Advertisements

Tuesday, September 2, 2014

Ikulu: Rais hakuwaomba Ukawa warejee bungeni

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu. Picha na Maktaba

Dodoma. Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete hakuwaomba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), warejee kuendelea na vikao vya Bunge hilo.
Ukawa ni umoja unaoundwa na wajumbe ambao ni wanachama wa vyama vya siasa vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF waliosusia Bunge la Katiba tangu Aprili 16, mwaka huu kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu alisema suala la Ukawa kurejea bungeni haikuwa ajenda kuu ya mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Kilimani, mjini Dodoma juzi na badala yake kulikuwa na majadiliano ya jumla mchakato wa Katiba.
Katika mkutano huo ulioratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), viongozi wa Ukawa walikuwa sehemu ya ujumbe uliokutana na Rais Kikwete kwa ajili ya kuzungumzia mambo mawili; mchakato wa Katiba na jinsi ya kuwa na uchaguzi bora wa 2015.
“Hilo suala halikuwa ajenda ya mkutano, hivyo kusema Ukawa wamemgomea Rais siyo kweli,” alisema Rweyemamu ambaye alikuwa akirejea habari iliyoandikwa na gazeti hili jana kuhusu yaliyojiri katika mkutano wa Rais Kikwete na viongozi hao.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa na kwamba watakutana tena na Rais Kikwete Septemba 8, 2014 baada ya kamati ndogo iliyoundwa kukamilisha kazi yake. Kamati hiyo inawajumuisha viongozi wa vyama vya siasa ambavyo mbali na kwamba ni wanachama wa TCD, ndivyo vimekuwa vikivutana kuhusu mchakato wa Katiba.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye ataongoza kamati hiyo na wajumbe wake ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Ukawa wamekuwa katika mvutano na CCM, ambayo katika kikao cha Kamati Kuu yake wiki mbili zilizopita, ilitoa taarifa kwamba inaridhika jinsi mchakato unavyokwenda ndani ya Bunge Maalumu na kuwataka wajumbe walitoka nje warejee bungeni.
Mwananchi

No comments: