Advertisements

Thursday, October 30, 2014

TUTASHIRIKIANA NA WAPENDA AMANI KUISAIDIA DRC KUWA NA AMANI-TANZANIA


Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa Mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikijadili ajenda kuhusu tathmini ya jumla ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zinazochangia wanajeshi wake katika operesheni hizo za ulinzi wa amani.


Sehumu ya wajumbe wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakifuatilia majadiliano ya ajenda kuhusu Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imeihakikishia  Jumuiya ya Kimataifa  ya kuwa itaendelea  kushirikiana na wapenda  amani katika kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC)  kuwa  na amani na usalama.
Akichangia majadiliano  juu ya ajenda inayohusu  tathimini  ya  jumla  ya Operesheni za Ulinzi wa Amani  chini ya Umoja wa Mataifa.  Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi amesema, Tanzania inafanya hivyo kwa kutambua wajibu wake katika  medani  ujenzi wa amani ya Kimataifa.
Amesema  pia  kuwa, ni kwa kutambua wajibu huo ,ndiyo sababu iliyoifanya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano  wa Tanzania kufikia makubaliano na nchi  wanachama wenzie  katika SADC na  Maziwa  Mkuu  ( ICGLR), kujitolea  kupeleka wanajeshi wake huko  DRC ili  kuunga   mkono juhudi za kuwasaidia wananchi wa  DRC kuwa na amani , usalama  na maisha  yenye uhakika.
Balozi Mwinyi amesema  kuwa Tanzania inajivunia  kuwa  wanajeshi wake  wanaohudumu kupitia FIB   ambayo ni sehemu ya     MONUSCO  licha ya  mazingira magumu na hatari wanayokabiliana nayo wameonyesha  umahiri  mkubwa  ikiwa ni pamoja na kujitoa muhanga maisha yao kuwalinda raia wasiokuwa na hatia DRC  pamoja na kurejesha amani na  usalama.

 Kwa sababu hiyo, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, amesema ni vema na haki ,  kujitoa  muhanga huko kwa wanajeshi  wanaohudumu  FIB kutambuliwa na wapenda amani wote na  vile vile  FIB iendelee kupata  uungwaji mkono stahili.
Aidha  Balozi Mwinyi amesema,  kutokana  mabadiliko ya  mwenendo mzima wa   machafuko  na vita  katika maeneo mbalimbali  Barani Afrika, ikiwa ni  pamoja na  matishio na kutumika   kwa  mbinu za kigaidi na mabomu ya kutengenezwa  kienyeji kunalazimisha  kufanyika mabadiliko katika  mfumo mzima wa  ulinzi wa Amani.
Amesema,  mabadiliko hayo     yanapelekea Umoja wa Mataifa  kulazimika kuidhinisha matumizi ya  mamlaka nguvu katika baadhi ya misheni zake  kutokana na ukweli kwamba matishio hayo  siyo tu ni  hatari kwa raia lakini pia   yamekuwa tishio kwa walinzi wa amani.
Kwa sababu hiyo, Tanzania imetaka kuwapo kwa  majadiliano ya kina ndani ya Umoja wa Mataifa  kuhusu dhana nzima ya  mabadiliko ya mwenendo wa  machafuko  na  vita vinavyoendelea na hatari inayowakabili  walinzi wa amani  pamoja na matumizi ya  nguvu kuwa sehemu ya mamlaka  nguvu ya misheni nyingi.
“ Tunahitaji majadiliano ya kina katika eneo hili,    kwa sababu, mwenendo wa machafuko  na mbinu za maaduzi  zimebadilika kabisa.   Kuna  matumizi  makubwa ya mbinu za  kigaidi na  mabomu yanayotengenezwa kienyeji, haya yote na mengine  mengi yanabadilisha kabisa historia ya  asili ya ulinzi wa amani”, amesisitiza Balozi Mwinyi.
Vile vile amesema,   majadiliano ya kina yanahitajika katika eneo la matumizi ya teknolojia za kisasa katika operesheni za kulinda  amani, zikiwamo ndege za kiuchunguzi zisizoendeshwa na  binadamu ( UAS).
Amesema hapana  shaka,  kama walivyozungumza  wajumbe wengine, matumizi ya  teknolojia hizo pamoja na umuhimu wake yanahitaji   majadiliano  ya kina na  makubaliano ya pamoja.
Aidha  Balozi Mwinyi amesema , Tanzania inakaribisha nia ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kufanya mapitio ya  Operesheni za Ulinzi  wa Amani za Umoja wa Mataifa ( UNPKOs)  na   Misheni  Maalumu za Kisiasa( SPMs). Na   ameahidi  kuwa   Tanzania itashiriki kikamilifu katika mchakato huo.
Awali  akizugumza mwanzoni mwa  majadiliano  hayo Mkuu wa Idara ya Operesheni  ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa  ( DPKO) Bw.  Herve Ladsous, amezungumzia mafanikio na  changamoto mbalimbali  zinazokabili shughuli za ulinzi wa amani.
Amesema katika DRC, Misheni ya Kulinda   Amani  ( MONUSCO) ambayo  ndani yake kuna FIB imeonyesha umahiri  na ujasiri mkubwa wa kutokubali kurudi nyuma katika mapambano yake dhidi ya makundi ya waasi yenye silaha.
Akasema uchupavu na uhodari huo, licha ya kutoa ulinzi kwa raia pia umefungua fursa mpya ambapo mamlaka za kiutawala za DRC zimeweza kutawala maeneo ambayo huko nyuma yalikuwa yakishikiliwa na kukaliwa na makundi ya waasi.
Katika majadiliano  hayo wazumgumzaji wengi wameelezea kusikitishwa kwao na  ongezeko la vitendo vya kuvamiwa kwa walinzi wa amani na  kusababisha wengi wao kupoteza maisha.
Wakasema,  jambo hilo halikubaliki na halipashwi kuendelea kufumbiwa  macho na kwamba ni j lazima pafanyike utafiti wa kina  wa kwanini kumekuwa na ongezeko la mashambulizi kwa walinzi wa amani . na wametaka   wahusika wa hujuma hizo watafutwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Wachangiaji wengine wameshauri    na kutoa wito  kwa  Umoja wa Mataifa kupitia DPKO na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya  operesheni za ulinzi wa amani, kuangalia upya  mazingira ya utendaji kazi  ya walinzi hao wa amani, ikiwa ni pamoja na  kuwapatia mafunzo zaidi  yanayoendana na wakati, vifaa na zana za kisasa na  vya uhakika,  malipo stahili na pia mamlaka zinazotekelezeka.

No comments: