Advertisements

Friday, April 18, 2014

Loga kulinda rekodi kwa Pluijm kesho?

Msemaji wa Yanga,Baraka Kizuguto.

Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amesema anakiandaa vizuri kikosi chake ili kiweze kushinda mechi ya kesho Jumamosi watakapokutana na watani zao Yanga, ili kulinda rekodi yake dhidi ya mpinzani wake, Hans van der Pluijm.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka visiwani Zanzibar walikoweka kambi Simba, Logarusic, alisema akiwa na klabu ya Ashanti Gold na Pluijm akiifundisha Berekum Chelsea aliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Logarusic alisema bado anataka kuendeleza heshima kila anapokutana na kocha huyo kutoka Uholanzi kama alivyokutana naye katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Ghana ya msimu wa 2010/ 2011.

"Naomba nipate ushindi, sitaki kuona Pluijm anavunja rekodi yangu," alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa, katika mazoezi yake anawaandaa wachezaji wake kuikabili Yanga kwa njia tofauti ili waweze kutimiza malengo ya kushinda mechi hiyo ya kufunga pazia la ligi hiyo ya Tanzania Bara.

Logarusic alianza vizuri kuikabili Yanga kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe Desemba mwaka jana.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Pluijm, alisema kikosi chake kinajiandaa ili kipate ushindi na kumaliza msimu wa ligi kikiwa na heshima.

Pluijm alisema licha ya ushindani na changamoto zinazotarajiwa kuwapo, bado anaipa nafasi Yanga kuibuka na pointi tatu muhimu kesho.

Tayari Azam imeshatwaa ubingwa wa msimu huu wa 2013/ 2014 huku ikiwa na mechi moja mkononi baada ya kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Yanga iliingia kambini juzi jioni ikiwa na wachezaji wake 20 kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo ambao umepoteza 'msisimko' kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, aliwataja wachezaji nyota wa timu hiyo, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Juma Kaseja, Athumani Iddi, Said Bahanuzi na Shabani Kondo kuwa hawajaingia kambini.

Bahanuzi na Kondo ni wagonjwa lakini sababu za wachezaji hao wengine kutoingia kambini hazijawekwa wazi.

Kizuguto aliwataja wachezaji walioingia kambini kuwa ni; Makipa: Deogratias Munishi 'Dida' na Ally Mustafa 'Barthez',Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Viungo; Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela, Hamis Thabit, na Nizar Khalfani, wakati washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Jerson Tegete, Hamisi Kizza, Hussein Javu na Saimon Msuva.
CHANZO: NIPASHE

No comments: