIKILA: Hajawahi kukanyanga hapa na hicho ndicho kinachonishangaza.

MWANDISHI: Je, huwa mnawasiliana kwa simu?

MAMA MTIKILA: Hatuwasiliani na nimebaki nashangaa kwa sababu enzi mchungaji akiwa hai, Mgaya alikuwa akija hapa saa 12 asubuhi, sasa amekata mguu.

MWANDISHI: Nguo alizokuwa amevaa mchungaji baada ya ajali hazikuonekana kuwa na damu, unazungumziaje kuhusu hilo?

MAMA MTIKILA: Ni kweli nguo zile hazikuwa na damu. Madaktari waliomfanyia uchunguzi kule

katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha nao walijichanganya nilipokwenda kupata habari ya uchunguzi wao. Kwanza waniambia mbavu zake saba zilipasuka lakini baadaye wakabadilika, wakaniambia mbavu hizo zilikuwa zimevunjika. Nikawauliza mbavu saba

zivunjike zisitokeze nje, inawezekana? Hawakunijibu tena.

MWANDISHI: Ulikwenda polisi kufuatilia sakata hili?

MAMA MTIKILA:Nilikwenda polisi Kibaha, nikaenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania, nikaonana na maofisa pale lakini wakawa wanasisitiza kwamba eti kifo kile kilitokana na ajali ya kawaida. Nikiwauliza maswali walikuwa wananifokea.

MWANDISHI: Baada ya kuambiwa hivyo, uliridhika na majibu hayo?

MAMA MTIKILA: Sijaridhika na sitaridhika mpaka watu waliomuua mume wangu sheria ifuate mkondo wake. Mimi naamini mchungaji walimniga (kumkaba), wakamuua, maana hata kwenye koo niliambiwa kulikutwa na mate mengi, walimniga hawa, amekufa kifo cha maumivu makali sana..…(analia).

MWANDISHI: Pole sana mama. Sasa umechukua hatua gani ya ziada?

MAMA MTIKILA: Nilifanya juhudi ya kuonana na Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa madarakani tena kwa msaada wa Msajili wa Vyama vya Siasa, ikashindikana. Novemba 2 mwaka huu nilikwenda Ikulu kupeleka barua yangu kwa Rais John Magufuli. Katika barua hiyo nimemueleza ukweli kwamba mtandao umemuua mchungaji na umeteka kila sekta na kuharibu ufahamu wa polisi na kuwafanya wasijali kujua ukweli juu ya mauaji ya mpendwa wetu. Nikamsihi atusaidie kuunda tume ili ukweli ujulikane.

MWANDISHI: Kwa nini unaamini kwamba Mchungaji Mtikila aliuawa?

MAMA MTIKILA: Naamini hivyo kwa sababu aliwahi kuhojiwa katika kipindi cha Tuongee katika runinga moja Septemba 25 mwaka huu na akazungumza tena Septemba 27 mwaka huu katika kipindi hichohicho alifuatwa na watu (anawataja watu waliowahi kuwa na nyadhifa nzito nchini) kutaka wamtumie kisiasa akakataa licha ya kumuahidi fedha nyingi, ndipo walipomtishia kumuua. Akiwa Bunda kwenda Mwanza Septemba mwaka huu, gari lake lilifuatiliwa usiku akanipigia simu kuniarifu, lakini akafanikiwa kulikwepa.

MWANDISHI: Mara baada ya tukio lile lililotajwa kuwa ni ajali iliyomuua licha ya wewe kukataa, picha ya maiti ya Mchungaji Mtikila ilisambaa kwenye mitandao. Uliwahi kufuatilia kujua zilitumwa na nani kwa mara ya kwanza?

MAMA MTIKILA: Nilikwenda Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) wakaniambia hawawezi kufanya kazi hiyo mpaka wapate kibali cha polisi. Polisi nilikwenda kulalamikia hilo, lakini wakapuuza.

Kilichonifanya kwenda kuwaomba Mamlaka ya Mawasiliano itusaidie kumjua mtu aliyeweka picha zile alfajiri kuonesha maiti ya mchungaji ni kutaka kujua alikuwa wapi wakati huo au ndiyo wauwaji, kwamba walifanya hivyo kutoa taarifa kwa ‘waajiri’ waliowatuma kuonesha kuwa kazi wameikamilisha?

MWANDISHI: Neno lako kwa Watanzania.

MAMA MTIKILA: Ukweli na haki ni vya Mungu, hakuna awezaye kuzuia. Tunategemea Mungu atawatumia watendaji wa serikali wenye nia njema na kwa ajili ya nchi yetu ili Mchungaji Mtikila apewe haki ya wauaji wake kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nitahangaika kila sehemu ili haki itendeke. Lakini wapo wote wanaoeneza habari kwamba kuna daktari mmoja anahusika na kifo hiki, watu hao tunawafahamu.

GPL

No comments: