Advertisements

Tuesday, August 4, 2015

Rushwa barabarani yamtia kichefuchefu JK


Rais Jakaya Kikwete akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyofanyika kwenye Viwanja vya Tangamano mjini Tanga jana. 
Picha na Freddy Maro 
Kwa ufupi
Alitaka Jeshi la Polisi kubuni teknolojia ya kisasa itakayosaidia kukomesha vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani na pia kuwadhibiti madereva wazembe ili kuepusha ajali.By Burhani Yakub, Mwananchi

Tanga. Rais Jakaya Kikwete amekiagiza Kikosi cha Usalama Barabarani kufanya mabadiliko ya teknolojia katika utendaji wake ili kuondoa mianya ya rushwa.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama inayofanyika kitaifa jijiji hapa kwenye Uwanja wa Tangamano.


Alisema miongoni mwa mambo yanayochangia ajali ni kukosekana kwa tekonolojia ya kisasa kudhibiti mwendo kasi wa vyombo vya moto, hivyo kutoa mianya kwa baadhi ya trafiki wasio waaminifu kudai rushwa kutoka kwa madereva wanaowakamata kwa makosa mbalimbali.


“Vikiwekwa vidhibiti mwendo kwenye barabara zote kuu, dereva atakayeendesha gari lake kwa kasi namba zinaonekana kwenye kompyuta, hapo tena hakutakuwa na mazungumzo baina ya dereva na askari,” alisema Kikwete.


Pia, Rais Kikwete aliliagiza


Baraza la Usalama Barabarani kurekebisha baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati ili kuongeza ufanisi.


“Baraza liende na wakati, sheria pia ziende na wakati, kadhalika askari. Tukifanya hivyo, tutapunguza ajali za barabarani,” alisema.


Agizo jingine alilotoa kwa baraza hilo ni kudhibiti vyanzo vya ajali kwa kuweka alama kwenye leseni za madereva wanaosababisha ajali, kukomesha rushwa na kutoa elimu ya usalama barabarani.


Rais Kikwete alisema asilimia 99 ya vifo vinatokana na uzembe na madereva kutofuata sheria za barabarani.
“Madereza wanaendesha kwa kasi bila sababu, wanayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, madereva wa pikipiki wanabeba abiria kwa staili ya mshkaki na magari mabovu yako mengi barabarani,” alisema.


Mwenyekiti wa baraza hilo, Pereira Ame Silima, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alisema takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2010/14, watu 19,264 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.


Alisema kuanzia Januari hadi Juni mwaka mwaka huu, watu 1,747 wamepoteza maisha, ambapo kati ya vifo hivyo, 1,352 vilitokana na ajali za pikipiki pekee yake.
Credit:Mwananchi.co.tz

2 comments:

Anonymous said...

Mheshimiwa hili halikuanza jana wala leo na watendaji wako wote wanalielewa mbona hawalikemei. Ya Escrow yamewashinda itakuwa ya barabarani. Tuache utani na wakati unajiiandaa kutimkahh..

Anonymous said...

Ungezungumzia ufisadi ningekuelewa; Escrow, IPTL, Radar, nk. Hiyo ya askari kupata chochote si rushwa wanatafuta pesa ya kulisha familia zao.