Advertisements

Friday, April 18, 2014

MUMEO AKIKUSALITI MARA MOJA, UKIMUACHA IMEKULA KWAKO!

WIKI iliyopita nilimalizia makala iliyokuwa inazungumzia mambo ambayo unatakiwa kuyaepuka ndani ya ndoa yako ili kuifanya iwe ya furaha na amani.

Wapo ambao waliona ugumu katika kutekeleza baadhi ya mambo. Kwa mfano, kuna ambao walinipigia simu na kuniambia, licha ya kwamba wanajua wake zao hawapendi masuala ya pombe lakini inakuwa vigumu kwao kuacha.

Kuna ambao wanajua wake zao hawapendi wao wachelewe kurudi nyumbani lakini wao wameshajijengea katabia ka’ kukaa kijiweni kwanza kupiga stori kabla ya kurudi nyumbani.

Kimsingi kila mmoja alisema lake lakini nashukuru wapo walionielewa na kuona yote niliyoandika ndiyo ambayo yamekuwa yakisababisha wanandoa wengi kutofautiana na hatimaye kuifanya furaha itoweke.

Mimi nadhani ifike wakati tukubali kuacha baadhi ya tabia ambazo tunajua fika zinawakera wenza wetu. Inaweza kuwa ngumu kuacha mara moja lakini naamini ukiwa na dhamira ya kubadilika, utaacha pombe, utawahi kurudi nyumbani, utaachana na marafiki ambao mwenza wako hawataki, n.k.
Baada ya kusema hayo sasa nirudi kwenye mada yangu ya wiki hii. Ndugu zangu, usaliti umekuwa ukitokea kila siku. Haiwezi kupita siku bila kusikia mume wa fulani kafumaniwa na fulani. Mafumanizi yamekuwa yakitokea kila kukicha.

Elimu ambayo nimedhamiria kuitoa leo hasa kwa wanawake ni kwamba, kama kweli mumeo unampenda na siku moja ukagundua amekusaliti, hiyo isiwe sababu ya wewe kuchukua hatua ya haraka kuomba talaka kwa kudhani umekukosea sana.

Kuna wengi ambao waliwafumania waume zao, wakazua vurugu na kujeruhi, lakini wakajikuta hawakukomesha tatizo, zaidi ya kuwapa usugu waume zao kuendeleza wizi tena kwa kejeli.

Katika hali ya kawaida usaliti ni jambo linalouma kwa kiwango kikubwa. Hakuna suala la kuazima mume wala mke katika maisha, watu huazimana magari na pesa lakini mpenzi, hakuna jasiri wa namna hiyo!

Swali ni je, ukimfumania leo mpenzi wako au mkeo au mumeo ni sahihi kuchukua hatua ya kumuacha mara moja? Wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, siyo sahihi hata kidogo na kama utafanya hivyo ipo siku utaumia sana na kujutia uamuzi wako.

Atakusaliti, utaamua kumuacha kwa kuona hajatulia lakini yawezekana kateleza tu na ungeweza kumpa nafasi nyingine na nyingine kabla ya kumuacha.

Inaelezwa kuwa, madhara ya kumuacha baada ya yeye kukusaliti ni makubwa kwani ukifanya hivyo ipo siku utakutana na huyo mumeo akiwa na yule mwizi wako wakiwa kwenye mapenzi mazito.

Mbaya zaidi wanaweza kukufanya mashauzi, wakashikana kimahaba na kubusiana mbele yako ili tu kukurusha roho. Kibinadamu lazima utaumia kama kweli ulikuwa unampenda. Utatamani umrudishe kwenye himaya yako lakini tayari ameshahamishia penzi kwa mtu mwingine.

Ndiyo maana tunatakiwa kuwa makini sana pale tunapohisi au kubaini kusalitiwa. Tuweke hasira pembeni, tufanye uchunguzi na kubaini ukweli ili tujue hatua sahihi za kuchukua.
Najua huwezi kuchukulia poa endapo utabaini kuna mtu anakuchovyea penzi lako lakini suluhisho si kumuacha.

Kama kweli unampenda kwa dhati na una imani ndiye mtu sahihi katika maisha yako mpe nafasi nyingine.
Katika hili pia naomba niseme kwamba, tunakosea sana pale tunapowafikiria tofauti wenza wetu. Kusaliti ni kitu kibaya sana na kwa maana hiyo kama utamwambia mumeo kuwa anakusaliti wakati siyo kweli, unamfanya ajisikie vibaya sana.

Ataamini huna imani naye na matokeo yake mapenzi lazima yatapungua. Yawezekana pia hata kama alikuwa hajawihi kukusaliti, akaanza kufikiria kufanya hivyo, jambo ambalo ni baya sana.

Kikubwa ni wawili waliotokea kupendana kuaminiana na kupeana nafasi ya kukosea mara moja. Kosa moja lisiwe sababu ya ndoa yenu kuparaganyika. Ikitokea hivyo hata watu wa pembeni watajua hamkuwa na mapenzi ya dhati bali mlikuwa mnatafutiana sababu tu ili muachane na hakika mtachafuka katika jamii yenu.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo...

GPL

No comments: