Advertisements

Saturday, December 20, 2014

Kamishna Kova: Polisi tumejipanga kusimamia uchaguzi

Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamanda Suleiman Kova

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema halitawaonea haya wale wote watakaosababisha kwa namna moja ama nyingine kuharibika tena kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kurudiwa kesho katika baadhi ya maeneo
Jumla ya mitaa 89 kutoka wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam, zinatarajiwa kufanya uchaguzi huo wa marudio kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna wa Kanda Maalumu, jijini hapa, Kamanda Suleiman Kova, anasema wamejipanga kila eneo kuhakikisha kuwa shughuli ya upigaji kura inafanyika kwa Amani.
“vikosi vyetu viko salama vimejiandaa kukabiliana na fujo zozote zitakazoweza kujitokeza, naomba nieleweke kuwa polisi haitakuwa tayari kuwavumilia wale wote watakaosababisha vurugu, tunawachukulia hatua za kisheria,”amesema Kamishna Kova.
Kamishna Kova anasema wametoa tahadhari kwa wananchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa wakati wa zoezi hilo ili wasije wakajikuta wanaingia kwenye mgogoro bila sababu yeyote.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema polisi wamejipanga vyema kuhakiki uchaguzi huo unaenda  kwa amani na utulivu kama ulivyopangwa.
“Kutakuwa na askari waliovaa sare nadhifu, na askari wa kiraia ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wakati wote amani inatawala katika vituo vya kupigia ,“ alisema Kamishna Kova.
Moja ya kasoro zilizopelekea kutofanya uchaguzi katika baadhi ya vituo ni kuchanganywa kwa majina ya wagombea wa uenyekiti na wajumbe.
Manispaa ya Temeke  ina mitaa 10, Kinondoni 16 na Ilala 63 .
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty, ameingia kwenye mvutano  mkubwa na Chama cha Wananchi (CUF), juu ya uamuzi wake  wa kutaka uchaguzi urudiwe katika mtaa wa Mwinyimkuu ambayo inadaiwa chama hicho kilishinda.
Mwananchi

No comments: