Advertisements

Friday, April 18, 2014

Mbowe kuwateua Cuf, NCCR Baraza Kivuli


Tumekuwa na mazungumzo na wenzetu na hili jambo ni moja ya mambo ambayo tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande unahitaji mwenzake katika kuikomboa nchi hii”  Freeman Mbowe,Mwenyekiti wa Chadema( katikati) 
Kwa ufupi
  • Baraza la Kivuli la sasa linawajumuisha wabunge kutoka Chadema pekee, ambacho kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni tangu kuanza kwa Bunge la 10, Novemba 2010.

Dodoma. Mvutano katika mchakato wa Katiba umeimarisha ushirikiano wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na sasa kuna mpango wa kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri Kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama hivyo.
Baraza la Kivuli la sasa linawajumuisha wabunge kutoka Chadema pekee, ambacho kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni tangu kuanza kwa Bunge la 10, Novemba 2010.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alithibitisha kuwapo kwa mpango huo na
kwamba atapanga upya baraza lake katika siku za mwanzo za Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
“Tumekuwa na mazungumzo na wenzetu na hili jambo ni moja ya mambo ambayo tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande sasa umekubali kuwa unahitaji mwenzake katika harakati za kuikomboa nchi hii,” alisema Mbowe.
Taarifa za kuwaingiza wabunge wa NCCR-Mageuzi na CUF katika Baraza la Mawaziri Kivuli, imekuja wakati ambao vyama hivyo pamoja na wajumbe wengine kadhaa wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa ndiyo iliyowaongoza baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka nje juzi kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana na kile ilichodai kuwa ni kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alithibitisha kuwapo kwa mpango huo: “Kweli ninafahamu kuwapo kwa mpango huo, lakini niseme tu kwamba mazungumzo haya hayakuanza sasa, yamekuwapo kwa muda mrefu kuona namna ya kushirikiana,” alisema Mbatia.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipoulizwa hakukanusha wala kukubali kuhusu kuwapo kwa mpango huo, badala yake alitaka atafutwe Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Akizungumza kupitia simu yake ya mkononi, kiongozi wa wabunge wa CUF, Habib Mnyaa alisema hakuwa akifahamu chochote kuhusu mpango huo kutokana na kutokuwepo nchini kwa siku kadhaa.
Pigo kwa CCM
Kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wa kisiasa hasa baina ya CUF na Chadema ni pigo kwa chama tawala, CCM ambacho kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na CUF  Tanzania Visiwani.
Kadhalika, hatua hiyo inavileta vyama hivyo karibu, tofauti na ilivyokuwa awali ambako walionekana kuwa na uhasama wa kisiasa kiasi cha kupingana waziwazi bungeni.

No comments: