Advertisements

Tuesday, September 2, 2014

Ukichukua fedha benki sasa ni roho mkononi

Dar es Salaam. Ni roho mkononi. Hayo ndiyo maneno matatu yanayofaa kuelezea hali ilivyo jijini Dar es Salaam na maeneo kadhaa nchini kwa sasa, hasa pale mtu anapobeba fedha nyingi.
Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki.
Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Salum Mashati alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha akitoka benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20, wanajuaje kuwa una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki uhalifu huu.”
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki lililopo Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe alikanusha madai hayo... “Si kweli kwamba benki zinashirikiana na majambazi kufanya uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers) hawaruhusiwi kuingia na simu wanapohudumia wateja.
“Hata mteja anapoingia benki hukatazwa kuongea na simu au kuandika ujumbe. Mazingira tuliyojiwekea hayaruhusu kabisa mawasiliano kati ya benki yetu na watu wa nje wakati wa kazi. Nadhani vitendo hivi vya ujambazi vinaanzia kwa wateja wenyewe kutoa taarifa juu ya mipango yao kwa watu ambao si waaminifu,” alisema.
Kauli ya Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alitupa lawama kwa wananchi akisema wamekuwa hawaombi ulinzi wa polisi wakati wa kupeleka au kuchukua fedha benki.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwahi kutoa wito pia kwa taasisi za fedha kulindwa na polisi badala ya walinzi binafsi.
“Wakuu wa benki wanaogopa gharama za ulinzi kwa jeshi la polisi ili kuhakikishiwa usalama lakini mwishowe wanaibiwa kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya kile ambacho wangelipa kwa polisi,” alisema.
Baadhi ya matukio
Juni 23, mwaka huu, Sista wa Shirika la Mtakatifu Maria, Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka, Dar es Salaam, Clecensia Kapuli aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City na kuporwa fedha.
Agosti 8, mwaka huu, Meneja wa Kampuni ya ununuzi wa korosho na ufuta ya Olam, Jaffari Mgumba aliporwa Sh47 milioni baada ya kuchukua fedha za ushirika katika Benki ya DTB Tawi la Quality Plaza.
Mtu mwingine ambaye jina lake halikufahamika alichukua mkopo wa Sh10 milioni, lakini kwa bahati nzuri, kiasi fulani cha fedha kilibaki benki na kingine akafanya malipo palepale na wakati anaondoa akiwa amebaki na Sh2 milioni alivamiwa na majambazi waliomtaka awapatie Sh10 milioni alizochukua.
Tukio jingine la hivi karibuni ni kuuawa kwa mmiliki wa Kampuni ya Sowers African iliyopo mkabala na Mlimani City, Adson Cheyo Agosti 22, mwaka huu alipokuwa akitoka Benki ya KCB kuchukua na kuporwa fedha hizo.
Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na ujumbe uliokuwa ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukionya watu kutembea na fedha nyingi katika maeneo ya Mlimani City, Millennium Tower na Kibo Complex kwa madai si salama.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

Hii ni syndicate inayo wahusisha wafanyakazi wa mabenki, polisi na wafanyakazi wa makampuni ambayo muhusika(target) anatoka.Ni common sense ambayo mtu haitaji kusomea intelligence kubaini hili.wakati umefika kitengo cha upelelezi kiache kufanyakazi kwa mazoea,wanapaswa kushirikiana na TCRA kumonitor mawasiliano ya baadhi ya wafanyakazi wa mabenki ili kulibaini hili,ili waweze kuokoa maisha ya wananchi.Vilex2 mabenki yanabaswa kufanyia kazi CCTV cameras zilizoko kwenye mabenki hayo ili kubaini watu waliona mazoea ya kuzururax2 nje na ndani ya mabenki hayo.Kumbuka"a crime of a 21st.century will only be sorved by a solution of a 21st century".