Advertisements

Thursday, July 2, 2015

HIKI NDICHO ALIKIELEZA MANJI NA KUTISHIA KUJIUZULU UENYEKITI YANGA SABABU YA UFISADI KAMA MENGI ATATHIBITISHA


KATIKA PITAPITA, TUMEPATA BARUA YA MWENYEKITI WA YANGA KUPITIA MTANDAO WA www.manjivsmengi.com IKIELEZA MAMBO MENGI NA MWALIKO WA MDAHALO AMBAO MANJI AMEUTOA KWA MENGI.
MDAHALO HUO UNAFANYIKA IJUMAA HII NA UTARUSHWA MOJA KWA MOJA NA TBC KUANZIA SAA 12 JIONI HADI SAA 1 USIKU. SOMA BARUA HIYO.
Hisia za Bwana Mengi kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni yangu inamiliki fedha za serikali chini ya Commodity Import Support (CIS)


Mengi ametupa lawama akizishutumu kampuni kama Farm Equip, Apollo Tires, Quality Garage (sasa inaitwa QG Engineering) kuhusika na ufisadi huo wa Sh bilioni 9.055.


YANGA ilikuwa chombo muhimu wakati wa utafutwaji wa uhuru wa nchini yetu ya Tanganyika na baadaye Tanzania. Vikao vya Chama cha TANU ilifanyika katika makao makuu ya klabu hii kongwe.
Vikao vilivyosaidia kuwaondoa wakoloni na kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.


YANGA ilikuwa ni chombo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ndiyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyonayo sasa.


Rangi tatu za Yanga ziko katika bendera ya Tanzania, sehemu ya jina lake iko katika wimbo wa taifa, mwenge wa uhuru ni sehemu ya utambulisho wa klabu hii.


Mwananchama namba moja wa klabu ya YANGA ni hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Marehemu Mzee Karume ndiye aliyejenga makao makuu ya klabu ya YANGA ikiwa ni sehemu ya shukurani wake katika klabu kwa kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya Zanzibar.


YANGA haimilikiwi na mtu mmoja, ni ya wanachama pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini inayowajumuisha Mama wa Taifa, Mama Fatma Karume. Wengine ni Mheshimiwa George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, mmoja wa watu wanaoheshimika katika taifa letu.

Si viongozi pekee ambao ni mashabiki wa Yanga, hata watu wa nchi jirani pia walipoishi hapa nchini kwa ajili ya kupambana kupata uhuru wa nchini zao walijikuta kwenye mapenzi makubwa na Watanzania kutokana na ukarimu wao. Kama walivutiwa na Watanzania ambao wengi ni mashabiki wa Yanga, hili halina ubishi na kwa kuwa mimi ni Mwenyekiti wa Yanga, nawatakia kila la kheri popote walipo.


Mimi ni Yusuf Mehbub Manji (39), Mwenyekiti kijana zaidi kutoka katika klabu ya Yanga.


Nilichaguliwa Julai 14, 2012 kwa ushindi wa 97.5%. Inapofikia hatua mwenyekiti wa klabu kubwa na kongwe kama YANGA kuitwa ni mwizi, fisadi na mla rushwa na kadhalika inanifanya nifikie uamuzi wa aina mbili.


Moja ni kuachia ngazi au nichukue uamuzi wa pili wa kujibu kwa Wanayanga, Watanzania na Afrika nzima. Kwani kukaa kimya ni kuleta maumivu na dharau kubwa kwa klabu hii kongwe na watu wake ambayo kazi yake kubwa ni kuwapa furaha Wanayanga na wapenda michezo.

Katika taarifa iliyoandikwa katika gazeti la NIPASHE la Juni 8, 2015 lililo chini ya IPP Media, inayomilikiwa na Bw. Reginald Abraham Mengi, inaeleza kuwa Kampuni zangu (limezitaja Farm Equip Tanzania and Quality Garage ) zimefanya ufisadi kwa serikali ya Tanzania unaofikia Sh bilioni 9.055 chini ya Commodity Import Support.


Taarifa hiyo ilitoka katika vyombo vya habari vya Bw. Mengi pekee. Ukweli ni kwamba habari hizo ni uongo mtupu, tena wa kupindukia kuhusiana name unaonezwa na vyombo hivyo vya habari vya Bw Mengi.


Mwenyekiti wa YANGA si fisadi, mwizi, mungo kama ambavyo taarifa zinazosambazwa na vyombo hivyo vya habari vya adui namba moja wa klabu ya Yanga Reginald Abraham Mengi.


Mwenyekiti huyu wa YANGA kamwe hapokei mshahara wala posho yoyote kutoka klabu. Hapati faida yoyote ya kifedha zaidi ya kuwa zawadi ya aina yake na kipekee kwa wengine na kuwa mtu anayeweza kuwapa furaha wengine.


Zawadi hiyo aliyonayo mwenyekiti wa YANGA ni furaha ya wengi hasa pale timu inapofanya vizuri kwa kushinda mechi zake na makombe na kuwapa mamilioni furaha ya moyo na kuwafanya wasahau matatizo yao na ndiyo furaha na malipo yangu.


Kwa wale ambao wanaweza kumkumbuka Mengi, alijaribu kutaka kuingoza Yanga katika miaka ya 1990 lakini wazee walimfukuza. Hii ilikuwa ni baada ya kugundua alikuwa akichochea migogoro ili aweze kuingoza Yanga kwa maslahi yake binafsi.


Wakati wa mkutano wa wanachama uliofanyika katika Hoteli ya Starlight na Bw Mengi kulazimika kujificha chooni baada ya walinzi wake binafsi kuzidiwa na hasira za wanachama. Nakumbuka mwanachama mmoja alimueleza hivi: …” ungeenda kwanza kumaliza matatizo ya ndoa yako kuliko kuendeleza mgogoro katika klabu yetu (kweli mgogoro ambao aliutengeneza kwa makusudi).” Baada ya siku hiyo kufanikiwa kuokolewa na Polisi, hakuwahi tena kurejea Yanga.


Mwanzoni mwa 2006, wakati ndiyo nikiwa na umri wa miaka 36, niliombwa kuingia kuisaidia klabu ambayo ilikuwa katika hali mbaya kifedha. Kwamba niwe mdhamini mkuu na siku chache baadaye taarifa zilimfikia Bw Mengi ambaye alionekana kutofurahia na Machi 26 alianza kutumia magazeti yake kunishambulia kwa nia ya kunichafua kwamba mimi ni mhalifu, muongo na fisadi.


Kwa kuwa nilikuwa ni mwananchi wa kawaida, si kiongozi wa klabu kubwa kama Yanga, niliamua kutafuta haki yangu kwa kumfungulia kesi mahakamani. Kesi ambayo nilishinda na yeye kutakiwa kunilipa Shilingi 1.

Nilipohoji uwezo wa kufikiri, kutafakari na kuamua wa mengi, aliamua kunifungulia kesi akidai nimlipe Sh bilioni 150, mwisho alishindwa na sasa anatakiwa kulipa kiasi cha Sh bilioni 5 kwa uendeshaji wa kesi.
Nawakumbusha kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita Bw Mengi alifungua kesi kesi mbili, moja akipoteza na nyingine alimua kujitoa au kuifuta mwenyewe. Hii inaonyesha kiasi gani kumekuwa na ukweli katika yale ambayo nimekuwa nikimueleza.


Kabla sijachaguliwa kuwa mwenyekiti wa YANGA mlinijua, mlijua nilikuwa mtu ninayekipigania ninachokiamini na kama nilikiamini kitu, basi ilikuwa ni njia yangu sahihi ya kushinda.
Najua kwa wanachama wa Yanga wamekuwa wakiona namna Mengi anavyonishambulia katika vyombo vyake vya habari lakini wamekuwa wakipuuzia na kunipa heshima yangu kama mtu niliomaliza mgogoro mkubwa na mgawanyiko ndani ya klabu ya Yanga ambao niliumaliza ndani ya miezi mitatu tu baada ya kuwa mdhamini mkuu wa klabu.


Niliunda bodi ya kwanza ya wadhamini kwa kuwaomba wazee waanzishe baraza lao. Halafu mimi nilijiuzulu kwa kuwa nilikua ni kijana mno, miaka 33 nisingefaa kuwa mmoja wa wajumbe wa baraza la wadhamini. Mwisho nikaaga kwa kuwa kazi yangu ilikuwa imekwisha.


Wazee wa Yanga waliamua kufanya dua maalum kwa ajili yangu, wakanisimika na kunifanya kuwa CHIFU wa kwanza wa klabu kwa kunipa ngao yenye nembo ya klabu pamoja na mkuki.

Nilipotakiwa kwa mara nyingine katika klabu, nikiwa na miaka 36 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu kongwe ya YANGA.Kitu ambacho najivunia kwa kuwa kiongozi kwani hata familia yangu imekuwa ikipata heshima kutoka kwa wanachama na mashabiki wa Yanga.


Wakati mwingine mama yangu anapokwenda sokoni, wakati mwingine hatakiwi hata kulipa kutokana na heshima ya kuwa mama wa Mwenyekiti wa Klabu yenye heshima ya YANGA. Mmenipa heshima kubwa, mfano watoto wangu katika akaunti zao za Facebook hawawezi hata kuweka picha yangu kwa hofu ya kupata marafiki wengi kupindukia.


Mke wangi analazimika hata kutumia jina tofauti kwa kuwa mapenzi makubwa anayopata kutoka kwa mashabiki wa klabu ya YANGA yanafikia hadi kumpa hofu na hii ni kwa kuwa wanachama na mashabiki wanajua huyu ni mke wa mwenyekiti wao ambaye wanamuamini na kumpenda sana.


Kwa mapenzi haya ninayopata ninaahidi nitaendelea kufanya kila ninaloweza kwa uwezo wangu wa juu, hali na mali kwa klabu katika kipindi changu chote wakati nikiwa mwenyekiti. Mapambano yanaendelea kwa ajili ya klabu yetu.


Tokea Bw Mengi alipofukuzwa na wanachama wa YANGA, amekuwa mwoga kuhusiana na maisha yake, amejaa hofu akidhani kuwa kila Mtanzania anataka kumuua! Anaomba ulinzi wa Jeshi la Polisi huku akiwa hajui asilimia kubwa ya askari Polisi nao ni YANGA.

Nashangaa alitaka Yanga iharibikiwe kabisa, lakini yeye ndiye anayekimbilia katika runinga akidai kuna watu wanatanga kumuua. Bw Mengi, YANGA haitaki kukuua, lakini tunakuchukia ingawa tumekuwa wastaarabu na tunajizuia. YANGA tunachotaka ni wewe kutuacha tuendelee na maisha yetu na familia yetu, endelea na yako.
Tungependa hata usizungumzie jina la klabu yetu kupitia kalamu yako wala midomo yako.


Lakini inaonekana kama shetani, umekuwa ukijaribu kurejea katika klabu ya YANGA tena ukionyesha umepania kutufelisha kitu ambacho kamwe hauwezi kufanikiwa hata kidogo. Hauwezi ukashinda uimara wa mioyo yetu ambayo imeunganika na kuwa kitu kimoja. Unaonekana unataka kutumia nafasi hii kurejea na kuomba msamaha kwa mabaya ulioifanyia klabu.
Kama kweli sisi Watanzania tunajulikana dunia nzima kama ni watu tunaoishi kwa amani, watu wenye upendo na wakarimu kwa nini kila mwaka unalalamika kuwa kuna watu wanataka kukua? Au ndiyo ndoto mbaya zinakuandama kutokana na mabaya uliyoyafanya huko nyuma, hivyo unataka kuomba msamaha?


Bw Mengi, mimi sihitaji kulilia ulinzi kama unaotaka wewe. Ulinzi wangu ni mamilioni ya Wanayanga waliopo. Sihitaji fedha ninapotembea sehemu yoyote ya Tanzania kwa kuwa hakuna Mwanayanga anayehitaji fedha kutoka kwangu.
Sihitaji tuzo yoyote ili nijulikane au matangazo ili wanijue, hakuna Mtanzania asiyenijua. Pia sihitaji pasi ya kusafiria ya kibalozi ninapokuwa uwanja wa ndege. Kama ni heshima ya red carpet, basi ninaipata kwa kuwa Mwenyekiti wa Yanga ambaye ni mkweli na muwazi.


Ntaendelea kuwa mwenyekiti mwaminifu ninayejitolea kwa uwezo wangu wote kwa klabu ninayoingoza, kama siku itafikia kifo. Basi nitakuwa na uhakika watoto na familia yangu itakuwa katika mikono salama ya wanachama na mashabiki wa YANGA ambao wamesambaa dunia nzima.




Bw Mengi, mimi ni mtu wa kawaida tu niliyelelewa na baba ambaye wakati wa vita ya kumng’oa Nduli Iddi Amini Dada alitengeneza bodi ya gari maalum kwa ajili ya wanajeshi wa Tanzania waliokwenda kupambana ambao baadaye walimshukuru kwa kutembelea sehemu aliyokuwa akitumia kutengenezea mabodi hayo.

Tokea hapo, kila Rais alitembelea katika gereji yake hiyo ndogo. Nilifunga ndoa mwaka 1994, ilihudhuriwa na wageni kama Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi, Marehemu aliyekuwa Wazidi Mkuu, Cleopa Msuya, Mheshimiwa John Malachela na viongozi wengi wakubwa. Sasa nina watoto wawili wa kiume, mmoja akiwa na umri wa miaka 17 na mwingine 12.
Nakuuliza, ulikuwa wapi wakati wa vita vya Kagera pia ndoa yako ya sasa ina umri gani?


Haujawahi kuchaguliwa hata kuwa myampara tu wa gereza, lakini ajabu unajidanganya mwenyewe eti ni kiongozi bora.


Tunajua haukufurahia Yanga kushinda taji lake la 25 la Ligi Kuu Bara msimu uliopita! Kumbuka Mataji 50 tu ymegombewa, hivyo Yanga imebeba nusu ya hayo hadi sasa. Haufurahii kuona kijana mdogo kama mimi napendwa na watu wengi kuliko wewe, ndiyo maana umekuwa ukiamua kujipamba kama vile vitabu vya ujanjaujanja kwamba wewe ni kati ya watu matajiri zaidi Tannzania!


Mtu usiye na huruma kuamua kupitia viwanda vyako kuchanganya dawa kutoka Marekani na maji ya Tanzania na kuyaita Coca-Cola, kuchanganya kalamu na karatasi na kuita taarifa! Kujionyesha wewe mwenyewe kwenye runinga yako, halafu unataka watu waamini hiyo ni taarifa kwao!


Unawalazimisha wanasiasa wakuombe ardhi au migodi ili uiendeleze wakati hauna mtaji wa kufanya hivyo! Waliogundua kuwa huna uwezo huo unawashambulia kwa madai wamewapa wageni na ungepewa wewe migodi ya gesi ungeweza kutuwasaidia sisi Watanzania masikini.


Kama sikosei thamani yako ni dola milioni 550, unapata faida ya 10%. Mfano dola milioni 55 utatakiwa kulipa kodi ambayo itakuwa si chini ya dola milioni 16.5 kwa mwaka. Je, umekuwa ukilipa kodi hiyo? Mimi kama Mwenyekiti wa Yanga najua kila kitu kuhusiana na wewe.

Bw Mengi, usitake kudanganya watu biashara uliyoanzisha miaka 10 iliyopita eti thamani yake sasa ni dola milioni 550. IPP ilianzishwa mwaka 1981, kabla ya hapo ulikuwa mhasibu tu. Nauliza, unafikiri YANGA hawajui kuhusiana na uhusiano wako kwao hadi walipofikia kuniongezea muda kama mwenyekiti wao. Wanajua thamani yangu kuliko wewe na uhasibu wako.

Ninaweza nikakupa mfano wa biashara zangu, lengo si kujigamba. Sitaki kuzungumzia kampuni kubwa ya uvuvi katika Ziwa Victoria au kampuni kubwa ya Rice Mill ya Morogoro. Nitakupa mfano mmoja tu, Novemba 25, 2011 nilifungua maduka makubwa ya biashara na mmoja wa wanasiasa wakubwa barani Afrika ambaye sasa ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Mheshimiwa Railla Odinga ndiye alikuja kuyafungua akiwa mgeni rasmi na mwalikwa siku hiyo. Wewe umefungua biashara gani kubwa ndani ya miaka 10 na kiongozi yoyote wa Tanzania akaja kuizindua?

Maisha yangu nimekuwa mjumbe wa bodi ya Afrika ya kupambana na ugonjwa wa ebola maarufu kama African Union Ebola Solidarity Trust Fund ambako nimesaidia kupatikana kwa fungu la dola milioni 50 kupambana na ugonjwa huo hatari na kuutokomeza kabisa kwa wale ambao waliobaki wameathirika katika nchi ya Sierra Leone.

Angalia mashabiki na wanachama wa Yanga katika mitandao wanavyoonekana wakiwa wameungana na wenye furaha kubwa kushangilia ushindi au ubingwa, hii inahamasisha hata vijana. Kwa miaka 10 nimefanya makubwa kwa bara letu la Afrika, ajabu unaona si sahihi, umeamua kufanya ujanja ujanja kwa kununua tuzo. Najaribu kujiuliza watu wangapi watakuja katika mazishi yako kama itakavyokuwa kwangu, kijana uliyejaribu kutaka kumharibia tokea akiwa na miaka 30, huku ukijaribu kuniharibia biashara zangu.
Lakini Mungu ni mwema, ameamua kunichagua kuwa mmoja wa vijana wanaopendwa zaidi nchini Tanzania kama si Afrika kote.

Bw Mengi, umekuwa na tabia ya kuwachafua watu kila unaposhindwa kupata unachotaka kwamba ni wala rushwa na mafisadi! Mahakama Kuu ya Uingereza ambayo ulifungua kesi kwa madai ya kuitwa muongo na maneno mengi, imetupa kesi yako kwa kuonekana haikuwa na mantiki. Sasa uamuzi umekugeukia kwamba si muongozo tu au si mwaminifu tu lakini imeonekana ni mtakatishaji wa fedha, vyombo vyako vya habari havifuati weledi, badala yake vinafuata wewe unafuata au kufadika na kipi!

Inaonekana IPP hakuna uhuru wa habari na waandishi wenyewe isipokuwa kile unachotaka wewe hadi kufananishwa na ujasusi wa habari (sawa na ule wa Osama Bin Laden wa Al-Quaeda au ISIS kwa siku za karibu).

Kesi hiyo imekugeukia kwamba kwa sharia za Tanzania unapaswa kushitakiwa kwa jinai na vyombo vya sharia vya Tanzania.

Kwa nafasi ya Mwenyekiti wa YANGA na kama mwangalizi mkuu, nitapambana kulinda jina la klabu hii tukufu na kama Mwenyekiti wa YANGA ningependa kutangaza kumualika Bw Mengi katika mdahalo utakaorushwa na runinga moja kwa moja Ijumaa ya Julai 3, 2015.

Watanzania watakuwa na nafasi ya kuulizwa maswali katika mdahalo huo wa wazi na moja kwa moja. Hii itakuwa nafasi nzuri kwa Bw Mengi kuja au kutoa ushahidi wake kuhusiana na ufisadi wangu kwa uthibitisho. Pia utakuwa wakati mzuri kwa Watanzania kujua nani ni mkweli na yupi hayuko sahihi.

Pia ningependa Watanzania wapewe nafasi ta kupiga kura kwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) kama kweli wameona mimi ni fisadi. Kama itakuwa hivyo, basi nitajiuzulu mara moja uenyekiti wa YANGA.

Ni jukumu langu kama Mwenyekiti wa Yanga kumaliza upuuzi huu ambao unaozushwa na Bw Mengi ambao unaweza kuiondoa klabu yetu katika utulivu na kuweza kufanya mambo yake kwa mpangilio mzuri kama ambavyo tumekuwa tukitaka. Yanga imekuwa ikiwavutia wachezaji wengi wakiwemo wa kimataifa, pia tuko katika harakati za kuhakikisha tunajenga uwanja wetu wenyewe na YANGA yenye mipango endelevu na thabiti.


Sioni kama kuna sababu ya kupoteza muda wangu wa kuitumikia Yanga kwa ajili ya mtu anayewalaghai watu kuwa yeye ni mtu mzuri, mwema, kitu ambacho ni uongo mtupu. Nasisitiza, sasa imetosha.


Ukweli utajulikana hiyo Julai 3, 2015 na kama Bw Mengi atakuwa na ukweli anaotaka kuuweka wazi, basi hatasita au kukimbia kuja kukaa name mbele ya Watanzania kwenye mdahalo. Lengo ni kumaliza ubabaishaji huu na ugaidi kupitia vyombo vyake vya habari kwa kuwa nimechoka sasa na hali hii kwa kuwa inanichosha na kuchukua nguvu zangu za kupambana na maendeleo ya klabu.


Klabu ya Yanga ni tukufu katika nchi, uongo wa Bw Mengi umekuwa ukifanya hata baadhi ya wanaotaka kufanya biashara na klabu, mashabiki au wanachama kuingoa hofu kwamba klabu yetu inaendeshwa na fedha chafu, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.


Yanga Daimba Mbele, Nyuma Mwiko. Ndiyo maana nataka huu mdahalo ili kumaliza maneno yasiyokuwa na ukweli ya Bw Mengi kwa miaka takribani 20 sasa. Tunataka kumaliza hilo ili tuelekeze nguvu zetu kwenye maendeleo ya klabu na kuachana na Bw Mengi ambaye amekuwa akitumia vyombo vyake vya habari kutaka kutuvuruga kwa makusudi.


Acha nihitimishe hili; kuwa mwisho lazima tujue ni mimi mbaya kwa Tanzania au Bw Mengi, kiongozi huyu ambaye alitaka kura za Wanayanga lakini sasa yuko ofisini akifanya kila analoweza kuivuruga Yanga huku akihakikisha tunashindwa katika kila jema na bora tunalotaka kufanya kwa ajili ya klabu yetu. Waanzilishi wa klabu yetu, taifa na viongozi tutakuwa na kila sababu ya kujilaumu wenyewe kama tutashindwa kufikia malengo na tunachokitaka kwa ajili ya klabu yetu.


MUNGU IBARIKI YANGA, TANZANIA NA AFRIKA.


NINAWASHUKURU SANA.

Yusufali Mehbub Manji

(Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga)


No comments: