Advertisements

Friday, October 31, 2014

Wabunge tisa wajiuzulu kumpinga Shy-Rose


Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (Eala) umechukua sura mpya baada ya wabunge tisa, wakiwamo makamishna watano na wenyeviti wanne wa kamati za Bunge hilo, kuwasilisha barua za kujiuzulu nafasi zao hizo, ikiwa ni matokeo ya sakata linalomhusisha mbunge mwenzao kutoka Tanzania, Shy-Rose Bhanji (pichani).
Kutokana na hali hiyo, Bunge hilo ambalo lilikutana kwa wiki mbili huko Kigali, Rwanda liliahirishwa jana kwa muda usiojulikana, muda mfupi baada ya kushindwa kufanya uamuzi wa kumwadhibu Bhanji ambaye anakabiliwa na tuhuma mbalimbali za utovu wa nidhamu.
Mgogoro huo ulisababisha Eala kwa wiki mbili, kushindwa kufanya lolote lililokuwa limepangwa kwenye kalenda yake, kwani kila lilipokutana, wabunge walitoa hoja liahirishwe hadi pale suala la nidhamu dhidi ya Bhanji litakapotolewa uamuzi.
Mbunge huyo anatuhumiwa kutoa maneno yasiyokuwa na staha kwa wenzake, kuwakashifu na kuwatukana baadhi ya viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa ziara ya ujumbe wa Eala katika nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), Ubelgiji.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana na baadaye kuthibitishwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi Odiko zinasema makamishna na wenyeviti tisa waliwasilisha barua rasmi za kuachia ngazi kwa Spika wa Eala, Dk Margaret Zziwa... “Ndiyo, naweza kuthibitisha kwamba wamejiuzulu nafasi zao kwa kuandika barua rasmi kwa spika… bado nafuatilia nyaraka husika na baadaye nitatoa taarifa rasmi.”
Baadaye Odiko, alitoa taarifa rasmi ambayo pamoja na mambo mengine, ilitaja majina ya makamishna waliojiuzulu kuwa ni Abubakar Ogle (Kenya), Christophe Bazivamo (Rwanda), Hafsa Mossi (Burundi) na Jeremy Ngendakumana (Burundi), Patricia Hajabakiga (Rwanda).
“Hii sasa inamaanisha kwamba ili tume iweze kufanya kazi yoyote, lazima iundwe upya kwa mujibu wa kipengele cha tatu cha Sheria ya Uendeshaji wa Bunge la Afrika Mashariki,” anasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Alipoulizwa kuhusu majina ya wenyeviti ambao wamejiuzulu, Odiko alisema asingeweza kuyataja na kwamba alikuwa akifuatilia taarifa zao katika ofisi ya spika. Eala ina makamishna 10; wawili kutoka kila nchi na wenyeviti sita wa kamati.
Kwa maana hiyo kushindwa kufanya kazi kwa Tume ya Eala hivi sasa kunatokana na kujiuzulu kwa makamishna wote wa Rwanda na Burundi, hivyo tume haiwezi kukutana bila uwakilishi wa nchi hizo.
Hata hivyo, Odiko hakueleza sababu za wabunge hao kujiuzulu lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema walisema hawawezi kufanya kazi chini ya uongozi wa Spika Zziwa kwani amekuwa akibadili uamuzi wanaoufikia kwenye vikao.
Miongoni mwa mifano waliyoitaja ni kushindwa kuwasilishwa katika Bunge hilo, ripoti ya ziara ya makamishna na wenyeviti wa kamati wa Eala nchini Ubelgiji, huku wakidai kwamba kutowasilishwa kwake kulilenga kufunika madhambi yaliyofanywa na Bhanji.
Mmoja wa waliojiuzulu, Ogle wa Kenya aliliambia gazeti hili juzi jioni kwamba asingeweza kuendelea kufanya kazi katika tume ambayo mmoja wa wajumbe wake amekuwa akiwatusi, huku Spika akishindwa kuchukua hatua.
Hukumu ya Shy-Rose
Mapema jana asubuhi, Bunge hilo lilishindwa kutoa hukumu kwa Bhanji baada ya kukosekana kwa akidi ya wabunge kutoka Tanzania, licha ya kwamba walikuwapo katika vikao vilivyotangulia.
Kanuni ya 13 ya Eala inasema akidi ya vikao ni nusu ya wabunge wa kuchaguliwa na kati yao, kila nchi mwanachama inapaswa kuwa na uwakilishi wa walau wabunge watatu kati ya wabunge wake tisa wa kuchaguliwa.
Wakati wa kufanya uamuzi, Tanzania ilikuwa na uwakilishi wa wabunge wawili tu; Nderakindo Kessy na Abdullah Mwinyi. Uwakilishi wa nchi nyingine ni Kenya (8), Burundi (8), Uganda (7) na Rwanda (9).
Kutokana na hali hiyo, Mbunge Susan Nakawuki alitoa pingamizi kwamba uamuzi hauwezi kufanyika hivyo Spika Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 kama kanuni zinavyotaka, lakini hata baada ya muda huo idadi ya wabunge haikuongezeka.
Hali hiyo pia ilijitokeza juzi mchana wakati wa kutaka upigaji kura ya kuamua iwapo Bhanji ang’olewe kwenye ukamishna pale akidi ya wabunge wa Tanzania ilipokosekana, licha ya kwamba kabla ya hatua hiyo, walikuwamo ndani ya ukumbi wa Bunge.
Juzi, mchana wakati mjadala wa hoja dhidi ya Bhanji iliyowasilishwa na Mbunge wa Uganda, Dorah Byamungu ukielekea ukingoni, Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia baadhi ya wabunge wa Tanzania wakitoka nje mmoja baada ya mwingine na walibaki watatu tu; Kessy, Mwinyi na Angela Kizigha.
Spika Zziwa aliahirisha kikao hicho kwa dakika 15 kwa mapumziko na aliporejea wabunge wa Tanzania walikuwa wamebaki wawili baada ya Kizigha kulazimika kuondoka kuwahi ndege kurejea nchini ambako alikuwa na majukumu mengine.
Katika mazingira hayo, Kanuni ya 18 hoja ya kumng’oa Bhanji katika ukamishna inapaswa kuwa moja ya kazi za Bunge hilo litakapokutana. Hata hivyo, haifahamiki ni lini litakutana kutokana kukosekana kwa idadi ya makamishna wanaopaswa kuunda tume ya uongozi.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

What shame, Ms Bhanji if the allegations are so strong to the point people are making stand about your moral compass than it stands to reason your integrity in that forum has been compromised. Thus means it will not be easy to walk with your head held high. Do your best to own up, a good leader or person had to take responsibility for their short falls. So so sad to see you fall in grace.