Advertisements

Friday, October 24, 2014

WARSHA KUHUSU AMANI NA USALAMA BARANI AFRIKA YAHITIMISHWA JIJINI ARUSHA

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Magese Mulongo ya kufunga Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika na kufanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. 
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika na nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz kwa pamoja na Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Afrika Mhe. Konjit Sinegiorgis wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) alipokuwa akifunga Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika iliyowakutanisha Mabalozi, Wataalam wa masuala ya Amani na Wasuluhishi. 
Sehemu nyingine ya Wajumbe wakimsikiliza Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) akiwemo Rais Mstaafu wa Cape Verde, Mhe. Pedro Pires (kulia) 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akifuatilia kwa makini hotuba ya kufunga warsha ya amani na usalama iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani). 
Wajumbe waliokuwepo wakati wa kufunga warsha ya amani na usalama. 
kwa picha zaidi na maelezo bofya soma zaidi
Kamishna wa Amani na Usalama katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui akitoa neno la shukrani kwa Uongozi wa Mkoa wa Arusha na kwa Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuwa mwenyeji wa warsha hiyo ya siku tatu ambapo wajumbe wamenufaika na masuala yote yalijadiliwa pamoja na huduma nzuri. 
Balozi Mstaafu, Prof. Joram Biswaro (kulia) akifuatialia hotuba ya Balozi Chergui (hayupo pichani) 
Bi. Shella Mbita, Mtoto wa Balozi Hashim Mbita nae pia alikuwa mmoja wa wajumbe waliohudhuria warsha ya amani na usalama jijini Arusha (Picha zote na Rosemary Malale) 


Na. Ally Kondo, Arusha
Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika (AU) imehitimishwa jijini Arusha siku ya Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014. Warsha hiyo ambayo kaulimbiu yake ilikuwa “Silaha zisitumike kuuwa watu Barani Afrika ifikapo mwaka 2020” ilimalizika kwa wajumbe kutoa Rasimu ya Tamko la Arusha (Arusha Declaration).

Katika Tamko hilo, kumebainishwa asili ya migogoro inayohusu nchi moja au baina ya nchi na nchi nyingine, vitu vinavyochochea migogoro na ukosefu wa utulivu Barani Afrika, wanaochochea na kudhamini migogoro pamoja na athari za maendeleo ya dunia kwa Bara la Afrika.

Aidha, Tamko hilo limeainisha juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na vitendo vya siasa kali, uhalifu wa kimataifa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika amani na usalama.

Tamko limebainisha pia kuwa migogoro mingi katika nchi za Afrika inasababishwa na ukosefu wa utawala bora katika Serikali, uwajibikaji, uwazi, uongozi shirikishi pamoja na kushindwa kutatua changamoto za umasikini na ukosefu wa usawa.

Kwa mujibu wa Tamko hilo, wajumbe kwa kauli moja walikubaliana na hoja kuwa ili nchi za Afrika ziondokane na matatizo hayo, hazina budi kutekeleza miongozo na maamuzi yanayotolewa na AU kuhusu amani, usalama na uongozi. Walisema kuwa maamuzi hayo yanatoa dira nzuri ya namna ya kukabiliana na changamoto za usalama Barani Afrika, isipokuwa nchi za Afrika hazina utamaduni wa kuyatekeleza.

Hivyo, wajumbe walisisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa AU kutekeleza maamuzi yote yanayofanywa na kuridhiwa na AU, Jumuiya za Kikanda na wadau wengine.

Aidha, walitoa wito kwa nchi wanachama wa AU, Kamisheni ya AU, Jumuiya za Kikanda, Baraza la Amani na Usalama la AU na wadau wengine kulipa kipaumbele suala la kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi hayo.

Sanjari na hayo, wajumbe walipongeza mabadiliko chanya yanayotokea Barani Afrika ikiwa ni pamoja na kupungua kwa migogoro ya kutumia silaha, kuongezeka kwa chaguzi za kidemokrasia, kukua kwa uchumi na ongezeko la kasi ya kupambana na vitendo vya ufisadi katika nchi nyingi za Afrika.

Licha ya maboresho hayo, wajumbe walielezea wasiwasi wao kuhusu tishio linalotokana na changamoto mpya katika amani na usalama wa Bara la Afrika. Walihimiza umuhimu wa kutumia mbinu za kibunifu kukabiliana na changamoto hizo ambazo ni; uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uharamia, biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha na dawa za kulevya na biashara ya fedha haramu.

Wakati wa kufunga warsha hiyo ambayo iliwakutanisha Mabalozi, wasuluhishi, wajumbe maalum, wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na wasomi mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe alielezea matumani yake kuwa, washiriki walipata fursa nzuri ya kujadili kwa kina chanzo cha migogoro Barani Afrika na kupendekeza njia muafaka za kukabiliana nayo. Alisisitiza umuhimu wa mapendekezo hayo kuingizwa katika sera za kitaifa, kikanda na kimataifa ili yaweze kuwa na manufaa.

No comments: