Advertisements

Friday, April 18, 2014

Kauli ya Interahamwe yamchefua Askofu Mtetemela

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Askofu Donald Mtetelela, ameeleza kusikitishwa kwake na Bunge hilo kuitwa Interahamwe.

Akizungumza bungeni jana, Askofu Mtetemela, ambaye ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana mstaafu, alisema alishangazwa na kauli hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye anaheshimika kimataifa.

Profesa Lipumba juzi jioni alililinganisha bunge hilona kundi la interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda kutokana na kukumbatia na propaganda.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo iliyosababisha wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje, akidai kuwa kauli alizozitoa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Jumamosi iliyopita ni za ubaguzi.

Lukuvi akizungumza katika sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Kanisa la Methodist Dodoma, alisema mfumo wa serikali tatu haufai na kwamba serikali ya Muungano ikikosa mapato itasababisha wanajeshi kukosa mishahara na kuiangusha serikali.

Lukuvi pia alisema kwamba kuruhusu serikali tatu kutasababisha kuibuka kwa siasa kali za Kiislamu upande wa Zanzibar na kuishutumu CUF kuwa inatekeleza siasa za kidini za kikundi cha Uamsho.

Askofu Mtemele alisema kauli ya Prof. Lipumba kuliita bunge hilo kuwa ni Interahamwe hakuwatendea haki wajumbe na kwamba alitaka amuone azungumze naye, lakini ametoka nje na wajumbe wenzake.

“Kutuita Interahamwe ni ubaguzi, Interahamwe ni kundi la wauaji, kutuita sisi ni wauaji siyo nia njema na inaweza kufufua hisia za wananchi wa Rwanda na serikali ya Rwanda kwamba tunatumia Interahamwe,” alisema Askofu Mtetemela. Alihoji: “Kwa nini tuinue suala hili tena linaloibuliwa na kiongozi kama yeye (Lipumba) anayeheshimiwa kimataifa?

Askofu Mtetemela alisema kuwa haikuwa busara kuibua suala hilo kwa kuwa Tanzania na Rwanda zilikuwa na tofauti katika siku za karibuni, hivyo kauli hiyo inaweza kuzorotesha uhusiano baina ya nchi hizo.

Askofu Mtetemela pia alisema siyo busara kuwakashifu waasisi wa Muungano ambao alisema ndiyo walioweka msingi wa utulivu na amani nchini.

Alisema ujenzi wa katiba ni maridhiano. Tuzungumze na tusikilizane, tushauriane na ikiwa kuna jambo tulimalize,” alisema.

“Vyama vyetu vitutajirishe na siyo kutubomoa,” alisema na kuongeza: “Tunapaswa kuangalie yasiyo sahihi ili yarekebishwe.”
CHANZO: NIPASHE

No comments: