Advertisements

Friday, October 24, 2014

HOFU YA UGONJWA WA EBOLA YATANDA MJINI MOSHI

Lango kuu la kuingia zahanati ya Shirimatunda likiwa na tangazo la kusitishwa kwa huduma za afya katika zahanati hiyo kwa hofu ya kuwapo kwa mgonjwa wa Ebola.
Baadhi ya wagonjwa na wauguzi katika zahanati ya Shirimatunda wakihamia katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Shirimatunda kuendelea na huduma za tiba ikiwamo utoaji wa chanjo ya Surua na Rubella


KAZI wa kata ya Shirimatunda katika maanispaa ya Moshi, wameingiwa na hofu ya kupoteza maisha yao,kufuatia taarifa za kuwapo kwa mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa hatari wa Ebola anayehudumiwa katika zahanati ya kata hiyo.

utokana na hofu hiyo,halmashauri ya manispaa ya Moshi imelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana zahanati hiyo na kuwahamishia wagonjwa katika hospitali nyingine ikiwamo ya St Joseph katika manispaa hiyo.

Ripota wetu ambaye alikuwa eneo la zahanati hiyo alishuhudia baadhi ya madaktari wakiongozwa na mganga mkuu wa manispaa hiyo,Dk Christopher Mtamakaya pamoja na wataalamu wengine wa afya wakifanya kikao cha dharura kujadili hali hiyo.


Kadhalika,waandishi wa habari waliokuwepo katika zahanati hiyo walishuhudia baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa na mavazi rasmi yanayotumiwa na madaktari wanaohudumiwa wagonjwa wa Ebola.Pamoja na kikao hicho,Zahanati hiyo imewekwa tangazo katika lango kuu
linalosomeka 'Huduma zote za afya zimesitishwa kwa muda, Utawala' hali
ambayo imeendelea kuzua maswali mengi kwa wagonjwa wanaokwenda kupata
matibabu katika zahanati hiyo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kigongoni,kata ya Shirimatunda ilipo zahanati
hiyo,Juma Sambeke alisema hajashirikishwa katika maamuzi ya kugeuza
Zahanati hiyo kama Karantini ya mtu anayedhaniwa kuwa na Ugonjwa wa
Ebola.

Alisema kuwapo kwa karantini hiyo kumeanza juzi majira ya saa 10 jioni
baada ya kupokea taarifa kutoka afisa mtendaji wa kata hiyo kwamba
zahanati hiyo itafungwa kwa muda ili kumhudumia mtu anayedhaniwa kuwa
Ebola.

"Manispaa haikuwa sahihi kuitumia zahanati hii kama karantini ya hofu
ya Ebola, hapa kuna shule ya chekechea, sekondari, seminari ya Don
Bosco na majirani kama unavyowaona....wasipopewa elimu na kama huu ni
ugonjwa wa Ebola watu watakufa sana"alisema.

Sambeke alisema maeneo yatakayoathirika zaidi na kufungwa kwa zahanati hiyo ni Shirimgungani,Cherereni ya Moshi vijijini,Karanga, Soweto,Bonite madukani na mtaa wa Kigongoni ambapo zahanati huudumia zaidi ya watu 5,000 kwa mwezi.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Shirimatunda,Felix Mushi alisema
huduma za utoaji wa chanjo ya magonjwa ya Rubella na Surua
zimehamishiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata hiyo huku wagonjwa
wengine wakihamishiwa maeneo mengine.

Alisema tarifa za awali alizopata ni kwamba mtu huyo alipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA), ambapo alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kuwa na dalilizinazoashiria ugonjwa wa Ebola.

Aidha taarifa zaidi zinadai kuwa wataalam wamechukua sampuli kutoka kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo, ili kujiridhisha, wakati huduma nyingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa kusafiri kutoka nchini Senegal.

Mmoja wa wakazi anayeishi jirani na zahanati hiyo, Thadei Sangawe,alisema ameanza kufanya mawasiliano na ndugu wengine waliopo maeneo mengine mkoani humo ili aweze kuhamisha familia yake kuepuka madhara kama ugonjwa huo utakuwa wa Ebola.

"Tunaomba viongozi wenye dhamana hususani madaktari watoe taarifa kwa
wananchi juu ya hii hofu iliyopo,maana kukaa kwao kimya kutasababisha
wananchi washindwe kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha
madhara"alisema.

Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi wa manispaa
ya Moshi Shaban Mtarambe, alisema hayuko tayari kuzungumza kwa maelezo
kuwa suala hilo ni la kitaalam zaidi linalohitaji waataala wa kada ya
afya kulizungumzia.

Naye mganga mkuu wa manispaa ya Moshi,Dk Christopher Mtamakaya
alipohojiwa kuhusiana na taarifa za kuwapo kwa mgonjwa huyo hakuwa
tayari kuzungumza zaidi na alipotumiwa ujumbe wa simu ya mkononi
alijibu kwa kifupi, huo ni Uvumi.

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa huo,Dk Mtumwa Mwako alipohojiwa kuhusiana na kuwapo kwa mgonjwa huyo naye alisema hafahamu na aliomba
kupewa muda kwani alikuwa katika kikao.Kuhusiana na suala la mgonjwa huyo,katibu tawala wa mkoa huo, DkFaisal Isa alisema taarifa za kwanza anapata kutoka kwa mwandishi wetu
na akaomba muda wa kufuatilia zaidi.

2 comments:

Anonymous said...

tanzania nchi yangu naipenda ila kwa kuficha mambo.mpaka itokee ya siera leone ndo watasema.hata elimu kwa wananchi wala haitiliwi mkazo kivile.mungu tusaidie lakini isiwe kweli.maanake na hizi rushwa wengi tutateketea.Luke asante kwa taarifa usisite kuziweka kila upatapo hizi habari.

Anonymous said...

Asante swala sio kufunga hozpitali. majuzi tu serikali imedai haina vipimo vya kupima kugundua ugonjwa huu!! Tangu umeanza kutangazwa serikali imechukua jukumu gani na kuandaa sehemu maalumu endapo atagundulika mgonjwa ili asikutane na watu wengine na wahudumu wa hospitali kupatiwa mafunzo pia na vifaa!! hii ni aibu Tanzania fedha zinawekwa mifukoni tu kwa nini? Waziri mhusika na afya uko wapi na hata Rais Kikwete umelionaje hili!!