Advertisements

Wednesday, April 23, 2014

WATANZANIA WAISHIO GENEVA-USWISI (TAS) WATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa  Tanzania Dkt Agnes Kijazi akikabidhi baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Chama cha Watanzania Waishio Geneva-USWISI (TAS).

 Chama cha Watanzania waishio Geneva wametoa mchango wa  vifaa ikiwa pamoja na  tank la kuhifadhia maji,viti na meza za kusomea, jiko la gesi na mtungi wa Gesi ili kusaidia watoto wa kituo cha Amani Orphanage Centre. Msaada huo uliwasilishwa kwa niaba ya TAS na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt Agnes Kijazi.  Akiwasilisha mchango huo kwa niaba ya TAS, Dkt Kijazi alielezea upendo walionao watanzania hao kwa  kuwakumbuka watoto wa kituo cha Amani. Alisema upendo huo ni mfano wa kuigwa kwa watanzania waishio ndani na nje ya nchi. Kwa upande wa watoto Dkt. Kijazi aliwahakikishia kwamba  TAS na TMA wanawapenda. Alichukua fursa hiyo kuwakumbusha upendo ambao umeonyeshwa kwao na wanawake wa TMA kwa kuwasaidia baadhi ya mahitaji yao.
Watoto wa kituo cha Amani Orphanage Centre wakifurahia baadhi ya vifaa vilivyotolewa na TAS

Aidha Dkt Kijazi alisema  TAS wameendelea kuonyesha moyo wa upendo kwani hivi karibuni wametoa msaada wa fedha (Tshs 500,000) kwa Mama Aida wa Mbeya aliyejifungua wototo wanne mwanzoni mwa mwaka huu. Msaada huo uliwasilishwa kwa niaba ya TAS na meneja wa TMA kanda ya nyanda za juu kusini magharibi Bwana Issa Hamad.
Akipokea msaada huo msimamizi na mwanzilishi wa kituo cha Amani Bi. Margareth Mwegalawa  aliwashukuru watanzania wote waishio Geneva kwa kuwakumbuka watoto wa Amani hata kuwawezesha kupata baadhi ya mahitaji waliokuwa wanahitaji, na alimuomba Dkt Kijazi kuwasilisha salamu hizo kwa kusisitiza msaada huo sio mdogo bali ni mkubwa sana kulingana na uhitaji wake. Bi. Magreth alisema kituo chicho kina watoto 37 wakiwa wasichana 25 na wavulana 12 wenye umri kati ya mwaka mmoja (1) na miaka kumi na tano (15).

Akizungumza kwa niaba ya watoto wa Amani Orphanage Centre mtoto Beatrice Phine alisema sote tunafurahi kwa kupata tank la maji, viti na meza ambavyo vitaboresha maisha yetu na mazingira ya kusomea. Alimuomba Dr. Kijazi awafikishie salaam zao za upendo na shukrani kwa TAS.

No comments: