Advertisements

Friday, July 25, 2014

Sitta aachwa njiapanda

  Ni kuhusu kupatikana Katiba mpya
  Wadau wakata tamaa kukosekana suluhu
  Wamwangukia Rais Kikwete, Ukawa
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.

Zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba kuanza tena mjini Dodoma, giza nene bado limegubika, huku kukiwa na uwezekano mdogo wa kupatikana kwa katiba mpya.

Hali hiyo inatokana na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushikilia msimamo wao wa kutorejea kwenye bunge hilo, wakitaka masharti yao yatimizwe.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali, wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, asasi zisizo za kiserikali, waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana, walionyesha wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa upatikanaji wa katiba mpya kwenye awamu ijayo ya bunge hilo.

SHEIKH ALHAD
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Musa Salim, alisema uko uwezekano mkubwa wa katiba mpya kutopatikana kutokana na hali iliyopo ya makundi yenye maslahi binafsi.

Alisema kuwapo kwa makundi tofauti, kama ya siasa na wale wanaowania urais mwakani, imekuwa ni sababu mojawapo inayokatisha tamaa juu ya upatikanaji wa katiba mpya.

“Uchaguzi wa 2015 tutaendelea na katiba ya zamani. Yote hayo yamesababishwa na viongozi wasio na mapenzi mema na nchi, hasa kwa kuangalia haja ya Watanzania, nikiyalinganisha naona huenda katiba mpya isipatikane,” alisema Sheikh Salim.
Aliwataka Ukawa kukubali kutatua tatizo kwa sababu wote wakitumia nguvu hakuna kitakacholeta mafanikio.

ASKOFU SHOO
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God Jimbo la Kilimanjaro, Giorius Shoo, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kuua mchakato wa katiba mpya kutokana na itikadi za kisiasa pamoja na msimamo wake usio na tija kwa Watanzania kilichojiwekea.

“Bila kumung’unya maneno CCM ina uwezo wa kujenga au kubomoa. Hivyo, Rais Jakaya Kikwete awe makini katika hilo. Pia iangalie upotevu wa fedha za Watanzania,” alisema Askofu Shoo.

CWT
Nacho Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilisema uwezekano wa kupatikana kwa mwafaka wa Katiba mpya ni wa mashaka na kwamba, inaweza kupatikana au isipatikane.

Rais wa CWT, Cratian Mukoba, alisema hofu ya kutopatikana kwa Katiba mpya kunatokana na CCM, ambayo imeshikilia msimamo wake wa kujadili maoni ya chama, badala ya wananchi.

Alisema kitendo cha kusema Ukawa hawataki kupata mwafaka siyo cha kweli na kwamba, wanachokitaka ni maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ndiyo yajadiliwe na siyo maoni ya vyama vya siasa.

“Mwafaka unatakiwa wa kujadili maoni ya rasimu ya katiba, ambayo wananchi walitoa humo na hata mimi nilitoa maoni yangu. Hivyo, Ukawa wanachokitaka ni maoni ya wananchi yajadiliwe na siyo vinginevyo,” alisema Mukoba.

Alisema kinachotakiwa kufikiwa sasa ni mwafaka wa kujadili rasimu ya katiba mpya na siyo mabishano na kwamba, kama itashindikana katiba iliyopo itaendelea kutumika.

TAMWA
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimewataka wabunge wa Bunge hilo, ambalo Mwenyekiti wake ni Samwel Sitta kurejea bungeni ili katiba mpya ipatikane.

Mkurugenzi Mtendaji wake, Valeria Msoka, alisema mchakato wa katiba unashirikisha maoni ya wananchi wote, hivyo uwapo wa wajumbe wote wa Bunge hilo unasaidia kupeleka mawazo yaliyotolewa na wananchi.

TUCTA
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya, amesema Katiba mpya haitawezekana kupatikana kutokana na wajumbe waliopewa jukumu hilo kutofahamu wanachokifanya.

Alisema mijadala ambayo ina matusi, kejeli, dharau na itikadi za vyama miongoni mwa wajumbe, haitaweza kuleta katiba mpya licha ya mchakato huo kutumia fedha nyingi za walipa kodi.

“Tukishirikiana tunaweza kupata katiba mpya. Lakini wajumbe bado hawajajua wanachotakiwa kukifanya bungeni. Watanzania milioni 45 waliweka matumaini yao makubwa kwa wawakilishi hawa zaidi ya 600, ambao wangejadili rasimu na si vinginevyo,” alisema Mgaya.
Alisema katiba haitaweza kupatikana pale itakapofikia hatua ya kutafuta theluthi mbili ya kura iwapo Ukawa hawatarudi bungeni.

WASOMI, ASASI ZA KIRAIA
Wasomi, na asasi ya kiraia wamesema iwapo Bunge hilo linalotarajia kukutana mapema mwezi ujao litafanya hivyo bila kuwapo na wajumbe wa Ukawa, rasimu ya katiba mpya itakayopendekezwa itakuwa ni ya wachache.

Wamesema mchakato wa katiba mpya katika hatua ya Bunge hilo kisheria unapaswa kuwashirikisha wajumbe wote kwa kuwa katiba ni ya wananchi na siyo ya kundi fulani la watu au vyama vya siasa.

WASOMI
Mhadhiri wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, tawi la Makumira, jijini Arusha, Elifuraha Laltaika, alisema jana iwapo vikao vya Bunge hilo vitafanyika bila kuwapo wa wajumbe wa Ukawa, hakutakuwa na matokeo ya katiba ya wananchi.

Ametaka nguvu kubwa zifanyike hata kama itabaki siku moja ili kuhakikisha Ukawa wanarudi bungeni, lakini kikubwa zaidi kuhakikisha rasimu inayokwenda kujadiliwa ni ile iliyowasilishwa na Jaji Warioba na si vinginevyo.

“Nafikiri haitakuwa sahihi kuwa na vikao vya Bunge hilo pasipokuwapo na wajumbe wa Ukawa. Na kama watafanikiwa kupitisha rasimu ya katiba itakayopendekezwa inaweza kukataliwa na wanachi katika kura za maoni,” alisema.

Aliongeza: “Lakini wakilazimisha kuwapo kwa katiba mpya basi haitakuwa imetokana na maridhiano ya wananchi, hiyo itakuwa katiba ya wachache.”

ASASI YA SLPC
Mwenyekiti Mtendaji wa asasi ya kiraia ya SLPC, Magesa Mashauri, aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kutambua kuwa katiba ni ya wananchi na siyo ya kundi fulani la watu au vyama vya siasa.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, katika utangulizi wake inasema kuwa katiba ni mali ya wananchi.
“Katika utangulizi huo unaonyesha dhahiri kuwa katiba ni mali ya wananchi na si vinginevyo.

“Bunge Maalumu la Katiba limepewa tu dhamana na wananchi na siyo kwamba, katiba itakayoundwa ni mali yao wenyewe. Vyama vya siasa, kikiwamo chama tawala au wanasiasa wenywe.

“Na pia wajumbe wakumbuke kuwa misingi ya katiba bora imejengwa katika uhuru, haki, udugu na amani,” alisema.
Aliwasihi wanaotumia mabavu ili kupitisha hoja na matakwa yao, waheshimu uhuru, haki, udugu (kuheshimiana na kuthaminiana) ili kuwezesha upatikanaji katiba bora na siyo bora katiba.

“Kutoka na hali hiyo, nawaomba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuacha agenda zao na kujadili rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Mstaafu Warioba ambayo ndiyo imebeba mawazo ya wananchi,” alisema.

JAJI MUTUNGI
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alisema kuwa jitihada za kusuluhisha mvutano uliopo kati ya pande mbili zilizotokana na kugawanyika kwa Bunge hilo zinaendelea na kwamba, wanatarajia kukutana Agosti, Mosi.

“Kwa sasa siwezi kueleza jitihada za usuluhishi zilikofikia, kikubwa fahamu zinaendelea na tumepanga kukutana tarehe moja Julai, tukikamilisha tutawafahamisha,” alisema Jaji Mutungi.

PROFESA BAREGU, DK. MKUMBO:
Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Kitila Mkumbo, kwa nyakati tofauti walisema mpaka sasa mchakato bado umekwama.
Hata hivyo, wanatofautiana kuhusu sababu na jinsi ya kuukwamua ambapo

DK. MKUMBO
Dk. Mkumbo alisema anaunga mkono hatua ya Rais KIkwete kubainisha bungeni msimamo wake juu ya mchakato huo, hasa katika suala la aina ya mfumo wa muungano wa serikali mbili au tatu.

Alisema Kikwete angekuwa Rais wa kwanza wa ajabu duniani kama asingeonyesha msimamo wake na kwamba, pamoja na masuala mengine, huo ndiyo unaotakiwa kujadiliwa na kutumia nguvu za hoja kuonyesha udhaifu wake.

“Wamkosoe au wamuunge mkono kwa hoja, Bunge liendelee lakini kwa sasa wengi wana mihemuko ya uchaguzi mkuu ujao, Bunge hili liahirishwe ili Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liendelee na lifanyie marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Dk. Mkumbo.


PROFESA BAREGU
Profesa Baregu alisema kiini cha mchakato wa katiba ni hekima na msimamo wa Rais Kikwete, kinyume cha chama chake cha CCM na kwamba, umevurugwa na yeye mwenyewe kugeuka kimsimamo.

“Labda kama hakufahamu hadhi na matendo yake akiwa kwenye nafasi ya urais, alipopokea na kusaini rasimu ya kwanza na ya pili ya katiba ilimaanisha kuwa na msimamo mmoja na yaliyomo,” alisema Profesa Baregu.

Aliongeza: “Kuibuka na kupinga rasimu hiyo ni kuvua joho la urais, kuvaa la CCM bila kujali kuwa ni kiongozi wa Watanzania siyo wana CCM hivyo ifahamike kuwa mwenye mamlaka na wajibu wa kurudisha mchakato reline ni Rais Kikwete tu.”

Profesa Baregu, ambaye ni mtaalamu mbobezi wa usuluhishi wa migogoro kimataifa, alimtaka Rais Kikwete kutohofia CCM katika suala hilo zito kitaifa, akisema ingawa ndicho kilimdhamini katika wadhifa wake siyo pekee kilichopigia kura.

MBUNGE MACHALI
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema matumaini ya taifa kupata katiba mpya yanapungua na kwamba, hata kama Bunge hilo litaendelea bila Ukawa kushiriki, katiba itakayopendekezwa itakataliwa kwa kura ya maoni.

Alisema kasoro inayoendelea kukoroga Bunge hilo ni ya kisheria.“Sheria ingezuia wajumbe wa Bunge Maalum kugombea nafasi yoyote ya uongozi, hali ingekuwa tofauti kwa sababu kusingekuwa na mgongano wa kimaslahi,” alisema Machali.

Alisema ingefahamika kuwa wanaotunga katiba wanalenga kupata mwongozo wa namna ya viongozi kuongoza wananchi, huku wao pia wakifahamu watakuwa miongoni mwa watakaoongozwa hali ingekuwa tofauti na kwamba, ingepatikana katiba bora kuliko inavyotarajiwa.

SPIKA BUNGE LA WANAFUNZI UDOM
Spika wa Bunge la Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (Udom), Mesanga Thobias, alisema la msingi pande mbili za Bunge hilo zinazopingana zitambue kuwa taifa linahitaji katiba mpya na haitakuwa rahisi kuendelea na katiba ya sasa inayosubiriwa kwa hamu iondolewe.

Alisema kwa hali ilivyo na muda uliosalia kufikia siku ya Bunge hilo kurejea tena kwenye vikao, ni dhahiri kuna hatihati ya taifa kupata katiba mpya na kwamba, hilo likitokea, hafahamu nchi itakuwa katika hali gani.

“Kuliko kuendelea na katiba ya sasa, ambayo wengi hatuihitaji tena, bora waafikiane ipatikane katiba nyingine hata kama haitakuwa na ubora uliotarajiwa, itakuwa mwanzo wa hatua ya kuelekea mabadiliko,” alisema Thobias.

CHIMBUKO LA MGOGORO
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa vyama vinavyounda Ukawa walisusia kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na Chama Cha Mapinduzi dhidi ya vyama vingine.

Wajumbe hao wanaounda umoja huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni za ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.

Msimamo huo ulitolewa siku hiyo jioni na Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa Lukuvi alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma.

Profesa Lipumba alisema Lukuvi aliyemwakiisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa mshahara wanajeshi, Jeshi litachukua nchi.

Alisema kauli hizo zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa na kuundwa katiba moja.
Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini wa dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni Tume iliyoundwa na Rais.

UBAGUZI
“Na Waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda…Mheshimiwa hii inasikitisha na inasikitisha kwa kuwa kauli hii pia inafanana na kauli ambayo Rais Jakaya Kikwete aliitoa wakati akitoa hotuba katika bunge hili,” alisema.

“Hii ni Rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba, lakini katika mjadala wetu hapa umekuwa na utaratibu wa ubaguzi, watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la ‘Intarahamwe’, hii ni hatari kwa nchi yetu,
“Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo, hii hatuitaji katika nchi yetu, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa, bila kujali, rangi zetu, makabila yetu, dini zetu, hii ndiyo nchi aliyotuachia Mwalimu Nyerere,” alisema.

“Kutokana na hali hii, tumechoka kusikiliza matusi, tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Interahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania…hili hatulikubali, hatulikubali, tunawaachia, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia Interahamwe muendelee na kikao chenu,” alisema.

“Hatuwezi kuwa sehemu ya Interahamwe,” alisema Profesa Lipumba na baada ya kumaliza kuzungumza, wajumbe wote wa Ukawa na wengine walisimama na kuondoka ndani ya ukumbi huku wakipiga kelele.

Baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku wajumbe wa kundi hilo linalojumuisha vyama hivyo pamoja na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, huku wakiimba nyimbo mbalimbali. “Tunaondoka, tunawaacha Interahamwe, Interahamwe.”

LUKUVI NA KANISA
Alitaja sababu nyingine iliyowafanya watoke nje ya ukumbi wa Bunge wakati mjadala ukiendelea ni hatua ya Lukuvi kuzungumza ndani ya kanisa, akieleza kuwa ulikuwa ni mkakati maalum wa kuwabana Wazanzibari.

Profesa Lipumba aliwataka wajumbe hao kuhudhuria kikao cha pamoja kitakachofanyika leo kwa ajili ya kuweka mikakati ya nini cha kufanya.

TUTARUDI IWAPO…
Baada ya kikao hicho, Prof. Lipumba alipoulizwa na waandishi wa habari kama Ukawa wamesusia moja kwa moja Bunge la Katiba, alisema wanaweza kurudi endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika Rasimu iliyopendekezwa na Tume ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali tatu.

MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni wataathiri upitishaji wa katiba kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi kisichozidi siku moja.

Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Ibara ya tatu inasema pale mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti ya fasiri ya (2).

Ibara ya Nne inaeleza, endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati ya mashauriano ili kupata muafaka.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwapo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: