Advertisements

Friday, October 31, 2014

Mkapa atoa ya moyoni rais 2015

Rais Mstaafu,Benjamin Mkapa.

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, amezungumzia mbio za kuwania urais wa 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitaja sifa za mtu anayepaswa kuteuliwa kuwa mgombea wake, ikiwamo ya kukubalika na kuuzika kwa jamii.

Amesema kukubalika na kuuzika kwa mtu katika siasa kunatokana na utendaji, haiba, wasifu na ushawishi wa mtu huyo ndani ya chama na serikalini na kwamba, umri siyo kigezo cha kuangaliwa ingawa siyo dhambi vijana wakajitokeza kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Mkapa, ambaye anasifika kwa kuwa kiongozi jasiri na asiyemung’unya maneno, alisema hayo wakati akihojiwa na televisheni ya Citizen ya nchini Kenya, kwa njia ya simu.

Alikuwa akihojiwa juu ya kifo cha Rais wa Zambia, hayati Michael Satta, aliyefariki dunia, jijini London, nchini Uingereza Jumanne wiki hii.

Katika mahojiano hayo, Mkapa pia aliulizwa na mwandishi kuhusu Tanzania kutazamiwa kufanya uchaguzi mkuu mwakani huku mambo mengi yakisikika, hasa kwa wanaojitokeza kupitia CCM kutaka kuwania urais katika uchaguzi huo hadi wengine kufikia kuadhibiwa na chama.

Kabla ya kujibu, Mkapa alianza kwa kucheka na kisha akasema anachelea kupata jibu sahihi kuhusiana na swali aliloulizwa na mwandishi.


“…Ila niseme CCM ni chama kikongwe na kina hazina kubwa ya kutosha. Na Katiba ya chama chetu inaelezea kuhusu dhumuni la chama chetu, kubwa ikiwa ni kuhakikisha tunakamata dola, kuanzia serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Sasa swali ni kwamba, dola inakamatwaje?” alihoji Mkapa.

Aliongeza: “Chama kama chama lazima muwe na mtu anayeuzika na kukubalika katika jamii kwa utendaji wake, haiba yake, wasifu wake (ndani ya chama na serikali).

“Lakini vile vile, ushawishi wake...Haya mambo ya umri na kadhalika, sisi hatukutazama wakati huo. Ila siyo dhambi vijana wakijitokeza. Maana yake hata wakati wangu, Rais wa sasa Mheshimiwa Kikwete na kina Lowassa walijitokeza. Na leo unaona Kikwete ndiye Rais.”


Alisema wakati wa utawala wake, viongozi wenzake wengi walihisi na kuamini kuwa hakuwa akimuunga mkono Rais Kikwete.

“Lakini mwandishi, nataka nikuhakikishie, hata kama mimi Ben Mkapa siko na Kikwete, mwisho wa siku wanachama ndiyo watakaosema wewe humtaki ila sisi tuachie huyo huyo...,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Na hayo yalijitokeza mwaka 2005. Watu walimtaka Mheshimiwa Kikwete. Sasa mimi kuwa mwenyekiti wa chama hakunipi Mandate (mamlaka) ya kushindana na walio wengi. Na mliona (Kikwete) alishinda kwa asilimia kubwa kweli kweli”.

“Hivyo CCM ina taratibu zake na wanajua nani anafaa. Maana yake siasa hizi, tuhuma zingine za kipuuzi kweli kweli. Sasa mkiendekeza tuhuma, mwishowe mnakuta mnabaki bila chama. Na kwenye siasa mkianza kutuhumiana, hakuna wa kusimama...”

Alisema yeye binafsi, anaamini chama kitapata mtu safi, mwenye nguvu ya kukisaidia chama na serikali na kuendeleza yatakayoachwa na Rais Kikwete.

Mkapa alisema hakuna chama duniani kinachoona fulani atakivusha halafu kimwache na kusema kufanya hivyo, maana yake ni kukiua chama.

“Hivyo, hata sisi vyombo vyetu vya ndani vilikuwa vinatueleza kabisa kwamba, fulani yuko vizuri sana. Ila labda kuna aka katatizo. Sasa ako katatizo tunakafanyia kazi kwa maslahi ya chama na kwa maslahi ya huyo ajaye,” alisema Mkapa na kuongeza kuwa ana amini ndivyo ilivyo mpaka sasa.

Alisema tafiti zimefanyika na kwamba, anaamini wamesikika watu wakisema wanamtaka nani.

“Na wakati wangu mimi mgombea alikuwa ameshatungiwa nyimbo na watu mbalimbali wenye mapenzi naye. Hivyo, labda hata sasa yaweza kuwa hivyo...Waswahili walisema nyota njema huonekana asubuhi,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Nimalizie kama nilivyosema, ukongwe wa CCM na viongozi wake, naamini watapata mtu bora na mwenye nia njema na Taifa hili...”

Akijibu kuhusu wana CCM waliotajwa kwamba, anaamini yupo mmoja au wawili, ambao ameona wanaweza ama kufuata nyayo zake au za Mwinyi au za Mwalimu Nyerere au za Rais Kikwete, kwanza alianza kwa kucheka.

Baada ya kicheko, Mkapa alisema Tanzania kuna Kamati ya Maadili na kwamba, yeye na wenzake hivi sasa kikatiba ni wazee washauri, hivyo akasema vikao vya chama ndivyo vitakavyowaongoza na baada ya hapo, nao wanaenda na mtu huyo huyo.

Makada wa CCM waliowahi kutuhumiwa kuanza kampeni za kuwania urais mwaka 2015 kabla ya kuzuiwa na chama kupitia Kamati yake Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kujihusisha na suala hilo kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa, ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira.

Yumo pia aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pia hivi karibuni alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akitangaza nia yake ya kuwania urais 2015. Mwingine aliyekwisha kutangaza nia ya kuwania urais mwakani ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla.

KUHUSU USHIRIKIANO WA VYAMA VYA UPINZANI (UKAWA)

Akijibu swali kuhusu ushirikiano uliosainiwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD wa kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi, kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa hadi urais kama ilivyokuwa kwa Kenya, Mkapa alisema bado hajajua
sera za vyama hivyo na namna makubaliano yao yalivyo.

Alisema pia bado hajaelewa kama inawezekana kuufananisha ushirikiano wa vyama hivyo na muungano wa Coard na Jubilee uliokuwapo nchini Kenya.

“Otherwise I'd like to wish them all the best (vinginevyo ningependa kuwatakia kila kheri),” alisema Mkapa na kumfanya mwandishi aangue kicheko.

KIFO CHA RAIS SATTA

Akimzungumzia hayati Rais Satta, Mkapa alisema hakuitwa “King Cobra” kimakosa, bali alistahili kutokana na uwezo aliokuwa nao ama wa kimaamuzi au wa kimsimamo.

“Nina hakika sana kwamba Wazambia na sisi kama Mataifa ya Afrika tutamkumbuka daima ndugu Satta. Satta daima alikuwa kwa ajili ya watu wake na Bara letu kwa jumla. Alisema na kusimamia kile alichokiamini kuwa ni cha kweli na chenye mafanikio, Satta ataendelea kuwa kiongozi mzuri daima,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Hivyo, maumivu yanayotukabili kwa kumpoteza Mzee Nyerere, Mzee Nkrumah, Mzee Mandela, Mzee Kenyatta ni sawa na yale yanayotukabili leo tunapomjadili Mheshimiwa Satta (Inatosha kusema kwamba tumempoteza shujaa mwingine katika Bara letu) Naitakia roho yake mapumziko ...”

Akijibu swali namna anavyoziona siasa za Afrika akiwa Rais mstaafu, Mkapa alisema ni kawaida na hana jambo kubwa la kusema japo kuna mengi yanatokea, ambayo mengine ni ya hovyo.

“Mathalan, Waafrika wazee wetu, walipigania sana ukombozi wetu. Ila nadhani wengi bado kuna watu wana matatizo na wanahitaji kukombolewa kifikra,” alisema Mkapa.

Aliongeza: “Maana yake kuna wenzetu wanatumika pasipo kujua na kusababishia nchi zao kuingia katika matatizo, kama vita na wengi wao wameanza kujuta”.

“Hivyo, ni lazma ifikie mahali watu waweze kujitambua na kujua ni yepi malengo mema kwa Bara letu ni yepi tunashinikizwa...” aliongeza kusema Mkapa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: