Advertisements

Thursday, March 5, 2015

DHAMBI YA KUMLIZA, KUMTESA ANAYEKUPENDA KWA DHATI!

Mpenzi msomaji wangu, hakuna ubishi mapenzi yanachukua nafasi kubwa katika maisha yetu. Mimi na wewe tunahitaji kuwa na wapenzi tena wenye mapenzi ya dhati ili maisha yetu yaweze kukamilika.

Bila kuwa na mtu ambaye kuna wakati unammis, ukiwa naye unajiona ni mwenye bahati kwa faraja anayokupa, ni lazima utahisi umepungukiwa kitu muhimu.Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo wanaochukulia mapenzi kama kitu rahisirahisi. Kitu ambacho anaweza kuingiza usanii na mambo yakaenda.

Hapa namaanisha hivi, mtaani kuna watu wa aina mbili. Kuna ambao wanajua kweli kupenda. Akisema anampenda fulani, anamaanisha na kuna wale ambao wanaweza kusema wamependa kumbe wametamani au wana nia zao wanazozijua wenyewe.

Unamkuta mwanaume anadanganya kuwa ametokea kumpenda msichana fulani na ana dhamira ya kufunga naye ndoa lakini kumbe hana lolote, nia yake amuonje kisha aingie mitini.
Achilia mbali hao, kuna wanaume ambao wanatumia pesa na utaalam wao wa kuongea kuwarubuni wasichana ili watembee nao kwa kipindi fulani kisha wakisharidhika, wanawaacha. Wavulana hao wapo na wamekuwa ni tatizo kubwa huko mtaani.

Lakini pia wapo wasichana ambao wenyewe wanajiita wa mjini. Yaani wao hawajui kupenda, wanachoangalia ni mwanaume ‘mwenye nazo’. Wakishampata, watajifanyisha kuwa na mapenzi ya dhati kupita maelezo kumbe hamna kitu, usanii mtupu!

Katika mazingira hayo sasa utaona ni kwa jinsi gani mapenzi yamekuwa janga. Ndiyo maana leo hii wapo wanaotamani kutojihusisha na mambo ya mapenzi kwa sababu hizihizi za usanii na ujanjaujanja mwingi.

Wakati mambo yakiwa hivyo, kuna baadhi ya watu ambao wamekithiri kwa tabia ya kuwatesa wapenzi wao kisa wameoneshwa kuwa wanapendwa sana. Wapo watu ambao wakipenda wamependa kweli na hawawezi kujizuia kuonesha hisia zao kwamba ‘wamekufa’.

Hatua hiyo sasa hivi badala ya kuwa changamoto kwa aliyependwa ili naye aongeze mapenzi, inakuwa tatizo. Uchunguzi unaonesha kuwa, sasa hivi mwanaume akioneshwa kupendwa sana na mwanamke, atavimba kichwa na kumfanyia mwenzake kila aina ya visa eti kwa kuwa amebaini amependwa na hawezi kuachwa.

Hili halipo kwa wanaume tu. Wapo wanawake ambao nao kwa kujua kuwa waume zao wamekufa kwao, dharau inaongezeka, heshima inapungua na kufanya hata yale ambayo wanajua yanawakera wenzao.

Hivi kwa nini tufikie hatua ya kuwatesa watu ambao wameshindwa kujizuia kuonesha mapenzi yao kwetu? Kupendwa sana imekuwa nongwa jamani? Hujui kwamba Mungu anaweza kukupa adhabu kwa kutenda dhambi hiyo ya kumuumiza mwenzako bila sababu hasa katika ulimwengu wa sasa ambao kupendwa ni bahati?

Mbaya zaidi mtu anakutamkia kwamba anakupenda sana na yuko tayari kufanya lolote ili kukufanya ufurahi na wewe unajibu kuwa unampenda, kumbe hamna lolote. Matokeo yake sasa kadiri siku zinavyokwenda, unaanza kuonesha uhalisia kwamba humpendi kwa matendo. Hii siyo sawa na ni dhambi kubwa. Mimi nadhani kama humpendi mtu ni vyema ukamwambia mapema ili asikupe nafasi kwenye moyo wake.

Unapokubali kuwa na wewe unampenda kisha baadaye unaanza kumtesa kwa kumfanyia mambo ambayo hakuyatarajia, unafanya makosa na ni dhambi hata kwa Mungu.

Kama kweli unapenda, mdhihirishie kwa matendo ili asiwe na shaka kwamba huenda ameingia kwenye penzi la kisanii, lakini kama yeye amekutamkia kuwa anakupenda lakini wewe ukahisi huna mapenzi naye, kuwa muwazi kwake ili ajue wazi amempenda mtu ambaye hampendi!

Lakini na sisi tunaopenda, tusilazimishe!Ukiona mtu ana kila dalili ya kutokuwa na penzi la dhati kwako, kubaliana na moyo wako umuache huku ukijipa imani kwamba utampata mwingine atakayekupenda na wewe ukampenda.

GPL

No comments: