Advertisements

Thursday, April 17, 2014

Uraia Pacha na Uzalendo

Katika siku zilizopita suala la uraia pacha lilikuwa gumzo kwa Watanzania waishio kwenye Diaspora na wale waishio Tanzania. Lengo kubwa la gumzo au mjadala huu lilikuwa ni kujadili kama uraia pacha unaweza kuruhusiwa kwa raia yeyote wa Tanzania au kwa mtizamo mwingine, na lengo ni kuelimisha umma kuwa mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania na atakayepata uraia wa pili hawezi kupoteza haki yake ya kuwa 

Mtanzania. Suala hili bado linajadiliwa na Watanzania lakini bado wapo Watanzania wanaopinga uraia pacha kwa kudai kuwa Watanzania waishio ughaibuni hawana uzalendo au “patriotism”. Nimeonelea ni vizuri kulijadili suala hili la uzalendo kwa vile Watanzania wengi wa ughaibuni na wale waishio Tanzania bado wanaamini kuwa si kweli kuwa Watanzania wa Ughaibuni hawana uzalendo na hapa natoa mifano iliyotolewa katika kuthibitisha ukweli huu. 

Kwa kuanzia ingekuwa vizuri dhana ya uzalendo ieleweke vizuri. Pili, dhana ya nani ni mzalendo na nani si mzalendo itawekwa bayana na mwisho, namna ya kupima uzalendo wa Watanzania waishio Tanzania na nje ya Tanzania itaelezwa kwa kifupi. 

Tunaanza na uzalendo na umaana wake. Uzalendo yaani “patriotism” ni hali ya kuwa mtii kwa taifa kwa maana ya kutii, kulinda na kutetea misingi iliyounda taifa. Kwa kifupi kabisa na bila kuchanganya mambo uzalendo ndio huu. Kwa mantiki hii, kuilinda na kuitetea misingi iliyounda taifa na hata kuhakikisha kuwa taifa halifi humfanya raia awe mzalendo. Lakini raia anaweza kuwa mzalendo kwa taifa lake na kutokuwa mzalendo kwa serikali au chama tawala. Na anapokosa uzalendo kwa serikali au chama tawala anaweza kubakia mzalendo kwa taifa lake. Mantiki ya kuwa na vyama vingi vya kisiasa ndio hii. Hivyo uzalendo huwa ni kwa taifa na sio kwa chama au serikali tawala. Kwa kuelezea hili, mimi mwandishi wa article hii sina chama cha siasa na naomba nisieleweke vibaya kwa chama tawala cha CCM kwa sababu natoa mifano tu ambayo inapatikana duniani kote na sina vita na CCM wala serikali yake na sina vita na chama chochote cha kisiasa. Natoa tu maelezo ya kiutaalamu, kwa sababu mimi ni mtaalamu wa masuala haya. 

Neno uzalendo yaani “patriotism” lilishika hatamu wakati wa kale ambapo nchi na serikali zililazimisha raia wafuate dini moja kwa misingi ya kujenga taifa na utaifa. Watawala walifikia hata kuwauwa wale waliokataa kuwa na dini ya kitaifa hasa kule Ulaya. Na mtu aliyefuata dini ya nchi ambayo kwa kawaida ilikubalika na serikali au watawala alionekana kuwa na uzalendo kwa nchi yake na yule aliyekataa kufuataa dini inayotambulika na nchi na serikali alionekana kukosa uzalendo. Baada ya usumbufu huu, baadhi ya raia wa Mataifa ya Ulaya walipinga mfumo huu na walipigania masuala ya dini na siasa yatenganishwe. Na kwa nchi za Ulaya ndipo ukawa mwanzo wa kutenganishwa kwa dini na siasa. Kwa lugha ya kitaalamu kwa mazingira ya Ulaya tunasema “separation of church from the state”, ili kila mtu apate uhuru wa kuabudu.

Kwa nchi za Kiafrika, uzalendo uliongezeka sana wakati wa kumfukuza mkoloni kutoka kwenye ardhi ya Afrika. Kila Mwafrika alikuwa na lengo na dhumuni moja, kukataa kutawaliwa. Na kauli mbinu ya Waafrika ilikuwa moja na ilisikika katika kona zote za bara la Afrika kauli hiyo ilikuwa ni “Uhuru” ambayo ilisemwa katika lugha tofauti za Kiafrika. Kwa mfano, hata Afrika ya Kusini wakati wa “Apartheid” uzalendo uliongezeka na raia waliungana kuupinga kwa nguvu zote wakiwapinga makaburu. Kwa Tanzania, uzalendo uliongezeka wakati wa vita vya kumng’oa Nduli Iddi Amini na wakati wa nguvu kazi wakati wa vijiji vya ujamaa.

Uzalendo vile vile hupotea. Raia anayeishi ndani au nje ya nchi anaweza kuwa au anaweza vile vile kukosa uzalendo. Mifano ni kama ifuatayo. Kama kuwa mzalendo ni kuwa mtii kwa taifa lako na kuilinda misingi ya taifa lako, pale raia au afisa wa serikali anapokuwa mbadhirifu wa mali ya umma ana uzalendo? Nadhani jibu ni la hasha au hapana. Mtu huyu au afisa huyu hana uzalendo. Kumbe raia aliye “corrupted” hana uzalendo kwa taifa lake. Na raia huyu anaweza kuwa anaishi ndani au nje ya mipaka ya nchi yake lakini kwa kuwa sio mwaminifu kwa taifa lake, anakuwa si mzalendo.

Mfano wa pili, raia aishie ughaibuni ambaye ni mtii kwa taifa lake na hayupo “corrupted” na anayesaidia ndugu zake kwenye nchi aliyotokea kwa hali na mali, je huyu sio mzalendo? Jibu ni kuwa huyu ni mzalendo.

Nadhani mifano hii ya awali inawafumbua macho kuhusiana na nani ni na nani sio mzalendo kwa taifa lake.Kwa maana hiyo, uzalendo peke yake hauwezi kuwa kigezo cha kuwanyima Watanzania uraia pacha kwa sababu hata Mtanzania aishiye Tanzania na ambaye hajawahi kutoka nje ya nchi anaweza kukosa uzalendo vile vile.

Mfano wa mwisho ni kuwa uzalendo vile vile unaweza kupungua au kuongezeka kufuatana na nyakati. Hivyo matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanaweza kuua au kuhifadhi uzalendo alionao raia. Hivyo sio kweli kuwa uzalendo wa kila raia bila ya kujali anaishi ndani au nje ya mipaka ya nchi yake hubakia vile vile maisha yake yote mpaka mauti yamtoe duniani. Uzalendo huweza kupungua au kuongezeka au kupotea kabisa. Hivyo suala kumnyima Mtanzania wa ughaibuni haki yake ya kuzaliwa Tanzania na haki ya uraia pacha kikatiba kwa misingi ya uzalendo peke yake ni sababu isiyo na msingi wala umaana wowote.

Nadhani kwa maelezo haya dhana hii ya uzalendo inaeleweka na naamini haitatumika kama kigezo cha kimsingi nambari wani cha kuwakatalia Watanzania haki yao ya kiubinadamu ya kupata uraia pachja na haki yao ya kuzaliwa Tanzania inayowapa haki ya kuwa Watanzania kikatiba. 

Imeandaliwa na Deogratius Mhella, Katibu wa Vikao vya Viongozi wa Jumuiya za Watanzania na DICOTA kwa lengo la kuelimisha Watanzania kuhusu suala la uraia pacha katika jitihada za Watanzania wa Ughaibuni kuendeleza mdahalo wa Uraia pacha ili Bunge Maalumu la Katiba liweze kuingiza suala la uraia pacha kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1 comment:

Anonymous said...

Good comments Katibu Mhella.