Advertisements

Tuesday, January 27, 2015

Anko kakumbuka jezi wakati refa kamaliza mchezo

Anko kakumbuka jezi wakati refa kamaliza mchezo
Kwa mujibu wa Mtandao wa Google, Uncle ana miaka 25. Kama unasahau habari za magazeti, basi kwa mujibu wa Google, Uncle alikwenda kufanya majaribio na West Ham mwaka 2009. Na kwa mujibu wa Google, huo ndiyo ulikuwa mwaka ambao Uncle aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Cecafa.
KWA mujibu wa Mtandao wa Google, Mrisho Ngassa, maarufu sana kwa jina la Uncle alizaliwa Aprili 12, 1989. Ina maana kwa mujibu wa Google, Uncle au Anko alizaliwa miaka mitano kamili baada ya kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Google, Uncle ana miaka 25. Kama unasahau habari za magazeti, basi kwa mujibu wa Google, Uncle alikwenda kufanya majaribio na West Ham mwaka 2009. Na kwa mujibu wa Google, huo ndiyo ulikuwa mwaka ambao Uncle aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Cecafa.
Kwa mujibu wa Google pia, Julai 2011, Uncle alikuwa Marekani akivaa jezi za Seattle Sounders kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United. Lakini kama tumeamua kuiamini Google kiasi hiki, basi mwaka 2009 wakati Uncle akiwa katika fomu ya ufungaji bora Cecafa Uncle alikuwa na umri wa miaka 19 tu.
Kabla ya kujadili kuhusu utoro alioufanya Uncle kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha mapya ya soka, najua moyo wako utakuwa umeanza tabia ya udadisi kama Uncle kasema kweli kuhusu miaka yake au hapana. Kwa sasa si muhimu tena.
Kitu muhimu ambacho wote tunafahamu ni kwamba Uncle alipaswa kwenda kutafuta maisha ya soka nje mwaka 2009 wakati ule alipokuwa katika ubora wa michuano ya Cecafa. Wakati ule alipokwenda katika michuano ya Chan pale Ivory Coast na Taifa Stars.
Hati yake ya kusafiria ilikuwa inaonyesha kuwa Uncle alikuwa na miaka 19. Ni umri sahihi zaidi na mwili wake ulikuwa unamtiii kwa kila kitu alichouomba kufanya uwanjani.
Nafasi za kwenda West Ham au Marekani zilikuwa za kisiasa zaidi. Lakini maisha halisi ya soka kwa Uncle alipaswa kuyaelekeza Afrika Kusini au nchi za Scandinavia kwa wakati ule.
Hatuhitaji kurudia mara nyingi kuandika tena na tena kuwa nchi kama zile za Sweden, Norway, Denmark, Finland ndizo ambazo wanasoka wa ukanda huu wanaotokea katika ligi za kawaida kama Kenya na Tanzania ndiyo huwa wanaanzia maisha ya kusaka safari ya mafanikio katika klabu kubwa za Ulaya.
Uncle hakuonekana kuwa makini sana katika ofa hizo, wakati ulikuwa wake kupendwa katika Uwanja wa Taifa. Inatokea kwa nadra sana kwa mchezaji kupendwa Uwanja wa Taifa kama Mbwana Samatta au Renatus Njohole na kisha ukaamua kuondoka baada ya kutamba kwa msimu mmoja.
Kama Uncle angekuwa makini nyakati zile leo angekuwa mbali sana, kama wakati ule angeanzia na Klabu ya Free Stars leo angekuwa mmoja kati ya wachezaji wanaoheshimika Kaizer Chiefs au Orlando Pirates. Katika soka la mbio la Waafrika Kusini, Ngassa angeshindwa nini?
Lakini baada ya kuona ufalme wake ukiondoka Yanga na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Msuva, Uncle ameamua kutafuta maisha ya soka Afrika Kusini. Ni wakati mwafaka? Sidhani. Mwili wake hauwezi kurudi tena katika kasi ambayo hata Wabrazili kina Michael Bastos na Fellipe Mello walishindwa kumkaba Juni 2010 pale Uwanja wa Taifa.
Pasipoti inaweza kuonyesha umri wa miaka wa miaka 25, lakini mwili bado utasisitiza katika miaka halisi. Ndiyo maana wenzetu kina Michael Essien wanapodanganya umri huwa wanafanya kazi ya kukusanya pesa haraka haraka. Leo Essien ana miaka 32 lakini amechoka mno.Frank Lampard ana miaka 36 lakini kaipatia City pointi saba muhimu msimu huu.  Lakini kabla hatujafika mbali, tujiulize. Hivi ile ofa ya El Merreikh kwa nini Uncle aliitosa? Dola 5,000 kwa mwezi achilia mbali usafiri, nyumba na bonasi 
nyingine. Maisha yanakwenda kasi.
Kuna wajanja wa klabu yake ya Yanga ambao walimuingiza katika gari pale Leaders Club Kinondoni wakamsihi aitose hiyo ofa naye akakubali lakini sasa anajuta. Akasaini Yanga. Leo wajanja wale ni mashabiki wakubwa wa Msuva. Hawana habari na Uncle.
Kila la kheri kwa Uncle. Kwa kiwango cha hali ya juu alichokionyesha kwa miaka 10 hapa nchini, ametuburudisha vya kutosha na sasa anakumbuka jezi wakati mwamuzi anamaliza mpira, anastahili japo kucheza soka la kulipwa nje ya mipaka yetu, hata kama ni kwa wiki kadhaa tu.
Na hasa unapozingatia kuwa Uncle ni rafiki wa kila mtu. Ni mtu mzuri, karibu kila mchezaji mwenzake anampenda. Binafsi ni rafiki yangu. Huwa ananikwaza anaposhindwa kuchukua uamuzi mwafaka katika wakati mwafaka. Basi!


Source:Mwanaspoti

No comments: