Advertisements

Wednesday, January 28, 2015

Vuta nikuvute Bungeni, Spika Makinda ahairisha bunge

Spika wa Bunge Anna Makinda amelazimika kuahirisha kikao cha Bunge kilichoanza jana, baada ya vuta nikuvute iliyotokea  baada ya kutolewa kwa hoja binafsi kutoka kwa Mbunge na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuhusu jeshi la polisi kumshambulia Profesa Ibrahimu Lipumba jana akiwa kwenye maandamano .
Akizungumza katika bunge hilo Mbatia amesema kuwa kitendo cha polisi cha kuwapiga raia wasiokuwa na hatia, kuwazalilisha waandishi wa habari na kupiga mabomu ya machozi kiasi cha kuwafanya watoto wadogo kuhangaika hakikubaliki.
Amesema polisi wakiendelea kuachwa kufanya vitu vya uvunjifu wa Amani Serikali haitatawalika hivyo ili kurejesha amani na imani ya wananchi kwa Serikali yao ni vema shughuli zote za Bunge zikaahirishwa kupisha mjadala wa hoja hiyo binafsi kwa lengo la kuinusuru nchi.
“Mheshimiwa Spika naliomba bunge lako liahirishe shughuli zake ili leo tuweze kujadili suala hili la uvunjifu wa amani uliofanywa na  jeshi letu la polisi jijini Dar es Salam jana, wao wanasema kuwa wamepewa amri kutoka ngazi za juu tunataka serikali ituambie ni nani anayetoa amri hizi za kupiga watu wasiokuwa na hatia yeyote, amesema Mbatia.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo asilimia kubwa ya wabunge walisimama juu isha ya kuunga mkono hoja hiyo lakini Spika Makinda akawaomba wakae ili aweze kutoa ufafanuzi kwa mujibu wa kanuni.
Spika makinda aliwaeleza wabunge hao kuwa suala hilo ni nyeti kwa sababu ni la kiusalama, ili kupata ufafanuzi zaidi anaiagiza Serikali kufikisha bungeni hapo majibu ya hoja hiyo kesho ili wabunge waweze kujadili.
Baada ya maamuzi hayo ya Spika Makinda kelele zikasikika bungeni huku wabunge wakitaka kufanyika kwa mjadala huo leo leo, ndipo Spika alipoamua kuahirisha bunge hadi saa kumi jioni.
MWANANCHI

No comments: