Advertisements

Saturday, October 10, 2015

Slaa: Rais wangu ni Dk Magufuli

Slaa: Rais wangu ni Dk Magufuli
KATIBU Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema anamkubali kwa asilimia 90 mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akisema anafaa kwa nafasi hiyo kwa kuwa ni jasiri na ana uwezo wa kupambana na ufisadi.

Kutokana na sifa hizo, amesema endapo atakabidhiwa nchi, atasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti rasilimali za nchi na hivyo kuifanya nchi ipae kwa kasi kimaendeleo.

Alisema katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, kuna wagombea urais hawawezi kukemea ufisadi wala kuzungumzia kwa kuwa wao wenyewe sio wasafi, kwa kile alichoeleza ukiwa mchafu huwezi kupata ujasiri wa kumnyooshea mtu mwingine kidole.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha Star TV kijulikanacho kama Ajenda 2015 juzi, Dk Slaa aliyejiweka kando baada ya Chadema kupokea makada kutoka CCM wanaodaiwa si waadilifu, alisema kwa sasa anatafutwa Rais wa nchi, lakini mgombea asiyeweza kufafanua sera kwa kushindwa hata kuzungumza kwa dakika 10, hawezi kwenda kuongoza au watakaoongoza ni wasaidizi wake.

Dk Slaa alisema Chadema, chama ambacho awali kilikuwa kinapingana na ufisadi, kwa sasa hakina ajenda hiyo kutokana na kukaribisha wasio wasafi.

Alisema akiwa mpambanaji wa vitendo vya ufisadi, ambavyo vilisababisha kutishiwa kuuawa baada ya kutangaza ‘Orodha ya Mafisadi’ mwaka 2007, sasa anaungana na Dk Magufuli aliyethubutu kusema ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi, jambo linaloonesha ana dhamira ya kweli kwa kutaka kutimiza hilo kwa vitendo.

“Ukweli Magufuli ametokana na CCM na ana mapungufu kama binadamu, lakini ukilinganisha kati ya wagombea urais waliopo, yeye ana nafuu na anaonyesha dhamira ya kupigania serikali,” alisema.

Dk Slaa alisisitiza kuwa wakati huu mgombea urais yeyote anahitaji kuwa na wabunge wengi, lakini Magufuli anaonesha dhamira ya wazi kukataa ufisadi kwa kukataa kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake, wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo.

Alisema, akiwa Chadema mwaka 2010 walimlaumu Rais Jakaya Kikwete kwa kuwanyanyua mkono wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi, lakini mwaka huu, Dk Magufuli amekataa kufanya hivyo licha ya kuwa ni wagombea kutoka chama chake.

Akizungumzia vitendo vya rushwa na ufisadi, alisema rushwa ndogo zinaathiri wananchi kwa kuwafanya waishi kwa unyonge kuliko kubwa ambazo madhara kwa wananchi wa kawaida ni kidogo. Alisema anasikitika chama chake kilichopata umaarufu kwa ajenda ya rushwa na ufisadi na kusikiliza nyimbo za hamasa kupinga masuala hayo, sasa hawasikiki tena.

“Kwa sasa chama cha ACT ndiyo kimerithi vita ya rushwa na ufisadi na kubeba ajenda kila wanapopita,” alisema.

Alisema Magufuli ameonesha kwa matendo kuwa anayozungumza yanatoka moyoni na siyo mdomoni, kutokana na kutokuogopa kukosa kura za baadhi ya watendaji wanaotuhumiwa kuwa mafisadi.

“Kama anatekeleza leo hajapewa rungu na akipewa itakuwaje, kwani haogopi kupoteza kura kwani ufisadi upo kuanzia vijijini na vitongojini, hatua hiyo ni ujasiri wa ajabu sana kwa mgombea,” alisema.

Alibainisha kuwa kampeni siyo ushabiki wala shamrashamra, bali ni kuangalia viongozi bora kwa kuzingatia sera. Alisema yeye baada ya kusikiliza mikutano na kuangalia kwenye mitandao na kuzingatia mapambano dhidi ya ufisadi, amebaini hakuna mgombea atakayepambana na ufisadi kama Magufuli.

Akizungumzia suala la wagombea wawili wa vyama vya CCM na Chadema kuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, Slaa alisema kuna michakato inaendelea wakati huu wa kampeni, ikiwemo kupeleka watu katika mikutano na kutoa fedha.

Alisema hali hiyo imefanya iwe vigumu kupima ni nani anakubalika zaidi.

Alisema wapo wananchi wa aina tatu, kwamba wapo wanamjua wanayekwenda kumpigia kura, wengine wanafanya maamuzi kabla ya kampeni na wapo pia wanaofanya maamuzi kwa kubadilika pole pole mpaka mwisho wa kampeni.

Slaa pia alitahadharisha Watanzania kuwa Tanzania ni mama yao, ambaye hawezi kutokea mwingine, hivyo akichezewa, watu wote wataathirika na hawataweza kupata mwingine kama huyo.

Alitaka zifanyike kampeni zinazozingatia amani, kama zilivyofanyika mwaka 2010. Alisema ikiwa itatokea migogoro, hata wanaotangaza uongozi hawawezi kutawala makaburi, hivyo ni vyema kuzingatia misingi ya amani.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia sheria katika kusimamia uchaguzi na kuepuka kuwa sababu ya vurugu. Slaa alisema kamwe Watanzania wasikubali masuala ya kwenda Ikulu, kuleta balaa nchini bali kwa ujumla kuzingatia masuala ya kitaifa.

HABARI LEO

9 comments:

Anonymous said...

Kama yeye ni mungu basi na hiwe hivyo. Na kwanini yeye alikuwa anang'ang'ana ccm watoke madarakani au kwasababu ameambiwa atapewa uwaziri na magufuli. Hii inaonyesha nijinsi gani hawa viongozi walivyokuwa wanafiki na wanawaongopea walala hoi.

Anonymous said...

Suala muhimu siyo muda gani mtu anaweza kuongea kwenye jukwaa, la muhimu zaidi ni kamaanayo dira nzuri na uwezo wa kuongoza watu. Watanzania wamechoka na wazungumzaji wazuri kwenye majukwaa, aina ya akkina Castro au Hugo Chevez ambao wanweza kuongea zaidi ya masaa matano! Angalia Cuba, sasa hivi imeanza kukumbatia mageuzi na mabadiliko! Huwezi kung'ang'ania mfumo na uongozi wa mazoea na kufikiri kwamba utasonga mbele kama taifa. Kwa hivi sasa ni wachache wanofaidika na mfumo uliopo, na kama wengi wanataka mabadaliko usijaaribu kuzuia. Nimesikiliza mahojiano yote nahisi kwamba ubinafasi na maslahi ya mbele ya mhojiwa yalitangulizwa mbele. Nawahurumia Watanzania kwa mtaji huu wa kujaribu kudaanganywa na kugilibiwa wasifuate mkondo wa mabadiliko!!

Anonymous said...

sasa wewe anonymous wa 9:54am, hata kusoma hujui. kamuongopea nani hapo. yeye alichosema magufuli ameonyesha uwezo wa kukemea rushwa hadharani na kukataa kuwapigia kampeni wabunge walihusishwa na rushwa. sasa wewe lowasa anaweza kufanya hivyo wakati yeye ndio papaa fisadi. ndio maana slaa amesema magufuli anafaa sana kwa sababu sio mla rushwa niu msafi, pili anaweza kukemea na kuchukua hatua kama alivyoonyesha mfano. sasa huyo mgombea wa ukawa aliyetengewa billion 8 za kumsafisha anaweza hayo. acha uzandiki wako na ushabiki, nchi yetu inahitajii rais ambaye ataweza kuongoza sio handicap anayeandikiwa speech hata kusoma hawezi, kusimama dakika tano shida na hana sera yoyote zaidi ya kusema nipeni kura nachukia umaskini!!!!

Anonymous said...

Nilikua nakuamini kama iongozi bora chadema umekosa utakua umefikia ccm hii inaonesha dhahiri lengo lako ni uraisi bora Ungekaa bila chama ningekustahi .Heshima yako imeshuka




m

Anonymous said...

Ajenda pekee na nzito iliyo kinyanyua chama cha Chadema/Ukawa ilikuwa ni vita dhidi ya ufisadi na yeye kama kiongozi mmojawao aliyekuwa mstari wa mbele katika vita hii alisimama kidete kutaka kuitoa CCM madarakani kwa ajili ilihusishwa na tuhuma za kukumbatia mafisadi. Baada ya Chadema kupokea wahamiaji kutoka CCM ambao walikuwa wanatuhumiwa kuwa mafisadi na baada ya mabadiliko ya uongozi kufanyika, Dk Slaa aliamua kuhama chama hiki. Tangia mabadiliko ndani ya Chadema/Ukawa kutokea ajenda ya ufisadi ndani ya chama hiki imekufa na badala yake CCM imefufua na inaahidi kuifanyia kazi. Ukizingatia msimamao usioteteleka wa Dk Slaa katika swala hili ni maoni yangu kuwa hii ndiyo sababu pekee iliyomfanya kumuunga mkono mgombea wa CCM ambaye ameahidi kuendeleza pambano dhidi ya mafisadi. Ni haki yake kabisa kumuunga mkono mgombea yeyote au chama chochote kwani kuwa mwanachama wa chama fulani hakumlazimishi mtu kumuunga mkono mgombeaa wa chama hicho. Na wala siyo lazima mtu anunuliwe na chama ambacho siyo chake kuweza kumuunga mkono mgombea wa chama hicho. Kitu muhimu chakuangalia wakati wakuamua kumpa mgombea kura ni sera anazoengela mgombea na ambazo mpiga kura anafikiri zitakidhi maendeleo yake. Ni kwa sababu
kama hizi pia zimemfanya kiongozi mwingine mashuhuri wa chama cha upinzani, Bwana Augustine Mrema, kumuunga mkono Dk Magufuli wa CCM.

Anonymous said...

We, usiminye!

Mosi, katika mfumo wa Demokrasia ya Kibunge (Parliamentary Democracy) tulitorithi kwa Waingereza, ni anguko kubwa kwa katibu wa chama cha siasa kuachia wadhifa wake wakati wa kampeini ya uchaguzi mkuu. Pigo kwa CHADEMA.

Pili, katika mfumo wa Demokrasia ya Kibunge (Parliamentary Democracy) tulitorithi kwa Waingereza, ni anguko kubwa kwa Kiongozi wa chama cha siasa kuachia wadhifa wake wakati wa kampeini ya uchaguzi mkuu. Pigo kwa CUF.

Katika mfumo wa Demokrasia ya Kibunge (Parliamentary Democracy) tulitorithi kwa Waingereza, ni anguko kubwa kwa Kiongozi wa Chama cha siasa kuacha kuwa mgombea wa Chama wakati wa kampeini ya uchaguzi mkuu na kutomuunga mkono aliyeteuliwa kugombea na huku akimuunga mkono mgombea wa chama kingine. Pigo kwa TLP.

ONLY IN TANZANIA!!!!!!!!!!!!!

Anonymous said...

huyu ndie alikuwa awe mgombea wa urais kwa tiketi ya chadema,leo ana tushauri tumpigie kura adui yake wa muda mrefu ccm kweli Tanzania wana siasa ni pesa tu,ni veizuri tumemjua mapema ujio wa lowassa kwenye ukawa umetuwekea wazi viongozi wengi wa juu wa vyama vya upinzani kama huyu na mwenziwe lipumba ambao tusinge wajua undani wao kama lowassa angeli baki ccm.

kiongozi wa aina hii haoni hata aibu kushauri umma kuyafanya yale aliyo wakataza kwa miaka yote,ana halalisha uamuzi huoeti kwa kuwa huyu fissadi,nani kamhakikishia kuwa magufuli hakuwahi kuwa fissadi? kwa nini asitushauri kukipigia chama kingine cha upinzani kilicho nje ya ukawa ikiwa ukawa hawafai? pengine jawabu ni pesa hivyo vyama ni masikini nayeye anaitumika pesa sio maadili,ningeli muelewa kama angelikaa kimya na kujitoa katika siasa kama alivyoahidi.

mimi kwa sasa ushindi nimeshapata tayari sio lazima kwangu kushinda lowassa au magufuli muhimu nimepata fursa ya kuwaondoa "write off" hawa viongozi wenye tamaa na wasio na misimamo kwanza.

mdau,

Honduras.

Anonymous said...

Hivi Lowasa akishinda tar 25/10 huyu jamaa atakuja kwenye vyombo vya habari na kusema hizo chuki binafsi alikuwa anatumwa na sisiemu. Nadhani ingekuwa bora angenyamaza Kimya Kama lipumba sidhani Kama kuna mtu anamdhamini huyu mzee mla mihogo.

Anonymous said...

Ajenda pekee na nzito iliyo kinyanyua chama cha Chadema/Ukawa ilikuwa ni vita dhidi ya ufisadi na yeye kama kiongozi mmojawao aliyekuwa mstari wa mbele katika vita hii alisimama kidete kutaka kuitoa CCM madarakani kwa ajili ilihusishwa na tuhuma za kukumbatia mafisadi. Baada ya Chadema kupokea wahamiaji kutoka CCM ambao walikuwa wanatuhumiwa kuwa mafisadi na baada ya mabadiliko ya uongozi kufanyika, Dk Slaa aliamua kuhama chama hiki. Tangia mabadiliko ndani ya Chadema/Ukawa kutokea ajenda ya ufisadi ndani ya chama hiki imekufa na badala yake CCM imefufua na inaahidi kuifanyia kazi. Ukizingatia msimamao usioteteleka wa Dk Slaa katika swala hili ni maoni yangu kuwa hii ndiyo sababu pekee iliyomfanya kumuunga mkono mgombea wa CCM ambaye ameahidi kuendeleza pambano dhidi ya mafisadi. Ni haki yake kabisa kumuunga mkono mgombea yeyote au chama chochote kwani kuwa mwanachama wa chama fulani hakumlazimishi mtu kumuunga mkono mgombeaa wa chama hicho. Na wala siyo lazima mtu anunuliwe na chama ambacho siyo chake kuweza kumuunga mkono mgombea wa chama hicho. Kitu muhimu chakuangalia wakati wakuamua kumpa mgombea kura ni sera anazoengela mgombea na ambazo mpiga kura anafikiri zitakidhi maendeleo yake. Ni kwa sababu kama hizi pia zimemfanya kiongozi mwingine mashuhuri wa chama cha upinzani, Bwana Augustine Mrema, kumuunga mkono Dk Magufuli wa CCM.