Advertisements

Tuesday, August 4, 2015

VIONJO VYA WIKI: Usajili wa Lowassa Ukawa umeacha maswali yanayohitaji majibu


Kwa ufupi

Majibu ya maswali hayo yatasaidia kuondoa shaka ambazo zimejitokeza
By Ndyesumbilai Florian
Nimeamini kuwa kumbe wanasiasa nchini mwetu siyo watu unaoweza kuwaamini, tena kwa asilimia 100.
Wao, pengine wachache au wengi wao ni kama kinyonga, wanabadili rangi kila uchao kulingana na wakati, mazingira au nafasi wanayojikuta siku ile.
Ni watu wa matukio, wapenda sifa, waliojaa kauli tamu, ghiliba nyingi ambazo wakati mwingine hazilingani na mawazo na fikra zao.
Baadhi yao ni wepesi wa kusaka huruma kutoka kwa watu, wapigakura au watu wengineo, ambao huamini kuwa wapo nyuma yao, wanawaunga mkono na hiyo ndiyo furaha ya mwanasiasa wa siku hizi.
Kwa jumla, katika siasa, hasa za nchi zetu hizi zinazojiita changa, kumbe hakuna rafiki, wala adui wa kudumu. Hili linaweza kujidhihirisha wakati huu unapokaribia uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Ni nani aliyekuambia kuwa ukiwa mwanachama wa chama hiki basi utamchukia mpinzani wako kutoka chama kingine?
Jibu ni hapana, hakuna mwanasiasa yeyote ambaye ni rafiki wala adui wa kudumu wa mwenzake, jambo linalozidi kujidhihirisha, hasa wakati huu ambao vumbi la aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Ngoyai Lowassa kuhamia Chadema linaanza kutimua.
Kabla ya kuzama kwenye sura za wanasiasa, acha nikupe mchapo kuhusu urafiki. Ninakumbuka nikiwa mdogo, zama zile za kuchota maji kutoka kwenye vijito kijijini kwetu, Kanamila wilayani Karagwe, mkoa wa Ziwa Magharibi (sasa Kagera), wazazi wangu walinijengea maisha ambayo pamoja na mambo mengine yaliniandaa kujenga urafiki.
Urafiki ule, ambao kwa mila za Wanyambo au Wahaya kutoka mkoani Kagera ulihitimishwa na watu kuchangia damu zao, kwa maana ya kuchanja miili yao, kuweka misingi ya uhusiano, ambao haukuwa rahisi kuuvunja.
Tukio hilo, omukago, linajulikana hadi leo , nalo liliheshimiwa, lilitosha kuwaunganisha na kuwapa udugu.
Ninatambua jinsi ambavyo punje ndogo ya kahawa ilivyotosha siku zile kuwaunganisha watu hadi kuwa marafiki wa kudumu, wenye kufaana katika maisha yao.
Kwa ufupi, kwa punje ile, watu hawakuruhusiwa kusalitiana, hakuna aliyeruhusiwa kwenda kwenye ukoo wa mwenzake ama kuoa au kuolewa, kwa imani kwamba ile damu waliyochangia kwa kukata sehemu ndogo ya miili yao, karibu na kitovu, ikawekwa tone la damu na kuitafuna ile punje ndogo ya kahawa ya kumchesha kule Kagera huitwa akamwani, ilitosha kuwaunganisha na kuwafanya ndugu.
Udugu huo uliendelea wakati wa raha na shida, ambako koo hizo zilizoungana zilibadilika na kuwa kitu kimoja kwa maisha yao yote.
Ninajiuliza je, urafiki wa wanasiasa wetu, akiwamo Lowassa, kiongozi aliyewahi kuandikwa au kuonekana kwenye runinga akiuzungumzia urafiki wake na Rais Jakaya Kikwete, atuambie ulianzia na kuishia wapi?
Je, urafiki huo ulikuwa wa kufaana, ulikuwa wa masharti kwamba ingefikia mahali uishie hewani na kila mmoja aende zake?
Ninawakumbuka wawili hao waliofikia mahali wakaitwa Boyz II Men, kikundi cha muziki kutoka kule Marekani, ambao harakati zao ndani ya chama tawala, CCM zinaweza kuwa zenye kufanana, kama si kulingana.
Itakumbukwa, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005, wawili hao walikuwa chanda na pete, kiasi kwamba ukiiona ndege iliyombeba mmoja wao, basi, mwingine ni abiria.
Ndiyo maana, haikuwa ajabu kusikia kauli ya ‘hatukukutana barabarani’, ambayo ilijaribu kumaanisha jambo kwamba lao wakati ule lilikuwa moja, walikuwa marafiki walioshibana, ambao kwa sasa watakuwa si marafiki, bali mahasimu, hasa wakati wa mchakamchaka wa kusaka kura za kuingia Ikulu ya Magogoni.
Ninauona uhasimu wao, wakati ambao Kikwete akiwa ndiye mwenyekiti wa chama, CCM ambacho Lowassa aliwahi kusema ndicho pekee anachokijua, mahali alikokulia, hakuwahi kufanya kazi yoyote na kwingine, amekiacha na sasa yuko Chadema, lakini swahiba wake, yuko kimya. Kwanini?
Ninajiuliza, kama wawili hao hawakukutana barabarani, maana yake wanajuana ndani na nje, imekuwa vipi Lowassa ahamie Chadema wakati ule Kikwete alikuwa ziarani Australia, ina maana alikuwa tayari amemuaga au alimtoroka?
Pia, ninalo swali jingine kwamba mchakato wa urais uliomuudhi Lowassa kwa kiasi kikubwa, hadi akatumia maneno ya demokrasia iliyobakwa kule Dodoma, ambako Kikwete ndiye alikuwa kiranja mkuu, ina maana kwa mtu aliyekuwa karibu naye kiasi kile aliwahi kumwelezea hisia zake za kutoridhishwa nao?
Kama jibu ni ndiyo, je, ni majibu yapi aliyokuwa ameyapata Lowassa kutoka kwa swahiba wake, Kikwete ambayo kwa kiasi kikubwa yakamkwaza kwa kiasi kile cha kukiacha chama pekee, CCM alichokijua na kwenda Chadema, mahali ambako mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alieleza kuwa siasa ni mchezo wa dynamics, ambao hauna rafiki wa kudumu.
Ni kule kule Chadema, mahali ambako sasa Lowassa ndiye mbeba bendera wao kwenye uchaguzi mkuu ujao, lakini nyuma yake kuna baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge waliomwita siku zile kwa majina mengi wakimwona siyo msafi, mwadilifu, leo amebadilika vipi kuwa safi, ameoshwa kwa sabuni na maji kutoka mto au ziwa lipi?
Si wajibu wangu kuyarudia majina yote aliyowahi kuitwa Lowassa, lakini nauliza, je, wanamwona sasa kuwa ndiye nabii wao, lulu au mwanasiasa na mkombozi wao, kwamba ndiye safi zaidi ya wengine ndani ya umoja huo wa vyama vinne vyenye mamilioni kama siyo maelfu ya wanachama, je, hawakuwa na chaguo zaidi au mbadala, hawakuwa na kimbilio zaidi kwenye azma yao ya kupata mgombea aliye safi? 
Sawa, siasa ni mchezo wa dynamics kama alivyoeleza Mbowe, ndiyo maana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walihitaji mgombea aliye sahihi, mwenye ubora na ambaye lazima alipaswa awe mtu anayekubalika kwa vigezo vyote, mwenye mvuto, yule anayeweza kushindana kwa hoja siyo nguvu na Dk John Pombe Magufuli wa CCM, lakini ilikuwa lazima awe Lowassa?
Sina tatizo lolote na Mzee Lowassa, ni mtu ambaye ninamfahamu, ni mchapakazi, hana mzaha katika kazi zote alizofanya, si uwaziri bali hata alipokuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa, mabosi wa vyama vya wakulima wa zao hilo mbona walimkoma.
Natambua kuwa Lowassa, kama binadamu yeyote yule ana haki ya kuyaishi au kuyatimiza mapenzi, matakwa na ndoto zake zote, zikiwamo za kuhakikisha anaingia mahali pale panapoitwa Ikulu, lakini kama atapewa ridhaa hiyo nasi wapigakura, siku ile ya Oktoba 25 na kama atakuwa amepitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuwakilisha Ukawa.
Tatizo pekee ni ile ndoto au tamaa yake kubwa kuwa ni lazima awe rais wa awamu ya tano ya nchi, ambayo hakuna shaka ameishi nayo siku nyingi akiwa na imani kwamba hawezi kushindwa, haikuwezekana kukatwa jina lake, wakati ule akiwa CCM, jambo ninaloamini ndilo limechangia zaidi kumwondoa CCM, akisema chama hicho si baba wala mama yake. Ninajiuliza, endapo kura hazitamtosha, je, atakuwa tayari kuyakubali matokeo yakitangazwa na NEC na ataendelea kuishi kwa amani, utulivu katika nchi ile ile au atakuwa tayari kuikimbia nchi kama alivyofanya kwa CCM?

4 comments:

Anonymous said...

Hizi porojo hazina tija. Agenda moja na ya mwisho delete CCM!

Anonymous said...

Nafikiri akishindwa atakimbia nchi. Inasikitisha sana kwani safari ya matumaini ya Lowassa naona itagonga mwamba unaoitwa Magufuli.

Anonymous said...

Ok; so you add UKAWA=LOWASA=UFISADI? How does that sound to you anonymous above?

Anonymous said...

Sio porojo wewe mchangia hoja ndio porojo najua mtu akishindwa kwa hoja basi huwa anazungumza utumbo. Nampongeza alietoa hii mada nzuri kuhusu lowasa nnaimani taaluma ya habaari itakuwa fani yake kwani ameuliza masuala ya msingi moja ya suala lilonikwaza ni jinsi lowasa alivyojiwekea matumaini ya kurisi uraisi kutoka kwa rafiki yake licha ya kuwa na mapungufu mengi je kikwete ameamua kumtafuna jongoo kwa meno kukisevu chama chake kwa tuhuma za ufisadi as lowasa kama ni hivyo maneno ya kujivua gamba yalikuwa sio maneno tu bali mikakati ya kweli. Hongereni ccm.