Advertisements

Thursday, March 5, 2015

WADAU WA ELIMU WAITAKA SERIKALI KUPANDISHA WASTANI WA UFAULU

Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyuo na shule(TAMONGSCO) Taifa, Leonard Mao, akizungumza katika mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho Kanda ya Mbeya uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Saut tawi la Mbeya.
Mwenyekiti wa Kanda ya Mbeya wa Tamongsco, Mzee Asanga akitoa utambulisho katika mkutano huo.
Wamiliki wa Shule na Vyuo, Wakuu wa Shule na Mameneja wakiwa kwenye mkutano mkuu wa Mwaka wa Tamongsco Kanda ya Mbeya.
CHAMA cha wamiliki wa vyuo na shule zisizokuwa za Serikali(TAMONGSCO) Kanda ya Mbeya kimeitaka Serikali kupandisha wastani wa ufaulu wa wanafunzi wakati wa kuvuka kidato kimoja kwenda kingine kutoka 30 ya sasa hadi 50.

Wito huo ulitolewa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO Taifa, Mringe Mzava, katika mkutano mkuu wa kawaida waKanda ya Mbeya uliofanyika katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT) kilichopo Mwanjelwa jijini Mbeya.

Mzava alisema kiwango kilichowekwa na Serikali cha kuwabana wanafunzi kuvuka kidato ni kidogo sana kiasi kwamba kinapunguza morali ya wanafunzi kujisomea hali inayopelekea kuwa na viwango vidogo vya elimu na kupungua kwa wastani wa ufaulu katika matokeo ya kidato cha nne.

Alisema shule zisizokuwa za serikali zimeweka wastani mkubwa jambo linalochangia shule hizo kufaulisha zaidi kuliko shule za serikali ambapo aliishauri Serikali kupandisha wastani huo kutoka 30 hadi 50 ili shule zote ziwe na wastani mmoja na kuongeza ufaulu kitaifa.

Alisema kwa hali ilivyo si rahisi sana kuendelea kupata wataalam watakaweza kulisaidia taifa katika maswala ya maendeleo kutokana na wengi kutokuwa na matokeo mazuri ambapo asilimia kubwa wanatengenezewa matokeo kutokana na Wanasiasa kuingilia mfumo wa elimu.

Aidha alitoa wito kwa Wamiliki wa Shule wengine kuacha kupokea ada kwa wanafunzi ambao hawajakidhi vigezo vya kujiunga na shule ama kuendelea na kidato kingine bila kuwarudishia jambo alililodai ni kuhujumu uchumi wa wazazi na kupelekea shule zote kuwa na sifa mbaya.

Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule zisizokuwa za Serikali, Fidelis Mwampoma, alisema hata kwenye vikao vya wakuu wa Shule walikubaliana kuishauri Serikali ili ipandishe wastani huo kwa kuwa ni mdogo na unapunguza ari ya kujisomea wanafunzi.

Alisema Wanafunzi wengi wanaosoma kwenye shule za Serikali wamebweteka na hawajishughulishi kutokana na kuwekewa kiwango kidogo cha ufaulu, hivyo Serikali inapaswa kuangalia upya kiwango hicho kwa maslahi ya taifa ili kuwe na wasomi wengi na wenye kujituma.

“ Sisi Wakuu wa Shule hatujakubaliana na wastani uliowekwa na Serikali kwani ni mdogo mno na unasababisha wanafunzi wabweteke, hivyo ni bora wastani ukapanda kutoka 30 hadi kufikia 50 hii itasaidia kuongeza nguvu ya kujisomea” alisema Mwampoma.

Alisema Serikali isipoliangalia kwa ukaribu suala hilo kuna uwezekano wa kupata wataalamu wasiokidhi vigezo na wasiokuwa na uwezo kabisa wa kufanya mambo ya maendeleo na badala yake watapatikana watu ambao wataendeleza ubabaishaji utakaoligharimu taifa.

“Mambo mengine Serikali inapaswa kuiga kutoka kwenye Shule zetu mbona na sisi kuna vitu tunaiga kutoka kwao, Serikali inachojaribu kufanya ni sawa na timu za mpira wa miguu zinapocheza uwanjani lakini zikashindwa kufungana ukaamua kupanua goli utakuwa huzisaidii timu” alisema Mwampoma.

Na Mbeya yetu

No comments: