Advertisements

Tuesday, August 4, 2015

WATU WANNE WANAOSADIKIWA KUWA MAJAMBAZI WAUAWA KATIKA MAPAMBANO YA KURUSHIANA RISASI NA POLISI

Watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wauawa katika mapambano ya kurushiana risasi na polisi wilaya ya Momba. 

Katika tukio hilo watu wanne wanaume wasiofahamika wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliuawa katika majibizano ya kurushiana risasi na Askari Polisi.


Tukio hilo limetokea Agusti 3, 2015 majira ya saa 09.00hrs eneo la Sogea, Kata na Tarafa ya Tunduma Wilaya ya Momba. 

Awali watu hao walivamia dukani kwa Thadeo Sanga (50), mfanyabiashara na wakala wa kuuza/kusambaza bia za TBL , mkazi wa majengo Tunduma.
Katika tukio hilo majambazi hao (ambao kwa sasa ni marehemu) mara baada ya kuvamia eneo hilo wakiwa na silaha /bunduki mbili aina ya SMG na Steering Gun waliwaweka chini ya ulinzi watumishi wa mhanga pamoja na yeye mwenyewe kisha kupora kutoka dukani humo pesa Tshs 200,000/=, Bastola moja namba B-15859 na gari T.215 BLZ aina ya Suzuki V6 mali za Mhanga na kuondoka huku wakifyatua risasi hewani kuelekea babarbara ya Mbeya.
Hata hivyo majambazi hao walipofika eneo la Chapwa walipata ajali na gari hilo hivyo kuamua kuliacha gari na kukimbilia porini.
Kwa kuwa taarifa za tukio zilikuwa zimefikishwa Kituo cha Polisi Tunduma Askari Polisi walifika mara moja eneo la tukio na kuanza kuwafukuza watuhumiwa ambao waliingia Msituni katika Makorongo makubwa yaliyopo eneo hilo na kufyatualia risasi askari Polisi ambao nao walijibu.


Katika harakati za kurushiana risasi Askari Polisi kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo majambazi hao walipigwa risasi kufariki dunia kutokana na majeraha ya risasi katika harakati hizo silaha mbili SMG namba 78421 ikiwa na risasi 1 na Steering moja namba KR 13079 ikiwa na risasi 5. 



Majambazi hao walipopekuliwa baada ya kuuawa mmojawapo alikutwa na tiketi ya basi la Power Tools Logistic LTD yenye namba 111683 iliyotolewa kwa Bw Msonda Agust 2, 2015 ikionyesha alisafiri kutoka Lusaka – Zambia kuja Nakonde, majambazi wengine walikutwa na simu mbili aina ya Tecno na MTN.



Hata hivyo katika harakati za kuwakamata /kukabiliana na majambazi hao raia wema wawili waliokuwa wanashirikiana na Polisi bega bega walijeruhiwa ambao ni 1. Abbas Siwale (22), mkazi wa Chapwa aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi paja mguu wa kulia na alimtambua mojawapo wa majambazi hao kuwa ndiye aliyemjeruhi na 2. Elias Fongo (28), Mkazi wa Chapwa aliyejeruhiwa kichwani kwa kupigwa kitu butu 2 kinachosadikiwa ni jiwe ambacho anadai kupigwa na mmojawapo wa majambazi hao.



Mpaka sasa gari iliyoporwa na majambazi imeokolewa hata hivyo silaha /bastola namba B- 15859 mali ya Bw Thadeo Sanga bado kupatikana. 



Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa majambazi hao ambao miili yao imehifadhiwa Kituo cha Afya Tunduma kusubiri uchunguzi wa kitabibu na utambuzi wanatokea nchi jirani ya Zambia.



Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa katika mamlaka husika juu ya mtu/watu wasiowafahamu ili hatua za haraka za kiuchunguzi dhidi yao zichukuliwe. 



Aidha amewataka wananchi hususani vijana kujitafutia kipato kwa njia halali kwani changamoto za kimaisha/maendeleo hazipatikana kwa njia ya mkato/haramu kwa kutaka utajiri wa haraka. Pia anatoa rai kwa yeyeote mwenye taarifa juu ya silaha/bastola hiyo azitoe katika mamlaka husika ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.



Imetolewa na Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi.

No comments: