Advertisements

Friday, October 24, 2014

Chadema walaani Meghji kuipigia kura Zanzibar

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Sengerema, Mwanza. Kushoto ni Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche. Picha na Ibrahim Yamola

Sengerema. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitendo kilichofanywa na uongozi wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba cha kumfanya Mjumbe wa Bunge hilo, Zakia Meghji kupiga kura kama Mzanzibar badala ya ‘Mtanzania Bara’ ni ‘uhuni’ unaotakiwa kuchukuliwa hatua na wananchi.
Hayo yalisemwa juzi na viongozi wa Mabaraza ya Wanawake na Vijana ya Chadema (Bawacha) na (Bavicha) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi, Segerema mkoani Mwanza.
Kauli hiyo wameitoa ikiwa ni saa 48 baada ya gazeti hili kubainisha utata wa kura ya Meghji wakati wa kuipitisha Katiba inayopendekezwa kupiga kama mjumbe kutoka Zanzibar badala ya Tanzania bara kama alivyotakiwa.
Akihutubia mamia ya wananchi, Mwenyekiti mstaafu wa Bavicha, John Heche alisema, “Kilichofanywa na Sitta (Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta) cha kumbadilisha dakika za mwisho Meghji kuhalalisha Katiba yao ni uhuni ambao Watanzania wanatakiwa kuwawajibisha kupitia kura ya maoni.”
Aliongeza: “Hivi kweli inawezekanaje mtu katika vikao vyote awe anahesabika kama mjumbe kutoka Tanzania Bara halafu dakika za majeruhi baada ya kuona wanachokifanya hakitapata theluthi mbili, hususani Zanzibar wampeleke huko….”?
Huku akishangiliwa na umati huo, Heche alisema wajumbe wa CCM wameondoa tunu za taifa za uwazi na uadilifu baada ya kuona zimewabana.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bawacha, Hawa Mwaifunga alisema wanawake wakiacha kutumika na CCM. hususani nyakati za chaguzi zinapokaribia wataifanya nchi hii iliyokosa maendeleo kwa miaka 52 baada ya uhuru kusonga mbele.
“Wanawake wenzangu nawaombeni mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali lakini pia kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na makazi ili muweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi hizo,” alisema Mwaifunga
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega alisema,”Nawasihi wanawake wenzangu na vijana wenye sifa kwenda kujiandikisha ili kuweza kuwa na sifa ya kuchagua na kuchaguliwa...wanawake msiache kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani tunaweza.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Kunti Yusuph alisema nchi hii imefika hapa kutokana na kuwakumbatia viongozi wasiotimiza wajibu wetu.
“Watanzania leo kupata huduma bora ni anasa, kuapata huduma za afya, elimu na maji navyo ni anasa hivyo tuchukue hatua kupitia uchaguzi wa serikaki za mitaa kubadili uongozi,” alisema Yusuph
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

chadema mnajitahidi sana na lakini
Haya yote ni makelele, mwisho wa siku ccm watashika tena hatamu kama walivyo weza kuchakachua katiba ya Tanzania na kuifanya iwe katiba ya ccm. kama wameweza kulifanya hili kipi watashindwa na cha zaidi wanaoumia ni wananchi walala hoi. Hii nchi inaongozwa na mafisadi, usipo kubaliana nao lazima wakutose! Tusubiri tuone huo uchaguzi kama hawatauchakachuwa kama walivyo fanya katika katiba mchana kweupeeee bila hata ya aibu.mweeee!.

jitahidini makomando wa chadema kuna siku may be mtashika nchi may be mungu mkubwa hakuna kinachoshindikana pakiwa na nia.