Advertisements

Friday, October 2, 2015

Mama Lowassa afichua atakavyokuwa 'first lady'.

Mke wa Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regina Lowassa

Mke wa Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regina Lowassa, amesema ana uhakika mumewe atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu kutokana na muitikio mkubwa anaoupata katika mikutano yake na pia kiu ya wazi ya wananchi katika kufanya mabadiliko.

Kadhalika, ametaja vipaumbele vinne alivyojiwekea katika kumshauri mumewe ili mwishowe aliongoze taifa kwa mafanikio makubwa katika kipindi chake cha kuwa madarakani.

Mbali na Chadema, Lowassa anawakilisha pia muungano wa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).

Mama Lowassa alielezea mambo hayo jijni Dar es Salaam jana katika mkutano wake na wanawake walio katika Baraza la Wanawake wa Chadema( Bawacha), Wilaya ya Kinondoni.

Akizungumza katika mkutano huo kuitikia shangwe zilizokuwa zikimtaja Lowassa kama rais ajaye, Mama Lowassa alisema amejawa na imani kuwa mumewe atashinda kwa sababu ameshuhudia mwenyewe muitikio wa wananchi katika mikoa mbalimbali waliyopita katika harakati za kampeni zinazoendelea nchini kote.

“Awali, nilikuwa ninafahamu kwamba Watanzania wengi wana matatizo. Lakini baada ya kutembea zaidi katika kila pembe ya nchi, sasa nikiri kugundua kwamba nilichokuwa nakifahamu juu ya matatizo ya Watanzania kilikuwa kidogo sana kulinganisha na ukweli uliopo... sasa nimejionea, ni matatizo makubwa na ndiyo maana wana kila sababu ya kuamua kufanya mabadiliko,” alisema Mama Lowassa.

ATAKAVYOKUWA 'FIRST-LADY'
Akieleza zaidi, Mama Lowassa ambaye atakuwa 'first lady' kama mumewe atashinda na kuwa rais baada ya Oktoba 25, mwaka huu, alisema atajielekeza katika kushauri na kupigania vipaumbele vinne kwa ajili ya wanawake nchini. Alivitaja vipaumbele vyake hivyo pindi atakapokuwa mke wa rais kuwa ni katiba, elimu, afya na uchumi.

Akifafanua, Mama Lowassa alisema ataendeleza mapambano kuhakikisha kuwa ukombozi wa mwanamke unapatikana kwa dhati kupitia Katiba ya nchi, ambayo serikali itakayoundwa na Ukawa imeeleza wazi kuwa itaisimamia ili iandikwe upya kwa maslahi ya Watanzania.

Alisema yeye kama Mke wa Rais mtarajiwa, atahakikisha elimu kwa wanawake inapewa kipaumbele na kuingizwa kwenye katiba kwani huo ndiyo ufunguo wa ukombozi wa kweli.

Akielezea kuhusu afya, alisema ni dhamira yake pia kuona eneo hilo linaboreshwa kwani waathirika wakubwa wa huduma duni ya hospitali ni pamoja na wanawake. Alizungumzia pia umuhimu wa kuwainua wanawake kiuchumi ili hatimaye waondokane na umaskini.

Alisema hapendi kuona wanawake wanakuwa tegemezi na kwamba atahakikisha mara zote anamshauri Rais ili kuhakikisha wanawake nao wanajitegemea kiuchumi kwa kuhakikisha wanapata fursa za kujipatia mikopo, elimu bora na afya bora tofauti na ilivyo sasa.

Aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi Oktoba 25 na kumpigia Lowassa kura nyingi za ndiyo ili aingie madarakani na kuleta mabadiliko kwa manufaa ya taifa.

Alisema mabadiliko na kuijenga Tanzania mpya yanawezekana, wala si kwa kutumia gharama kubwa na nguvu kubwa isipokuwa kwa kuweka mikakati mizuri, thabiti na kuitekeleza kwa vitendo.

“Ninaomba wanawake mniamini katika hili...kwa sasa siwezi kusema mengi, ila ninanawahakikishia kuwa baada ya Lowassa kuchaguliwa, nitarudi kwenu na tutapanga kwa pamoja mikakati zaidi ya kuishauri serikali ya Ukawa katika kutimiza dhamira ya kuwakomboa wanawake na Watanzania wote,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Kunti Yusuph, alisema katika vipindi vyote vya uchaguzi, wanawake wamekuwa wakirubuniwa na chama tawala kwa vizawadi vidogo kama khanga na kisha kutelekezwa baada ya uchaguzi, lakini sasa hawapaswi kukubali hali hiyo bali washiriki kwa dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli kupitia Ukawa.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Hii inaonyesha jinsi huyu mama na mumewe walivyokuwa na uchu wa madaraka na ndoto zao za kuota mchana za kuingia, uhakika gani wa ushindi wa mumewe aliokuwa nao mbele ya taasisi madhubuti kama CCM na mgombea wake mwenye nguvu kama maghufuli? Kama sio kuwadanganya wafuasi wao basi ni kutengeneza viungo vya kuleta ulalamishi pingine kupelekea wafuasi wao kufanya machafuko endapo watashindwa uchaguzi.

Anonymous said...

Na wafuasi wao wamejiandaa kwa vurugu huku mbeya wanajificha kwenye gest mija wakiongozwa na kiongozi wao msigwa,,,, mama lowasa utaiona ikulu ukienda feri kupanda panton,,,, ukawa habari ndio hiyo ccm miaka 1000000