Advertisements

Friday, July 25, 2014

Jaji Mahakama Kuu adai fidia mil.300/

Jaji Grace Mwakipesile wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, amewafikisha mahakamani watu wawili na Kampuni ya Bima ya Zanzibar Corporation, akiwadai Sh. milioni 300 kama fidia kufuatia majeraha na maumivu ya mwilini aliyoyapata kutokana na ajali iliyosababishwa kwa uzembe wa mdaiwa wa kwanza, dereva Kamota Hassan.

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepangwa kusikilizwa mbele ya Hellen Riwa.
Mbali na Kampuni ya bima ya Zanzibar na Hassan mlalamikiwa mwingine ni, Michael Mosha.

Katika Madai ya msingi, Jaji Mwakipesile anadai kuwa Septemba 31, mwaka 2011 katika barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza katika kijiji cha Bubihi Wilaya ya Kishapu Shinyanga akiwa kwenye gari lenye namba usajili STJ 1870 Toyota Land Cruiser liligongwa na Fuso yenye namba za usajili T 683 AKA.

Hati hiyo ya madai imeeleza kwamba, siku ya tukio mdaiwa wa kwanza, akiwa dereva wa fuso, alikuwa akiendesha gari hilo kwa uzembe iliyowekewa bima na mdaiwa wa tatu.

Alidai kuwa baada ya gari aliyokuwa akisafiria kugongwa na fuso ilimsababishia mlalamikaji majeraha na maumivu makali kutokana na uzembe wa mdaiwa wa kwanza aliyekuwa kwenye mwendo mkali huku akitumia upande wa kulia wa barabara hiyo badala ya kushoto.

Kwa mujibu wa hati hiyo, mdaiwa wa kwanza alishindwa kusimama kwa kukanyaga breki kuzuia ajali hiyo na kwamba alishindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani. Jaji aliendelea kueleza kupitia hati hiyo kwamba siku ya tukio fuso hiyo ilikuwa na bima iliyokatwa na mdaiwa wa pili Mosha ya Januari 31 mwaka 2011 hadi Januari 30, mwaka 2012 .

Ilidaiwa kuwa mdaiwa wa tatu, anahusika kisheria kutimiza matakwa ya uamuzi au hukumu ambayo inaweza kutolewa na mahakama na kwamba ameunganishwa katika kesi hiyo kama mhusika wa ziada.

Kutokana na ajali hiyo, Mdaiwa alipelekwa hospitali ya Shinyanga kwa matibabu ya haraka kutokana na majeraha aliyoyapata miguuni na mikononi pamoja na sehemu mbalimbali za mwili na baadaye alihamishiwa Taasisi ya Mifupa (Moi), kwa ajili ya matibabu ya haraka kwa muda wa miezi sita.

Aidha kutokana na majeraha na maumivu hayo, mdai alikosa amani, alipata usumbufu na uwezo wa kufanya kazi umepungua kwa kiasi kikubwa hivyo anastahili kulipwa fidia hiyo.

Awali mdaiwa wa kwanza alishitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga kwa kosa la kusababisha maumivu kwa njia ya uendeshaji hatari na alihukumiwa kwenda jela miaka mitano na kulipa faini.

Hukumu hiyo ya mdaiwa wa kwanza haijapingwa hadi kesi hii ya madai ilipofunguliwa mahakamani hapo.Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa Agosti 4, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: