Advertisements

Friday, October 24, 2014

Chadema wapata hati ya shaka ya Mkaguzi Mkuu

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu akionyesha nakala za hati walizokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata hati yenye shaka kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake zinazoishia Juni 2011/12 na 2012/13
Ukaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 7 ya mwaka 2009, unampa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.
Katika ripoti hiyo kwa hesabu zilizoishia Juni 30, 2012, CAG ametilia shaka maeneo mbalimbali. Mkaguzi anasema katika ripoti hiyo kuwa Chadema kilionyesha kina mali zenye thamani zaidi ya Sh650 milioni, ambazo ni magari, mashamba, nyumba na pikipiki. Hata hivyo, CAG anasema hakuona kitabu cha usajili wa mali hizo.
Pia, ripoti hiyo inaeleza kuwa Chadema ina akaunti zaidi ya 200, ikijumlisha akaunti za makao makuu, kanda, mikoa, wilaya na majimbo. Shaka ya mkaguzi ni kwamba hakuona salio la kufungia kitabu likihusisha akaunti zote zinazotumia jina la Chadema.
Chadema kilitoa utetezi wake kuwa akaunti kuu ya chama ndiyo inatoa fedha kwa akaunti za mikoani, hivyo wanaona mgao huo wa fedha ni sehemu ya matumizi yao.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu alisema Chadema iliwasilisha salio la akaunti kuu kwa kutambua kuwa akaunti za mikoani zinapokea fedha kutoka makao makuu, hivyo waliona hiyo ni sehemu ya matumizi yao.
“Chama chetu kimepokea taarifa aliyoitoa CAG na tunaichukua kama sehemu muhimu ya kuboresha ujenzi wa chama chetu kama taasisi ya kudumu na inayokua. Tutazifanyia kazi changamoto zote alizoziainisha,” alisema Komu.
Aliongeza kuwa chama chake kinamtaka CAG aweke bayana ni vyama vingapi havijakaguliwa na lini vitakaguliwa. Alivitaka vyama vingine vilivyokaguliwa vitoe taarifa zao ili Watanzania wajue.
“Tunakumbuka CAG alitoa kauli bungeni kuwa si vyama vyote vimekaguliwa. Kama sehemu ya jamii na chama kinachopigania utawala wa sheria, aweke wazi ni vyama gani havijakaguliwa na kwa sababu gani,” alisisitiza mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri, John Mrema alisema mpaka kufikia jana (juzi) walibaini kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa hakijakaguliwa hesabu zake.
Alisema waliamua kupigania CAG kukagua hesabu za vyama vya siasa kwa sababu mwaka 2005 walibaini kuwa CCM ilitumia fedha za EPA katika kampeni zake. Aliongeza kuwa hawakutaka utamaduni huo ujirudie.
“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma mpaka kufikia jana, CCM kilikuwa bado hakijakaguliwa,” alisema Mrema na kuongeza kuwa chama chake kimeonyesha mfano licha ya mapungufu yaliyobainika.
Alipouliza juu ya kukaguliwa kwa chama chake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Chadema wanakuja na jambo ambalo lilishatolewa ufafanuzi siku nyingi. Alisema chama chake kilieleza na kutoa vithibitisho kuwa walikaguliwa.
Nnauye aliongeza kuwa CAG pia alilitolea maelezo jambo hilo mara nyingi kusisitiza kuwa alishakikagua Chama cha Mapinduzi.
“Sasa hawa Chadema wamegeuka kuwa wasemaji wa CAG? Kwanini nanyi msiende kumuuliza CAG juu ya jambo hili. Ina maana mmeshasahau tuliyowahi kusema au aliyowahi kueleza CAG juu ya ukaguz?” alihoji .
Nnauye na kusisitiza aulizwe CAG.
Hata hivyo, imebainika kuwa utekelezaji wa sheria ya ukaguzi wa vyama vya siasa umeanza kutiliwa mkazo miaka ya hivi karibuni, huku Chadema kikimsukuma CAG kufanya ukaguzi kila mwaka.
Kwa hesabu za mwaka ulioishia Juni 30, 2013, ripoti ya CAG imetilia shaka kutoonekana kwa kitabu cha makusanyo ya fedha chenye namba 451 – 500 kilichorekodiwa katika vitabu vyao kuwa kilikusanya zaidi ya Sh31 milioni.
Kadhalika, mkaguzi mkuu alihoji ununuzi wa magari 10 ya CMC (Ford Rangers) bila kushirikisha kamati ya zabuni ambayo ndiyo ina dhamana na manunuzi yote ya kichama. Hata hivyo, Komu alifafanua kuwa uamuzi ulifanywa na kamati kuu na kamati ya katiba kupewa taarifa.
Ununuzi wa jenereta lenye thamani ya Sh27.5 milioni unaelezwa zabuni haikutolewa kwa ushindani, jambo ambalo mkurugenzi wa fedha alisema walifanya utafiti na kubaini kuwa ni kampuni moja tu ndiyo ilikuwa na jenereta waliyoihitaji.
Mwananchi

No comments: